Uongozi wa Yanga umesema kuwa hauna presha na kuondoka kwa kiungo
wa Simba, Emmanuel Okwi mwenye kesi nao huku ukisema kuwa hata angejichimbia
wapi, atapatikana tu kusikiliza kesi yake.
Yanga ilimfungulia kesi Okwi katika Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa) ikimdai kitita cha dola mil moja (Sh bilioni 2) kutokana na
kuvunja mkataba kisha kujiunga na Simba kabla ya kupata shavu barani Ulaya kwa
kujiunga na Sonderjyske ya Dernmark na kusaini mkataba wa miaka mitano mwishoni
mwa wiki iliyopita.
Nyota huyo raia wa Uganda, alitua Jangwani msimu wa 2013/14 na
kuingia kandarasi ya miaka miwili, lakini akaingia kwenye mvutano na klabu hiyo
kwa kile kilichodaiwa hakulipwa fedha za usajili ambazo ni dola 40,000, lakini
Yanga wakapinga na kumfungulia kesi Fifa.
Mwanasheria wa Yanga, Frank Chacha, ameliambia Championi Jumatatu
kuwa, hawana presha na kuondoka kwake na hata angekwenda wapi lazima apatikane
kusikiliza kesi yake.
“Suala la kuuzwa kwake sisi hatuna shida nalo. Cha msingi ni
kwamba madai yetu yapo palepale na kesi ipo palepale huko Fifa. Hata angekwenda
Marekani, Ufaransa hawezi kukwepa hilo. Kila kitu tulikamilisha na jalada la
kesi limeishafunguliwa, hivyo tunachosubiri kwa sasa ni Fifa kutupa majibu na
kutuambia ni lini kesi itasikilizwa,” alisema Chacha.
0 COMMENTS:
Post a Comment