Huku kandarasi ya beki wa Simba, Hassan
Kessy ukielekea ukingoni huku Yanga ikitajwa kuwa huenda ikamsajili beki huyo ikiwa
tayari imeshaonyesha nia hiyo, Kocha Mkuu wa Simba, Dlyan Kerr amekuwa mkali
kwelikweli baada ya kusikia taarifa hizo na kutamka: “He is not for sale”.
Kauli hiyo ya Kerr inamaanisha kuwa Kessy
hawezi kuuzwa kwenda kokote, na kudai kuwa mipango aliyonayo kwa mchezaji huyo
ni ya muda mrefu, hivyo ni vigumu kwake kukubali aondoke kirahisi.
“Kessy hatuwezi kumuuza kwa kuwa ni
mmoja wa wachezaji wetu tegemeo, hawezi kwenda kokote hata Yanga ambapo
nimesikia wanamtaka, nafikiri hizo ni tetesi na zitabaki kuwa tetesi,” alisema
kocha huyo na kuongeza:
“Kama ni kuondoka
basi ataondoka kwa dau kubwa sana, nimepanga kukutana na beki huyo na viongozi
wangu kujua jinsi gani tunamshawishi Kessy ili aongeze mkataba mwingine kabla
ya huu aliokuwa nao kumalizika.”
Inaelezwa kuwa kufikia mwezi ujao, Kessy
ambaye alitua Simba akitokea Mtibwa Sugar, atakuwa amebakiwa na miezi sita ya
mkataba wake, hivyo kwa mujibu wa kanuni za usajili, ataruhusiwa kuzungumza na
klabu nyingine yoyote kuhusu suala la uhamisho.
0 COMMENTS:
Post a Comment