Muda mfupi
baada ya kuvaa jezi ya Mbeya City na kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu
Bara msimu huu akiwa na kikosi cha Mbeya City, kiungo Haruna Moshi ‘Boban’
amepewa majukumu mazito na kocha wake, Meja Mstaafu Abdul Mingange.
Boban ambaye
alicheza katika mchezo dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Sokoine, alionekana
kutokuwa kwenye ubora wake, hali ambayo ilielezwa na kocha wake kuwa bado
hajawa fiti na kuahidi kuwa kama akizingatia mazoezi basi anaamini atakuwa
msaada mkubwa kwa timu hiyo.
Mingange amesema Boban ni mchezaji mzuri
lakini hakuridhishwa na kiwango chake, ambapo amemtaka kupambana kurejea katika
ubora wake uliozoeleka.
“Boban bado
hajawa fiti kwa asilimia zote, hivyo leo (juzi) hajaniridhisha sana pamoja na
kwamba amecheza kwa kujituma na kuwafanya wenzake pia kuwa na bidii, najua
atakuja kufanya vizuri zaidi ya leo.
“Tumefungwa leo
kutokana na kupoteza umakini kipindi cha kwanza ila natumaini michezo ijayo
nitafanya kila namna ili nihakikishe tunapata ushindi.
“Kwenye soka
siku zote huwezi kuwa unacheza kwa historia hata kama tumefungwa na Simba watu
bado wanatakiwa kuwa na imani na Mbeya City, kwani timu yangu ina upungufu mwingi
ambao tutaufanyia kazi haraka iwezekanavyo,” alisema Mingange.
Kabla ya kutua
Mbeya City, Boban alikuwa Uarabuni kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa lakini
hakufanikiwa kufuzu, kwa kuwa alikuwa ameshasaini mkataba wa kuichezea Mbeya
City kabla ya ligi kuanza, amerejea nchini na kujiunga na timu hiyo kuitumikia
kama mkataba wake unavyomtaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment