October 2, 2015


Na Saleh Ally
KATIKA mechi ya Ligi Kuu Bara, mabingwa watetezi Yanga walipokuwa wageni wa watani wao Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huu ulikuwa mchezo muhimu sana.


Mechi hiyo iliisha kwa Yanga kufuta mambo ya uteja baada ya kuifunga Simba mabao 2-0 na kuamsha shangwe kuu kwa mashabiki wao.

Kawaida mechi hiyo huwa haiishii kirahisi katika habari za matokeo au nani kafunga pekee. Badala yake hujumuisha mambo mengi ambayo mara nyingi hubaki kwenye historia.

Moja ya matukio yaliyotokea ni kuhusiana na kiungo mwenye kasi wa timu hiyo, Simon Happygod Msuva, ambaye alitolewa katika kipindi cha kwanza baada ya kuonekana mchezo umekataa kabisa.

Hakika Kocha Hans van der Pluijm alikuwa sahihi kumtoa Msuva katika dakika ya 34 na nafasi yake kuchukuliwa na Malimi Busungu.

Wakati Msuva anatoka, baadhi ya mashabiki wa Yanga waliokuwa uwanjani hapo walipaza sauti za kumzomea. Haikuwa rahisi kujua kwa nini walikuwa wanamzomea kiungo huyo mwenye kasi ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa kupambana kwa ajili ya timu na heshima ya klabu yake.


Kelele za mashabiki kumzomea, zilinifanya nijiulize maswali mengi ambayo majibu hayakuwa na uhakika. Mfano, labda kwa kuwa baba yake ni shabiki wa Simba? Au labda kwa kuwa hakucheza vizuri wanahisi ametumika?

Kwa nini mashabiki wanaweza kudhani hivyo? Hakika hata wao wako ambao wanafuata hisia au maneno ya ‘mitaani’ au yale ambayo wameyasikia kutoka kwa baadhi ya viongozi wao ambao wengi wao hawajui mpira, ila wako kwenye mpira kwa maslahi yao.

Msuva alizaliwa Oktoba 2, 1993, maana yake sasa ana umri wa miaka 23. Huwezi ukasema ni mkongwe au mzoefu, lakini katika umri huo tayari amekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara wakati huo Yanga ikichukua ubingwa.

 Ukizungumzia ubingwa wa Yanga msimu uliopita, lazima utamtaja Msuva ambaye ‘alitoboa’ nyavu mara 17 katika msimu huo na kuisaidia Yanga kuwa mabingwa. Lazima anastahili pongeza.

Sasa ajabu unaona baadhi ya mashabiki wake wanamzomea kwa kushindwa kucheza mechi moja ambayo kutokana na kuipania tu, ikasababisha ashindwe kucheza vizuri.


Bado hakuna anayejua Msuva anajisikiaje, alikuwa na tatizo gani ndani ya mwili wake au nje lakini limemjaza mawazo kichwani mwake. Sasa vipi abandikwe ubaya kwa siku hiyo moja tu?

Msuva anapaswa kuelewa mambo mengi sana, lakini la kwanza, hauwezi ukafanikiwa kama utacheza soka huku ukiwa unategemea shukrani. Wapenda soka ni watu wasio na shukrani na ndivyo walivyo wa Tanzania, Kenya, Afrika nzima tena utafikiri wamezaliwa na mama mmoja maana hata wale wa Ulaya, wako hivyohivyo.

Kunaweza kuwa na tofauti ndogo ya ulewa, mfano wale wa Ulaya, wakati mwingine mchezaji akikosea au angetolewa hivyo kama Msuva ungeona wamesimama na kumpigia makofi ya kumpa moyo.

Wanasimama kumpigia makofi kwa kuwa pamoja na pongezi ya kazi, lakini ni kutaka kumuonyesha kwamba kazi yake wanaithamini na kama ameshindwa siku hiyo ajaribu siku nyingine. Pia wanajua baada ya mechi hiyo atakuwa na muda wa kutafakari kabla ya kurudi tena katika mechi nyingine, vizuri kumuonyesha kuna watu wanamuunga mkono.

Huko Ulaya pia kuna wendawazimu, utaona wale ambao walikuwa wakimzomea Iker Casillas. Inashangaza kuona Casillas anazomewa Santiago Bernabeu. Kipa Gianluigi "Gigi" Buffon amesema kwa makubwa aliyoifanyia Madrid, hata angechukua mpira akaupiga uingie wavuni bado alitakiwa kupigiwa makofi na si kuzomewa.

Wamemzomea hadi alipoamua kuondoka na kuhamia FC Porto, bado anaonyesha ana uwezo na msaada katika timu yake mpya.

Ukicheza soka, hutakiwi kuamini shukrani, badala yake ni kutenda majukumu yako muhimu, pia kutenda wema na kwenda zako.

Kama Msuva atataka shukrani, itakuwa rahisi kwake kufa kisoka siku moja. Jambo ambalo halitakuwa sahihi, mashabiki wa soka pia ni vigeugeu na hao kesho watapiga kelele kumshangilia kwa nguvu.

Mfano mzuri, walimbeba Morogoro akiwa ameingia dakika za 10 za mwisho, akasaidia kupatikana kwa bao la pili lililofungwa na Donald Ngoma wakati Yanga ikiifunga Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.


Safari ya Msuva kisoka bado ni ndefu sana, analazimika kuwa mvumilivu na wakati mwingine ajue kazi anayoifanya si kwa ajili ya kumfurahisha mtu, badala yake ni jukumu lake na utekelezaji bora wa mkataba kati yake na mwajiri wake Yanga, wanaopiga kelele awafananishe na chura, hasa kama akiona kelele zao, hazina faida.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic