July 17, 2015


Kocha wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, ameonekana kuwa na uchu wa timu yake kufunga mabao mengi msimu ujao baada ya kila siku kuwafundisha wachezaji wake jinsi ya kutumia nafasi za kufunga kila wanapozipata.


Simba ambayo imepiga kambi wilayani Lushoto jijini Tanga, imekuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Sekomu, ambapo Kerr amekuwa akiwakazania zaidi wachezaji wake kufunga mabao ya mbali ambayo ni nje ya 18.

Kwa muda mrefu katika kikosi hicho, mabao ya aina hiyo yalikuwa yakifungwa na Mganda, Emmanuel Okwi aliyetimkia Denmark, moja likiwa ni lile alilomtungua kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’, msimu uliopita.

Lakini hivi karibuni kocha huyo ameonekana kuanza kuwajenga wachezaji wengine kwa kufanya hivyo.

Katika mazoezi ya timu hiyo, Kerr alionekana kutofurahia sana mabao ambayo yalikuwa yanafungwa ndani ya eneo la 18, akisisitiza wachezaji kufunga nje ya eneo hilo.

Kerr ameiambia SALEHJEMBE kuwa, mchezaji si lazima afunge bao akiwa karibu na goli bali ni kokote pale endapo tu akipata nafasi.

“Nawaandaa wachezaji wangu si kwa ajili ya kufunga tu bali hata kukaba ili kabla msimu ujao haujaanza, kikosi chote kiwe tayari kwa kupambana na wala sitaki kuona huku pazuri halafu kwingine pabovu.

“Pia kwa upande wa kufunga kama ulivyoona kila mchezaji namjaribu kufanya hivyo nikiwa na maana kwamba hakuna wa kumtegemea mmoja, lakini nataka wafunge mabao hayo kwa umbali wa mita 18 kama akipata nafasi ya kufanya hivyo.


“Kusubiri mpaka afike karibu na goli ndiyo afunge si sahihi kwani tunaweza kukutana na wapinzani ambao wao wamekuja kwa ajili ya kulinda lango lao tu,” alisema Kerr.  

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic