Na
Saleh Ally
HIVI
karibuni Msemaji wa Yanga, Jerry Muro, aliingia kwenye matatizo na wadau wa
soka hasa baada ya kujisifia kwamba kikosi cha Taifa Stars kinaundwa na ukuta
wa Yanga ambao ni wa kimataifa.
Alichokisema
Muro kilikuwa ni sahihi kwa kuwa ukiachana na Shomari Kapombe, kipa hadi namba
tano wanatokea Yanga na si kwamba wamependelewa, hakika ni uwezo wao, hilo
halina ubishi.
Alichokisema
Muro kilikuwa ni ukweli mtupu, lakini hata mimi nilipingana naye kwa kuwa alishindwa
kusoma alama za nyakati, akazungumza tu.
Kwamba
huu ndiyo wakati Watanzania wanataka kuinua morali ya timu yao ya taifa ambayo
ilikufa kabisa kipindi cha yule Mholanzi, Mart Nooij ambaye kwangu niwe wazi
tu, kaivuruga kabisa Stars na kuifanya kama sehemu ya kujifurahisha kwake.
Niliambiwa kuna kiongozi mmoja wa TFF alikuwa
akimhakikishia hataondoka. Ndiyo maana alikuwa anafanya anavyotaka, lakini
alisahau ile timu ni ya Watanzania na si ya yule kiongozi aliyekuwa
anamdanganya. Sasa amekaa kando, kocha ameondolewa angalau matumaini yanaanza
kurejea.
Siasa za Simba na Yanga zina nguvu sana,
lakini wakati mwingine bora kupambana nazo ili kutafuta mafanikio ya mpira wetu
ambao tunajua, unatambaa tu kila kukicha, haujawahi angalau hata kusimama ili tuanze
kuangalia matumaini ya kutembea na baadaye tukimbie.
Stars sasa ipo chini ya mzalendo, Charles
Boniface Mkwasa ambaye ameonyesha njia kwamba tukiendelea kumuunga mkono
kuanzia wachezaji, viongozi wa TFF, viongozi wengine na wadau wote wa mchezo wa
soka, basi ataweza.
Lakini inaonekana wazi suala lake lina
mkanganyiko na sasa ni muda mrefu tangu tumekuwa tukisikia Mkwasa atapewa
mkataba rasmi ili achukue kazi ya kuinoa Stars.
Niliambiwa
Yanga na TFF walikuwa katika makubaliano na Mkwasa alikuwa amekubali kuondoka
na kufanya kazi ya Taifa Stars. Tunajua hii haitakuwa mara ya kwanza kufanya
kazi na TFF.
Alifanikiwa
kuipeleka Twiga Stars katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika baada ya
kuitwanga Ethiopia nyumbani kwao Addis Ababa kwa mabao 3-1.
TFF wanamjua vizuri Mkwasa kwamba ni
mchapakazi, ana uwezo wa kutoa msaada katika kikosi cha Stars na ameonyesha.
Swali linakuja hivi, vipi suala lake la mkataba linakuwa la kuzunguka sana?
Kwa
nini TFF wasimpe mkataba huo Mkwasa halafu waitaarifu wizara husika ianze kumpa
ule mshahara wake ambao wakija makocha Wazungu wamekuwa wakilipwa?
Kwa kiasi fulani nimekuwa nikiona hata wizara
husika nayo inasuasua kutoa mshahara huo kwa Mkwasa kwa kuwa ni mzalendo! Kama
itakuwa ni hivyo, basi litakuwa jambo kubwa baya ambalo hawajawahi kufanya kwa
miaka mingi.
Hakuna
kitu kibaya kama kujidharau, kujishusha. Huu ndiyo wakati pia wa kuonyesha mzalendo
anaweza kufanya kinachoonekana kigumu. Vizuri kabisa apewe mkataba mpya na
alipwe stahiki zake kama walivyolipwa makocha kutoka Brazil, Denmark na
Uholanzi ambao baadhi walijitahidi na wengine hawakutusaidia lolote na bado
walilipwa.
Pamoja na kumthamini Mkwasa pamoja na msaidizi
wake, Hemed Morocco na kumpa moyo zaidi kwamba anaaminiwa na Watanzania wapo
pamoja naye, lakini itamuongezea uhuru zaidi wa kazi yake.
Saa
hizi mwajiri wake ni Yanga, upande wa Stars ni deiwaka tu. Sasa kati ya hizo
wapi utatoa kipaumbele? Jibu ni rahisi kwa kila mtu, hivyo TFF waliangalie hili
kwa kuwa asije akaanza kuona kama anatumiwa kwa muda tu.
Motisha itamfanya Mkwasa aone kweli anapewa
thamani. Pia itapunguza maneno mengi.
Kama
Mkwasa atakuwa kocha mwenye ajira Stars na wengine wakalaumu, basi hawatakuwa
na hoja za msingi. Lakini wakati huu, lawama nyingine zinakuwa na mashiko.
Pia
kingine ninachokiona, kocha wa timu ya taifa kuwa kocha msaidizi katika klabu,
kiaina fulani haipendezi. Lifanyieni kazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment