October 16, 2015

ANGALAU HAWA WANAFUNZI WALIIIONA KAZI YAKE NA KUMFUATA KUMPONGEZA, WADAU WENGI WA SOKA, WAKO KIMYA WANASUBIRI AHABARIBU....

Na Saleh Ally
SOKA ni mchezo unaojumuisha watu wa aina nyingi sana, wako wenye mapenzi ya dhati na wengine wasiojali wala kufikiria hata kidogo, nature au asili ya mchezo wa soka ni nini.


Katika mashabiki wa soka, mjumuisho wa watu ni mkubwa sana, wako waelewa, wako wasiolewa na wengine wanajiehusha makusudi!

Mashabiki wa soka hasa hapa nyumbani, wengi wanasubiri kupaza sauti zao wakati wa makosa. Lakini mambo yanapokwenda vizuri, kila mmoja hukaa kimya.
Hauwezi kusema watu hawapendi mazuri, huenda wanapenda zaidi kukosoa kwa kudhalilisha, kuumiza au kuudhi. Ndiyo maana ikitokea mchezaji kakosea uwanjani, suala lake lazima litahusishwa na rushwa au haipendi timu hiyo.

Inawezekana mchezaji huyo atahusishwa na mapenzi na timu nyingine au hata kuzushiwa aliwahi kuonekana akiwa na kiongozi wa timu Fulani, ndiyo maana amefungwa.

Ajabu, ni hivi, kila yule mchezaji anapokuwa akifanya vizuri, hakuna lawama lakini hakuna pongezi, ajabu kabisa.
Nimeamua kumzungumzia Ally Mustapha, kipa wa Yanga ambaye anajulikana sana kama Barthez. Hakika yuko katika kiwango cha juu kabisa kipindi hiki.

Barthez ameweza kumuweka ‘mkeka’ kipa Aishi Manula wa Azam FC ambaye kwangu namuona ndiye kipa bora kabisa kinda katika kipindi hiki.


Barthez ameitumikia Yanga kwa kiwango cha juu zaidi, umewasikia hata wanamsifia. Lundo la mashabiki na wanachama, wameweka akiba ya mashambulizi siku atakapokosea waseme alitokea Simba. Msaada wake wa sasa unaonekana ni ilimradi tu.

Achana na ishu ya klabu, twende kwenye timu ya taifa, Taifa Stars. Barthez ameendelea kuwa katika kiwango kizuri na huko Manula analazimika kusubiri kwa kuwa kipa huyo mkongwe kwake yuko sawa kweli.

Kwa kipindi hiki, hata kama si peke yake, lakini Barthez yuko katika kiwango cha juu sana na amefanya kazi kubwa kuisaidia Stars kuiondoa Malawi na sasa itakutana na Algeria kuwania kucheza Kombe la Dunia.

Ukiangalia mechi ya kwanza wakati Taifa Stars inacheza na Malawi jijini Dar es Salaam, utaona namna alivyokuwa mwokozi. Stars ilishinda kwa mabao 2-0, lakini hali haikuwa nzuri na safu ya ulinzi na kiungo cha ulinzi kiliruhusu kupenywa zaidi ya mara nane.

Barthez aliokoa michomo mitatu iliyokuwa imelenga lango ambayo usingetemea hata kidogo kama kweli aliiona. Kweli ni jukumu lake lakini ilikuwa ni kazi bora kabisa ya kujivunia na kumsifia.

Mechi ya pili ambayo Taifa Stars ilipoteza mechi ikiwa ugenini Malawi kwa kufungwa bao 1-0 lakini ikasonga, mambo bado yalikuwa magumu.

Barthez aliokoa shuti lililopigwa na mshambuliaji wa Malawi, hatua tano tu kutoka langoni. Kama Stars ingefungwa bao katika dakika ya kwanza, hakika dakika 89 zilizobaki  ‘ingefia ‘ Malawi kwa kuwa wachezaji wangechanganyikiwa mapema.


Umakini wa Barthez hata kama ndiyo kazi yake, umechangia Stars kufikia hapa ilipo. Kama angekuwa pale langoni ni ‘kapu’, watu wanatupia tu, basi Stars ingepotea na isingefanikiwa kuitoa Malawi.

Ukimuangalia, Barthez ambaye ni mtaratibu alikuwa anaonyesha yuko tayari ya mchezaji na alikuwa amenuia kuisaidia Stars kufikia hapo ilipo sasa na zaidi.

Kwa kila alichokifanya BArthez kwa kuwa ni kizuri, si lahisi kusikia akizungumziwa au anasifiwa kwa ubora wa kazi yake.

Akiharibu ndiyo itakuwa gumzo, akiharibu ndiyo atatajwa sana. Watu watafungua vinywa vya na kuanza kusema kuhusiana naye kwa mabaya.

Leo nimeona huu ni mfano sahihi wa kuwakumbusha kwamba inapotokea mtu amekosea, pia ni vizuri kuangalia kabla ya kukosea alikuwa akifanya vipi kuhusiana na kupatia.

Yeye ni binadamu, lakini mchezo wa soka makosa ni lazima. Kama utakuwa na watu wanacheza tu bila ya kukosea, hata katika soka ingecheza timu moja ambayo ingeshambulia mfululizo kwa dakika zote 90. Hivyo lazima tujifunze na vizuri pia kujifunza na kupata uelewa wa unachokishabikia kuliko kuwa bendera fuata upepo.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic