NGOMA... |
STRAIKA mpya wa Yanga aliyetawala kwenye
vinywa vya mashabiki kwa sasa, Mzimbabwe, Donald Ngoma leo anafikisha siku ya
nne katika mazoezi ya timu hiyo lakini kikubwa kinachozidi kukuza jina lake ni
makali anayoendelea kuyaonyesha kikosini hapo.
Ngoma ambaye ametua Yanga kwa mkataba wa
miaka miwili akitokea FC Platinum ya Zimbabwe awali alifanya mazoezi na timu
hiyo wiki iliyopita kwa siku mbili mfululizo kabla ya kuelekea kwao kukamilisha
baadhi ya vitu na kurejea kazini juzi na jana akaanza rasmi mazoezi huku
akizidi kuonyesha kuwa yeye ni bora.
Mchezaji huyo ‘aliyeenda hewani’ amekuwa
akizidi kumshawishi Kocha wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van der Pluijm kwa
kubainisha kwamba ana vitu vingi anavyopaswa kuwa navyo straika wa uhakika huku
jitihada zake zikionekana kuwazidi kiaina baadhi ya nyota wengine kikosini hapo
wakiwemo Kpah Sherman na Hussein Javu.
Katika siku hizo tatu alizohudhuria mazoezi,
mshambuliaji huyo amefanikiwa kuonyesha wazi vitu sita vya msingi ambavyo kama
ataendelea kuwa navyo katika siku za usoni, basi ni ngumu kwa jina lake
kufutika mapema kwenye ramani ya soka nchini na Yanga watafurahia matunda yake
miaka yote atakayoitumikia timu hiyo, hakika unaweza kusema hakuna atakayekuwa
bora kama yeye:
Anaweza kulinda mpira
Ngoma anajua kulitumia vema umbo lake na
kuwatesa mabeki linapokuja suala la kuudhibiti na kuuficha mpira pale
inapotokea. Mara kadhaa anapopewa mipira
kwenye msitu wa mabeki, kwake imekuwa si tatizo kwa kuwapa mwili na kusumbuana
nao kwa nguvu huku akiendelea kuulinda mpira aliopewa usipotee huku akitafuta
upenyo wa kuwatoka, kupiga shuti ama kutoa pasi.
Ni hatari kwenye vichwa
Katika upande wa kucheza krosi pia amekuwa
na ubora wake katika hilo baada ya kufanikisha kuruka sambamba na mabeki na
kuwazidi kwa kuwahi kuicheza mipira hiyo kwa ufanisi mkubwa, aidha kwa
kuunganisha na kutoa pasi hatari kwa mwenzake au kuelekeza mwenyewe wavuni
inapotokea kuna ulazima huo wa kufanya hivyo kwa kichwa.
Mashuti anayopiga ni hatari
Ingawa kwa haraka haraka unaweza kumuona
kama mtu wa kusubiri ‘ku-press’ sana langoni anapokutana na kipa lakini kwenye
suala la kupiga ‘mashine’ pia amejaaliwa, hasa inapotokea amepata nafasi ya
kupiga mashuti ya kushtukiza basi kwake inakuwa siyo ishu na kujaribu bahati
yake.
Katika hili, faida nyingine ni kwamba si
mshambuliaji wa kupiga ilimradi bali ‘tageti’ ya lango ndiyo shida yake kubwa,
mara nyingi anaonekana kupima kwa kina mahala anapoupeleka mpira kwa shuti
japokuwa kipimo hicho hukifanya kwa uharaka mkubwa kwa ajili ya kuwahadaa
mabeki.
Siyo mchoyo/uamuzi wa haraka
Faida nyingine aliyonayo Ngoma ni katika
uamuzi wa haraka anapokuwa na mpira bila ya kuvunga na kuharibu ‘timing’.
Anapopokea mpira mara moja huwa naye anautoa na kisha anajipa nafasi ya
kujipanga kuupokea tena na kusonga mbele kupitia soka la pasi. Hata inapotokea
anahitajika kupiga pasi za mwisho kwa ajili ya kufunga bao pia hufanya hivyo
kwa mshambuliaji mwenzake au mchezaji mwingine aliyetangulia eneo la hatari.
Ana spidi
Wachezaji wenye maumbo makubwa kama yake
mara kadhaa hukumbwa na tatizo la kuwa wazito uwanjani na kukosa spidi, lakini
kwake ni tofauti kwani amekuwa akionyesha kuwa ni mtu mwenye spidi na mwepesi
sana kila akiwa na mpira.
Hali hii inaonyesha kuwa atakuwa msaada
mkubwa kwa Yanga ili kuhakikisha timu hiyo inatwaa makombe kadhaa makubwa.
Hapa anasaidia pia katika suala la kukaba
inapotokea mpira umepotea karibu na eneo lake kwani ni mwepesi wa kukimbia na
kupigania tena ‘mali’.
Anaelewa haraka:
Maelekezo mengi yaliyokuwa yakitolewa na
Pluijm kwa mastraika wake katika mazoezi hayo, yeye amekuwa akiyashika na
kucheza kama vile inavyotakiwa, hapa anaungana kwa kiasi kikubwa na Amissi
Tambwe kwa kuwa naye ana sifa hiyo anapokuwa mazoezini.
Ngoma amekuwa mwepesi katika kupokea
maelekezo na amekuwa akifanya kile kinachotakiwa, hali ambayo inamrahisishia
kazi yake katika suala la kuongeza mbinu za kuwahadaa mabeki.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment