August 17, 2015


Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita, Lionel Messi, alifunga mabao mawili na kuiwezesha Barcelona kubeba taji la Uefa Super Cup baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-4 dhidi ya Sevilla.


Mechi ilikuwa ngumu na Sevilla walikuwa sawa ile mbaya, lakini mabao hayo mawili ya Messi ukiyaingiza kwenye hesabu, ndiyo yanayoipa Barcelona ushindi huo.

Hauwezi kusema hakuwa na msaada. Huyu ni mtu wa aina yake katika soka, huenda sifa zake zinaweza zikawa zinamchosha kila mmoja.

Kila kukicha ana jipya, kwani baada ya fainali hiyo ameweka rekodi yake mpya dhidi ya Sevilla ambayo katika michuano yote ya Hispania na ile ya Ulaya amekutana nayo mara 24 na kuifunga mabao 24, kitu ambacho amekifanya pia kwa Atletico Madrid.


Messi tayari ameingia kwenye fainali ya Tuzo za Mchezaji Bora wa Dunia, maarufu kama Ballond’Or, akiwa na Luis Suarez na Cristiano Ronaldo anayeishikilia tuzo hiyo.

Sijui kama atazuilika, lakini rekodi yake nyingine inayomfanya awe mchezaji wa aina yake ambapo unaweza kumuita ni shabiki wa fainali, ni namna alivyocheza fainali nyingi na kwa mafanikio makubwa huenda kuliko mchezaji mwingine yeyote duniani.

Wakati anashuka dimbani kuivaa Sevilla kwenye mechi hiyo ya fainali ya kumpata bingwa namba moja wa Ulaya kwa kuwa wanakutana bingwa wa Uefa Champions League na bingwa wa Europa League, ilikuwa ni fainali ya 20 kwake.


Baada ya mechi hiyo ya fainali dhidi ya Sevilla kuisha, mambo yalikuwa hivi; katika mechi 20 za fainali, Messi alipambana na kuiongoza Barcelona kushinda mara 16.

Hii maana yake hivi; katika fainali 20 akiichezea Barcelona, Messi alishindwa kuisaidia Barcelona mara nne tu ikapoteza mechi, iwe kwa dakika 90, dakika 120 au kwa penalti.

Wapizani wakubwa wa Barcelona, Real Madrid amekutana nao kwenye fainali mara tatu, mbili zikiwa za Copa del Rey na moja ya Super Cup ya Hispania na mbili kati ya hizo, walishinda.

Katika fainali 20, Messi ameonyesha ni kweli ndiye mchezaji mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kufunga katika mechi ngumu na zenye presha kubwa, kwani amepachika mabao 22.

Mabao 22 katika mechi 20 ni wastani wa bao moja na nyongeza kwa kila mechi. Hii ni sehemu inayomaliza ubishi kuhusiana na ubora alionao.

Lakini pia inavutia kwamba, katika fainali hizo 20, mabao yake hayo amefunga kwa namna zote. Mguu wa kulia, kushoto, kichwa na kifua.

Takwimu zake nyingine zinaonyesha katika fainali zote ambazo Barcelona ilicheza kuanzia mwaka 2011 hadi 2013, Messi alifanikiwa kufunga bao.

Mara kadhaa, mjadala unaibuka wa Pele, Maradona na Messi yupi hasa ni mchezaji bora katika soka, tokea enzi?



Kinachoonekana Messi ambacho amekosa ni ubingwa au kombe akiwa na kikosi cha timu ya taifa, mambo ambayo waliyafanya akina Pele na Maradona.

Pamoja na ubora wao wa enzi hizo uliowapatia heshima kubwa, hakuna ambaye ameweza kufikia kwa karibu ubora wa juu wa Messi akiwa na klabu kwa maana ya makombe au upachikaji ‘kapu’ wa mabao.

Messi ana kipaji cha juu kabisa ambacho huenda ni nadra kutokea katika mchezo wa soka kwa kipindi hiki. Lakini jiulize, anafanya nini kufikia hapo?


Unajua alitua Barcelona akiwa na miaka 13, tena ni sababu ya ugonjwa na baba yake alilazimika kuacha kazi kwao Rosario, Argentina ili kusimamia matibabu yake. Barcelona wakicheza ‘bahati nasibu’, watumie fedha zao kumtibu, halafu huenda siku moja atakuwa na faida kwao.

Alipata namba katika kipindi kigumu kabisa, kwani wakati anaanza kucheza Barcelona katika kikosi cha kwanza mwaka 2004, staa wa kikosi hicho alikuwa ni Ronaldinho, si unaijua kazi yake? Lakini bado Messi alionekana na mwisho akachukua usukani.

Mwaka mmoja tu ulitosha Messi kuwa staa, hadi leo 2010. Miaka 10 Muargentina huyo anaendelea kuwa nyota wa Barcelona, pia dunia nzima.

Hakuna ubishi, anakaribia kuingia katika rekodi ya kuchukua mchezaji bora wa dunia mara tano na huenda akafanya hivyo zaidi ya hapo.

Kwa mchezaji wa Tanzania, huenda anaweza asiwe kama Messi. Lakini kama akiukaribia ubora huo, basi atakuwa gumzo huenda Afrika nzima.

Nani amewahi kujiuliza Messi anakula nini, analala saa ngapi, anafanya mazoezi yapi na huenda ana nguvu gani ya kujipa matumaini na kufikia kila anachotaka?



Msimu mmoja kabla ya uliopita, haukuwa mzuri kwake na kila sehemu mjadala ulikuwa amekwisha. Ulikuwa msimu wake wa kwanza kuwa majeruhi, kabla ya hapo alionekana kama chuma.

Lakini aliweza kupiga moyo konde, akaonyesha ujasiri wa moyo wake sasa amerejea na inaonekana tena hakuna kama yeye.

Kuna ule msemo; “hili nalo litapita.” Unaweza kuwa sehemu ya maisha ya Messi ambayo yanaweza kumfunza mwanasoka yeyote wa Tanzania lakini binadamu yeyote katika maisha ya kawaida, kwamba ukifeli unaweza kuinuka tena lakini kama tu unaamini vipindi vigumu vipo na vinapita kama unaamua iwe hivyo.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic