MSUVA AKISAINI MBELA YA KATIBU MKUU DK JONAS TIBOROHA NA JEMBE JINGINE LA USAJILI LA YANGA, ISAAC CHANJI. |
Kama amemkomesha baba yake mzazi vile, winga Simon Msuva amesaini mkataba
mwingine wa miaka miwili ya kuendelea kuichezea Yanga inayojiandaa na Kombe la
Kagame, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Awali, baba wa winga huyo, Happygod Msuva, alimzuia mwanaye
kusaini mkataba mwingine wa kuendelea kuichezea Yanga, badala yake aende Simba
akapate changamoto mpya.
Baba yake Msuva mwenye mapenzi na Simba, alitaka kuona mwanaye anajiunga
na timu hiyo kwa madai ameshaifanyia Yanga vitu vingi ikiwemo kuipa ubingwa wa
ligi kuu msimu uliopita.
Msuva alisema ameingia makubaliano ya kusaini mkataba wa miaka
miwili baada ya timu yake kumtangazia ofa nzuri ya mshahara na dau nono la
usajili.
Msuva alisema, kabla ya kusaini mkataba huo wa miaka miwili,
alikuwa amebakiza mwaka mmoja, hivyo jumla sasa ana mkataba wa miaka mitatu utakaomalizika
2018.
“Hizo timu zinazoninyemelea
kwa hivi sasa za hapa nchini, naomba ziniache kabisa kwani nimeshaongeza mkataba
mwingine wa miaka miwili na Yanga kufikisha jumla ya miaka mitatu.
“Nimesaini Yanga bila ya kushawishiwa na mtu yeyote na kikubwa
kilichonibakiza Yanga ni ofa nzuri niliyopewa,” alisema Msuva.
Kuhusu kauli za baba yake, Msuva alisema: “Hizo taarifa za baba
kutaka kunipeleka Simba naomba kwa sasa ziishe na ninaomba ieleweke kuwa, mimi
ninacheza soka kama kazi haihusiani na ushabiki wa baba kwa Simba.”
Msimu uliopita wa ligi kuu kiungo huyo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji
bora akipachika mabao 17, pia akatwaa uchezaji bora wa msimu mzima.
0 COMMENTS:
Post a Comment