Na Saleh Ally
Hivi karibuni Rais wa Simba, Evans Aveva alikwenda kushitukiza
katika mazoezi ya Simba baada ya kutokea bila ya taarifa.
Simba ilikuwa ianajifua katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Aveva aliibuka na kujificha akashuhudia mazoezi yote ya Simba hadi walipomaliza.
Baada ya hapo benchi zima la ufundi likiongozwa na Kerr lilimfuata
na kuanza kuzungumza naye. Wengine walikuwa ni Kocha Msaidizi, Selemani Matola,
Kocha wa Makipa, Iddi Salim na Menaja, Abbas ‘Gazza’.
Siku chache baadaye, Matola alitangaza kuachia ngazi akieleza
sababu kadhaa kuhusiana na Kerr ambaye aliamini wasingeweza kufanya kazi
pamoja.
Baadhi ya sababu hizo ni Kerr kuonekana kutotaka kusikiliza
ushauri wowote kutoka kwa Matola, kupanga kikosi bila ya kumshirikisha na
wakati mwingine alisema kumtafutia fitina na wachezaji.
Ukirudi katika picha ambayo benchi la ufundi lilimfuata Aveva na
kuanza kuzungumza naye siku ile, utagundua jambo ambalo huenda hatukuliona.
Wakati Aveva akizungumza na mabosi hao wa benchi la ufundi la
Simba. Kila mmoja alionekana kuchangamka na kuzungumza naye.
Matola pekee ndiye alionekana muda wote akiwa ameinama yuko busy na simu yake na uchangiaji wake pia ulikuwa mdogo sana.
Inaelezwa siku chache baadaye, Matola alipata shutuma kwamba
alikuwa akipeleka maneno kwenye uongozi na uvamizi wa Aveva ulihusishwa naye.
Picha ile ingeweza kusema maneno mapema sana kama uongozi wa Simba
ungefuatilia kwa karibu na huenda pia lingekuwa jambo zuri sana kuanza kuokoa
hali iliyokuwepo.
Ninaamini Simba ingeweza kuwaweka pamoja Kerr na Matola na
kuwaeleza hali halisi na Simba ilikuwa inataka nini badala ya wao kufikia
katika hali hiyo.
Inawezekana kabisa Simba waliona ni sahihi kumuacha Matola aende. Lakini
suala la kujaribu kulimaliza suala hilo lilikuwa ni jukumu lao.
Kuondoka kwa Matola, kwangu naona alichelewa na wala hakutakiwa
kusubiri mgogoro ndiyo aondoke. Badala yake aliatakiwa kufanya hivyo kwa ajili
ya maendeleo yake kama kocha mwenye kipaji na uwezo wa kufanya vizuri akiwa
kocha mkuu kijana.
Lakini msisitizo, uongozi wa Simba unapaswa kuwa mwepesi wa kung’amua
mambo na kuyasawazisha kabla hayajafikia kuwa tatizo kubwa na wengine kujiuzulu
kama ilivyokuwa kwa Matola.
0 COMMENTS:
Post a Comment