August 17, 2015


 
KIKOSI CHA SIMBA 1993.
Na Saleh Ally
USIPOSOMA vizuri na kunielewa, utaona kama ni mtu mchokozi sana, huenda nataka kukupa maumivu kwa makusudi tu kwa kuwa unaipenda sana Simba.


Ukitulia na kusoma ukanielewa, utagundua mengi sana kuhusiana na mpira wa Tanzania unavyokwenda lakini mfano mzuri nimeamua uwe Simba ambayo ndiyo timu ya Tanzania iliyokuwa ikitoka nje kucheza michuano ya kimataifa, inajulikana kazi yake.


Simba ndiyo timu iliyoonekana kuwa ukombozi wa Watanzania katika mechi za kimataifa. Unakumbuka hadi leo hakuna rekodi ya mapokezi kwa timu yoyote kama ilivyopokelewa Simba mwaka 2003 wakati ikitua nchini kutoka Misri baada ya kuitwanga Zamalek.

Simba iliifunga Zamalek kwa mikwaju ya penalti na kuivua ubingwa wa Afrika. Wakati inafanya hivyo nchini Misri, Zamalek walikuwa ndiyo timu bora ya Afrika.

Nakumbuka wakati huo, kwa mara ya kwanza nilimuona Augustin Lyatonga Mrema kwenye Uwanja wa Taifa (Sasa Uhuru) akiwa pale kuipokea Simba pia. Lakini bahati mbaya pia watu kadhaa mashabiki wa Simba walifariki dunia katika harakati za mapokezi hayo.
KERR AKIKIANDAA KIKOSI CHAKE...
Kabla ya hapo, Simba nusura iweke historia ya aina yake baada ya kufika fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993, lakini ikafungwa na Stella Abidjan. Bado inabaki kwua timu ya Tanzania kuwa na rekodi ya juu kabisa ya kucheza fainali ya michuano ya Afrika.

Simba ya 1993, ilikuwa inanolewa na Mtanzania, Abdallah ‘King’ Kibadeni. Simba ya mwaka 2003, ilikuwa inafundishwa na Mkenya, James Agrey Siang’a ambaye aliunganisha nguvu na Talib Hilal wakati wa kati ya Simba nchini Oman.
KIKOSI CHA SIMBA SASA...

Hoja yangu hapo ni kutaka kukuonyesha kuwa Simba za miaka hiyo, zikifundishwa na makocha wa nyumbani au nchi jirani ndizo zinabaki kuwa na historia ya juu kabisa hadi leo.

Simba inayoandaliwa na Kocha Mwingereza, Dylan Kerr inaonekana kama ndiyo timu mpya inayoanza kutambaa kwa kuwa ndani ya miaka mitatu inaonekana haina lolote kabisa.

Kerr ambaye ni mgeni, kamwe huwezi kumlaumu. Hauwezi kusema ameshindwa kwa kuwa hatujaiona kazi yake ingawa unaweza kuwa huru kuweka hofu yako, kwamba kama Milovan Cirkovic, Patrick Liewig na Goran Kopunovic walishindwa, yeye atakuwa na nini kipya?

Kwamba ukombozi wa Simba, irejee tena na kuwa timu tishio Tanzania Bara na Afrika umekwama wapi? Kwa viongozi ambao kubadilishana kwao kijiti kumefanya mambo yawe yanayumba tu, au makocha nao ni wana tatizo?

Simba imefanya vizuri miaka kumi na ushee iliyipita, lakini leo haiwezi tena, tena haisikiki kabisa na jina lake limebaki kuwa kubwa bila ya uwezo. Je, viongozi wanaridhika? Inawezekana hapana.

Maana tumeona juhudi zao kuhusiana na kambi, wamefanya kila linalowezekana. Lakini kweli kila mmoja wao ana moyo wa dhati kuonyesha kweli kinachofanyika ni kwa ajili ya klabu?

Hapa ninakumbusha kuaminiana, kupendana na kuwakubali wengine kwa maana ya kufanya mazuri kwa ajili ya klabu na si kuifanya sifa ya mmojammoja.

Matatizo yanayoikuta Simba, ndiyo matatizo yanayoikuta Yanga. Kwani ile iliyokuwa chini ya Abbas Gulamani ilifika mbali. Hii ya miaka hii chini ya Yusuf Manji, ikiingia kwenye michuano ya Caf, mapemaa, inarudi nyumbani!

Nani anajiuliza au kutaka kujua tiofauti ya zamani na sasa. Au nani anapiga hesabu kutaka kujua kama kweli timu zetu hizi kubwa zinapiga hatua au ndiyo zimefika na sasa zinaporomoja kurejea nyuma?

Yanga na Simba za miaka ya 1990, zilionekana bora zaidi kuliko za sasa? Kama hivyo ni kweli sasa tunakwenda wapi au unabaki kuwa muonekano wa jezi mpya lakini uchezaji au viwango ni bora ya zamani. 

Iko haja ya kujipima na kila tunalofanya, bado kuna nafasi ya kuangalia rekodi za nyuma kwani zinatuhukumu kwamba sasa tuna uwezo wa kifedha na teknolojia imeimarika, lakini timu zetu zinafanya vibaya, hazina uwezo kama wa timu za zamani. Viongozi wanahusika? Au wachezaji ni tatizo? Tujipime!



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic