Na Saleh Ally
UNAIJUA tofauti ya ushabiki wa soka hapa
nchini? Huenda ukawa ndiyo tofauti kuliko ushabiki wa aina nyingine yoyote duniani
kwa kuwa watu ili waonekane wanapenda soka, lazima wawe wanazishabikia Yanga au
Simba!
Lakini ukiwa England, kuna mtu humuelezi
kuhusu Newcastle, Southampton, Leeds, Stoke City hata kama zitateremka daraja,
kamwe, shabiki atakufa na timu yake.
Ukiangalia chimbuko, utaelezwa anatokea eneo
ilipo Leeds United au Everton na si kuangalia timu kubwa tu yenye mafanikio
kama ilivyo hapa, wote tunashindana kuwa Yanga na Simba.
Ilitakiwa anayetokea Shinyanga, leo mapenzi
yake yawe kwa Mwadui au Stand United. Mwanza ni Toto African, Pamba au nyingine
za mji huo. Mbeya waendelee na Mbeya City yao, Iringa wafe na Lipuli kama
ambavyo Tanga wanavyoweza kugawana Coastal Union, African Sports au Mgambo.
Bado kunaweza kukawa na mapenzi ya wachezaji
ambayo yanakuwa ya dhati kweli. Hii ni sehemu ya kuonyesha furaha ya moyo kwa
mtu fulani kutokana na kile alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Bado tuna ugonjwa unaweza usiwe kwenye soka
pekee, huu uko hata katika maisha ya kawaida kwamba hatuna tabia ya kukubali ubora
walionao wenzetu. Badala yake tutashindana nao hata kama hatuna uwezo au kipaji
kama chao.
Louis Diamond ni Mwingereza mwenye miaka
mitano tu, sasa tayari ni mtu maarufu sana duniani hata kuliko Simon Msuva wa
Yanga au Mussa Hassan Mgosi wa Simba.
Umaarufu wa Diamond umetokana na machozi
yake ya dakika tano akilia kwa uchungu kutokana na kuumizwa na taarifa kuwa
mshambuliaji Robin van Persie anauzwa na Manchester kwa kitita cha pauni
milioni 23 kwenda Fernabahce ya Uturuki.
Mama yake alimrekodi mwanaye huyo akilia,
akionyesha uchungu wa juu kwa kuwa van Persie anahama. Siku chache baadaye,
idadi kubwa ikaiangalia video hiyo, Diamond akawa maarufu sana.
Klabu ya Fernabahce iliamua kutoa ofa
kumsafirisha Diamond, wazazi wake na wadogo zake wawili kwenda Istanbul,
Uturuki ambako waliishi kwa siku tano katika hoteli ya kisasa kabisa.
Wakapata nafasi ya kutembelea klabu hiyo,
sehemu mbalimbali za mji huo ikiwa ni pamoja na kumuona van Persie, kupiga naye
picha kabla ya kushuhudia akiichezea timu yake, mechi ambayo Fernabahce
waliibuka na ushindi.
Theo Walcott alikuwa mwokota mipira,
alivutiwa zaidi na Michael Owen wa Liverpool iliyokuwa timu yake ya kwanza
kuishabikia. Wayne Rooney pia alifanya kazi hiyo na shujaa wake alikuwa Dancun
Ferguson wa Everton, timu ambayo aliichezea zamani na wote hawa mapenzi yao
hayakuwa ya kupikwa na walipenda timu zilizokuwa karibu na maeneo waliyotokea
au kuvutiwa na mchezaji fulani.
Jiulize kwa nini unaipenda Yanga au Simba?
Sababu za msingi ni zipi hasa na kweli mapenzi yako ni ya dhati kutoka moyoni
au kwa kuwa Simba na Yanga zinaweza kukuletea mlo?
Mapenzi ya Diamond unaweza ukayachukua kama
kipimo sahihi cha kuona namna kutokuwa wakweli ndani ya mioyo yetu kunakuwa
chanzo cha kuuangusha mpira wetu.
Huenda mapenzi ya wengi kwa Yanga na Simba,
hayana sababu za msingi. Ndiyo maana wanashindwa kuwa msaada na klabu hizo
zinaendelea kubabaisha miaka nenda rudi!
Wengi hawaamini unaweza kuwa shabiki wa
Mbeya City au Stand United au Ndanda FC pekee. Ndiyo maana Pamba, Lipuli,
Kahama United, Kariakoo ya Lindi na nyingine zimebaki hadithi tu leo.
Lazima tujipime, lazima tukubali, mapenzi ya
dhati tena yenye sababu ni hadithi njema ya mabadiliko sahihi ya kitu.
Usishangae siku ukisikia Diamond ni nyota wa
Manchester United au Fenabahce kutokana na kilichotokea na atakuwa na kila
sababu ya kufanya vizuri kwa kuwa ana sababu za msingi na za dhati kutoka
moyoni mwake.













0 COMMENTS:
Post a Comment