Mabeki wa
kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani, wamejikuta wakipewa
majukumu mazito na benchi la ufundi la timu hiyo, kisa kikiwa ni habari za safu
kali ya ushambuliaji ya Gor Mahia ya Kenya.
Timu hizo
zinatarajiwa kukutana kesho katika mechi ya ufunguzi ya michuano ya Kombe la
Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo kumekuwa na taarifa kuwa safu
ya ushambuliaji ya Gor Mahia ipo vizuri.
Baada ya
habari hizo, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi,
aliamua kufanya kazi nzito kwa mabeki wake hao ili wawe fiti licha ya kuwa
alikuwa akitoa mbinu mbalimbali kwa wachezaji wake wote kuelelekea kwenye mtanange
huo wa ufunguzi.
Imeeleza
kuwa mbali na mbinu wanazopewa lakini wametakiwa kuwa makini muda wote na
kutofanya utani hata kidogo kwa kuwa watu wanaokutana nao ni washindani wakali
na wajanja katika ufungaji.
Mmoja wa
wachezaji wa Yanga amesema amesema kuwa, baada ya Pluijm kupata taarifa hizo, ndipo akawa na zoezi hilo
kali.
“Kutokana
na taarifa hizo, kocha alifanya mazungumzo na sisi na kututaka tuwe makini
zaidi na tucheze kwa ushirikiano mkubwa lakini pia akawataka mabeki wote
wakiwemo Yondani na Cannavaro, kuhakikisha hawafanyi makosa ya kizembe,”
alisema mchezaji huyo.
Mechi hiyo
itakuwa ya kwanza kuzikutanisha timu hizo mbili baada ya miaka 16, mechi ya
mwisho kuzikutanisha timu hizo, Yanga ililala kwa mabao 4-0 na ilikuwa ni ya kutafuta mshindi wa tatu
wa michuano hiyo iliyofanyika nchini Kenya.
Akizungumzia
mchezo huo wa ufunguzi, Pluijm alisema: “Tunatambua kuwa wana kikosi imara
lakini sisi pia tupo imara na hatutaidharau hata kidogo mechi hiyo na ndiyo
maana tumepanga kuanzisha kikosi imara ili tupate ushindi.”







0 COMMENTS:
Post a Comment