September 9, 2015

CANNAVARO...

Na Saleh Ally
MUNGU akimjaalia maisha marefu, hata baada ya kustaafu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ atabaki kwa muda mrefu sana kwenye midomo ya wapenda soka nchini na ukanda wote wa Afrika Mashariki.


Hata Pele na Maradona, hawakupewa sifa nyingi sana kutokana na uwezo wao wakati wakicheza. Inajulikana, wamezungumziwa sana baada ya wao kuachana na soka.
Cannavaro hana kiwango cha Pele na Maradona, lakini kwa kiwango cha soka hapa nyumbani, amefanya mengi ambayo wengi sana hawakuwahi kuyafanya katika muda wao wote wa soka.

Cannavaro ndiye nahodha wa Yanga, Zanzibar Heroes na Taifa Stars na huu ni uaminifu wa juu kabisa kuwahi kupewa mchezaji hapa nchini.

Beki huyo kisiki wa Yanga anaonyesha kiasi gani anafanikiwa kutokana na juhudi kubwa ya utendaji, nidhamu ya kazi na mapenzi na kazi yake. Lakini uliwahi kujua kwamba alikuwa na kaka yake wa damu ambaye pia aliwahi kuitumikia timu ya Yanga, Malindi pia timu za Zanzibar Heroes na Taifa Stars?

Kaka yake alikuwa kipa bora wa Yanga, kama ilivyo kwake aliwahi kuipa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati sasa maarufu kama Kagame. Lakini alikuwa anaichezea Zanzibar Heroes pia Taifa Stars.

Huyo ni Rifat Said Mohammed, kipa nyota wa zamani wa Yanga, Malindi, Zanzibar Heroes na Taifa Stars. Wengi wanamkumbuka katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki mwaka 1993, Yanga ilipobeba kombe jijini Kampala, Uganda kwa kuwafunga vigogo, SC Villa.

Yanga ya kuungaunga, iliondoka ikiwa haina kitu, wachezaji walisafiri kwa basi lakini mwisho wakarejea na kombe hilo na kuwashangaza wengi.
RIFAT

Rifat aliingia wakati wa fainali kuchukua nafasi ya Steven Nemes aliyeumia. Aliingia uwanjani wakati mgumu kabisa wakati SC Villa wakiwa wamecharuka wanatafuta bao la kusawazisha lakini akawa kisiki likiwemo lile tukio la kuudaka mpira kwa mkono mmoja.

Baada ya Yanga kufungwa kwa mabao 3-1 na Pamba ya Mwanza katika mechi ya ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), mwaka huo wa 1994, Rifat aliamua kuondoka Yanga na kurejea Malindi na ndiyo ilikuwa mara yake ya mwisho kuonekana akiwa na Yanga.

Kumbe Rifat ni kaka wa damu wa Cannavaro, nahodha wa sasa wa Yanga? Beki ambaye ameiwezesha timu yake kutwaa makombe ya Kagame mara mbili.

“Kweli Rifat ni kaka yangu wa damu kabisa, wengi wamekuwa hawajui hili. Ingawa baba zetu ni tofauti lakini sisi ni watoto wa mama mmoja.

“Rifat ndiye aliyenisomesha mimi, alifariki bado nikiwa shule. Nilikuwa nina wakati mgumu kwa kuwa kipindi hicho pamoja na kunisomesha, nilikuwa nikibeba viatu vyake kila alipokuwa akienda mazoezini.


“Alikuwa shujaa wangu, mtu aliyeniongezea hamu ya kucheza soka. Lakini mwisho ndiyo hivyo, mambo ya Mungu,” anasema Cannavaro.

“Kwangu yalikuwa majonzi, tegemeo langu na shujaa wangu aliondoka. Lakini bado amebaki kuwa shujaa kwa kuwa ndiye alinipa moyo kwamba siku moja nitakuwa mchezaji tegemeo. Sikujali kipaji pekee, nikajituma sana kwa kuwa niliona wakati akifanya hivyo,” anaongeza Cannavaro.

Lakini utamu was tori hii ni kwamba, baba mzazi wa marehemu Rifat ni Said Mohamed. Huyu ndiye yule mwenyekiti wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Azam FC.

Mohamed maarufu kama Mzee Said, alikuwa mme wa mama Cannavaro. Baada ya kuachana naye ndiyo akaolewa na baba yake Cannavaro.

“Kweli, mzee Said ni baba yangu wa kambo. Ninamheshimu sana. Analijua hilo ingawa tunapoingia katika masuala ya kazi, kila mtu anafanya majukumu yake,” anasema Cannavaro.

Cannavaro anasema kwa kuwa anaamini katika familia yake kuna vipaji vya soka, basi angependa hata mwanaye naye acheze soka.

“Nilikuwa na kaka yangu pia alicheza soka huko Zanzibar. Mwanangu akiwa tayari, nitamuunga mkono acheze soka,” anasema Cannavaro.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic