CHAMA cha Mapinduzi (CCM), jana Jumapili kimekamilisha
mchakato wake wa kumsaka mgombea wa Urais kwa muhula wa 2015-20.
John Pombe Magufuli ndiye amechukua nafasi
hiyo baada ya kuwazidi wagombea wengine 37 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo
kupitia chama hicho kikongwe nchini.
Magufuli ameshinda nafasi hiyo kwa kishindo
akipata kura 2,104 ikiwa ni asilimia 87%, ushindi ambao unaweza kuuita kuwa ni
wa kishindo sana.
Ushindi huo wa kishindo ndani ya CCM unaweza
kuwa ni dalili nzuri za wazi kwamba Magufuli ana nafasi kubwa ya kuendeleza
ushindi na mwisho kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa awamu ya
tano, hilo linawezekana.
Wakati tukiwa tunasubiri uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu, Magufuli ana mambo kadhaa anapaswa
kuyajua kuhusiana na michezo nchini na hasa soka.
Najua hawezi kukwepa kuizungumzia michezo
wakati wa kampeni zake kuwaomba wananchi wa maeneo mbalimbali wampe kura ili
aibuke na ushindi wa kishindo safari hii kwa Tanzania nzima.
Juzi Jumamosi, niliandika makala kuzungumzia
namna wagombea wa nafasi ya Urais wa CCM walivyokuwa wakiizungumzia michezo
wakati wengi wao hawakuwa washiriki hata kidogo katika michezo hiyo.
Nilifafanua kuhusiana na namna walivyokuwa
wakijaribu kuonyesha wako karibu na michezo kwa kuwa wanajua ina nguvu. Hivyo
walifanya ujanja-ujanja kuonekana ni rafiki wa karibu wa michezo, kitu ambacho
hakikuwa kweli kwa wengi wao.
Magufuli huenda amekuwa rafiki wa michezo
mingine, lakini hakuna ubishi hakuwa karibu na anaonekana si mpenzi sana wa
michezo.
Lakini hana ujanja, wakati wa kampeni lazima
ataizungumzia michezo kwa kuwa ina nguvu kubwa. Lakini pia ina faida kubwa kwa
taifa letu ambalo ataliongoza kama atashinda na hakuna ubishi lazima aifanyie
kazi.
Kwanza nimkaribishe Magufuli kwenye michezo,
kwamba asiidharau na kuona ni kama burudani pekee. Badala yake ajue michezo ni
ajira na kitu kinachoweza kulipa taifa heshima kubwa kama itafuatiliwa na
kufanyiwa kazi na serikali yake kama sehemu ya ajira.
Soka ni kati ya sehemu inayoweza kuwa msaada
kwa serikali katika suala la heshima. Hakuna taifa ambalo halitafurahia kupata
ajira za kutosha kwa wananchi wake.
Kama Magufuli atashinda, basi michezo na
hasa soka litakuwa msaada mkubwa kwa uongozi wake kutatua mambo hayo mawili.
Lakini michezo kwa ujumla ni sehemu kubwa ya kuwasaidia vijana kuepukana na
tamaa au kujiingiza kwenye madawa ya kulevya.
Michezo inaweza kuwa ngao, pia silaha ya
kumsaidia Magufuli katika mapambano yake ya kuliongoza taifa, huku likipunguza
misukosuko ya mambo mengi.
Rais Jakaya Kikwete alionyesha njia kupitia
kuamua kulipa mishahara ya baadhi ya makocha wa soka, riadha, netiboli na
ngumi.
Jambo ambalo lilikuwa zuri, lakini sasa
achana na kuwalipa mishahara tu makocha, badala yake nakushauri kuwekeza katika
soka la vijana, pia kuwekeza katika michezo mingine lakini kwa vijana.
Soka la vijana ni nguzo ya sasa na baadaye.
Tumekuwa tukipiga kelele kuwa lipewe kipaumbele, lakini inaonekana bado hakuna
mwamko wa kutosha.
Kuliko kumpa kocha mshahara wa Sh milioni 24
kwa mwezi. Vema fedha hizo zikaingia kwenye kukuza watoto ambao watakuja kuwa
watumishi wa klabu zao, timu zetu za taifa na baadaye makocha wazuri
watakaolitumikia taifa.
TFF, vyama na mashirikisho mengine, wawe na
jukumu la kuwalipa mshahara makocha ambao wanawaajiri kupitia wadhamini wao
ambao hakika watakuwa na nafasi ya kufanya hivyo.
Kingine ajitahidi kuimarisha mienendo ya
wizara inayohusika na michezo kiutendaji, pia kibajeti kwa ajili ya kusaidia
michezo. Washiriki wa Tanzania kimataifa kwa kuwa wanawakilisha taifa letu,
watengewe bajeti ambayo itawainua kiuwezo na morali kwa kuwa watajua fedha za
kodi zimetumika kuwapa wao, hivyo wanadaiwa na Watanzania. Najua kuna mengi ya
kuzungumza kuhusiana na michezo, tutakutana wakati mwingine. Kila la kheri.
0 COMMENTS:
Post a Comment