Dalili za mvurugano kati ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) na klabu za Ligi Kuu Bara zinaonekana kunukia ambapo klabu zimejitokeza
kupinga utaratibu mpya wa shirikisho hilo kutaka klabu zilipe dola 2,000 (Sh milioni 4) kwa
kila mchezaji wa kimataifa anayesajiliwa kwenye klabu.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Azam FC, Saad Kawemba,
amesema kuwa, klabu hiyo inapingana na utaratibu huo kwani
ni wa kushtukiza na hawakushirikishwa.
“TFF katika hili hawajatutendea haki kwani
hawajatushirikisha, hata hivyo tutaangalia jinsi gani ya kufanya ili haki yetu
iweze kupatikana,” alisema.
Upande wa Simba kupitia rais wake, Evans Aveva, naye
alipinga kwa kusema: “Hatukubaliani na uamuzi huo na hivi karibuni tutakutana
ili kuangalia tunafanyeje.”
Yanga nao kupitia kwa katibu mkuu wa klabu hiyo,
Dk Jonas Toboroha, wameupinga uamuzi huo wa TFF na kuungana na Simba na Azam FC
ambazo ni klabu zenye wachezaji wengi zaidi wa kigeni kuliko nyingine.
Hivi karibuni Rais wa TFF, Jamal Malinzi
alinukuliwa akisema bila ada hiyo hakuna mchezaji wa kigeni atakayeruhusiwa
kucheza, hiyo ina maana kwa klabu yenye wachezaji saba itatakiwa kulipa dola
14,000 (zaidi ya Sh milioni 28).
0 COMMENTS:
Post a Comment