October 3, 2015


Na Saleh Ally 
MSHAMBULIAJI nyota duniani, Cristiano Ronaldo, amefikisha mabao 500 aliyoyafunga akiwa na timu tatu pamoja na timu yake ya taifa.


Ronaldo amefikisha mabao 500 katika kipindi ambacho ametimiza miaka 30, jambo ambalo si dogo au si la kuliacha lipite tu.

 Hakika Ronaldo ambaye amekuwa mwanasoka bora duniani mara mbili, ana kipaji cha juu kabisa.

 Mabao hayo na mfano utaona amefikisha mabao 323 sawa na gwiji wa Real Madrid, Raul Gonzalez si jambo dogo. Sasa ana nafasi ya kuwa gwiji kwa kufunga mabao mengi zaidi.

 Tayari Ronaldo ana rekodi ya wastani wa juu zaidi katika ufungaji kwenye Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’. Ana wastani wa 1.05 ya mabao. Maana yake amefunga bao katika kila mechi kama mabao yake yatagawanywa.

 Mafanikio ya mabao 500 tangu alipofunga bao lake la kwanza akiichezea Sporting Lisbon ya Ureno Oktoba 7, 2002.
Ndani ya miaka 13, Ronaldo ameweza kufunga mabao hayo 500 tena akicheza katika timu kubwa tatu ambazo hakika zinakuwa na ushindani wa juu na wachezaji wake hupambana na upinzani wa juu kabisa.

Ameshinda kila kombe kwa ngazi ya klabu akiwa na Manchester United na Real Madrid ambazo ni moja ya timu kubwa tatu zaidi duniani.

 Wakati anatua Real Madrid, msimu wa kwanza aliweza kuweka wastani wa mabao 20 kwa msimu. Baada ya hapo akapanda kwenda hadi mabao 53, kitu ambacho si mzaha hata kidogo.
Msimu wake wa kwanza na Madrid ambao ulikuwa ule wa 2009/10, alifunga mabao 21, uliofuata wa 2010/11 akatandika kimiani mabao 50.

Msimu wa 2011/12, akafunga mabao 66, msimu wa 2012/13 akashuka kwa kufunga mabao 51, ule wa 2013/14 akafunga mabao 56 na 2014/15 akafunga mabao 66.

Angalia ushindani wa La Liga au michuano ya Ulaya, lakini huyu mtu ana uwezo wa kufunga hadi mabao 50 kwa zaidi ya misimu miwili au mitatu anafanya hivyo.

Katika hali ya kawaida unaamini kweli ni kipaji pekee? Ndiyo maana nikaamua kukumbusha kwamba mafanikio ya watu hawa hayapatikani ukiwa umelala na kufumba macho.
Lazima kujituma, lazima kujipambanua na kuamini mtafutaji hachoki. Historia ya Ronaldo inajielezea, kwa kuwa wazazi wake walikuwa ni watu wa maisha ya chini kabisa.

Baba yake alikuwa ni mtunza bustani tu huko kwao katika Kisiwa cha Madeira, Ureno. Ronaldo alionyesha anataka kufanikiwa na utaona wakati akiwa Manchester United wachezaji wengi walimshangaa kwamba anaishi vipi, kweli anaweza kula raha na maisha yake. Kwamba hakuwa akijipa nafasi ya kula maisha?

Maana alikuwa akifika mazoezini saa moja au mbili kabla ya wenzake, aliondoka mazoezini saa moja baada ya wenzake. Muda wote aliokuwa pale aliendelea kujifua zaidi.

Hata walipokwenda gym, yeye ndiye alibaki muda mwingi zaidi ya wengine. Kuna wakati hadi Kocha Sir Alex Ferguson aliwahi kumuonya kufanya hivyo, kwamba apunguze mazoezi.

Wakati anatokea Manchester United kwenda Madrid, wengi walichambua na kusema angefunikwa kabisa na Lionel Messi na kupotea. Lakini leo amebaki pekee anayechuana vikali na mshambuliaji huyo wa Barcelona mwenye kipaji cha juu kabisa.

Ronaldo si mashine, ni binadamu kama wewe lakini ameamua kuishi tofauti, ameamua kutaka kufanikiwa. Amepania kutimiza ndoto zake bila ya kusikiliza maneno mengi ya pembeni ambayo hukatisha tamaa.

Hii inakuhusu wewe mchezaji wa soka wa Tanzania katika daraja lolote, achana na woga na kusikiliza sana maneno ya watu hasa yale yanayosisitiza ‘hauwezi’.

Unaweza zaidi ya wanavyofikiri, unaweza kufika zaidi ya ulipo. Lakini usifumbe macho ukalala. Hauwezi kuwa kama Ronaldo, lakini unaweza kupata mafanikio ya juu yanayoweza kuwashangaza wengi kama Mreno huyo anavyoshangaza kwa mabao yake hayo 500.

Kwa Tanzania hata kufunga mabao 50 kwa misimu minne nayo ni shida kubwa. Bado wewe unaweza kuwa wa kwanza kama utaachana na woga, kukubali kukatishwa tamaa.

Ronaldo si mashine, ni binadamu lakini anafanikiwa. Lakini lazima ukubali kuumia zaidi na kujituma zaidi ili kufikia mafanikio.

Usiyaache mafanikio yake ya mabao 500 yapite tu kama kitu cha kukushangaza, badala yake yafanyie kazi siku nyingine yakusaidie hata katika maisha ya kawaida. Panga ndoto, iote ukipambana na mwisho ufanikiwe.


BAO LA KWANZA AKIWA….
SPORTING LISBON
Oktoba 7, 2002 vs Real Betis.

MAN UNITED
Novemba  Mosi, 2003 vs Portsmouth.

REAL MADRID
Agosti 29, 2009 vs Deportivo.

TIMU YA TAIFA URENO
Juni 12, 2004 vs Ugiriki.

MABAO:
NDANI YA BOKSI: 417
NJE YA BOKSI: 83
PENALTI: 81
ADHABU:  45

ALIFUNGAJE?
Mguu wa Kulia: 326
Mguu wa kushoto: 89
Kichwa: 83

TIMU ALIZOZIFUNGA LA LIGA:

Sevila-21, Getafe-18, Barcelona-15, Atletico Madrid-15, Malaga-14

WALIOMPA ‘ASISTI’ NYINGI:
Karim Benzema 31, Mesut Ozil 28, Angel di Maria 20, Gareth Bale 15, Ryan Giggs 16, Gonzalo Higuain 15.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic