Na Saleh Ally
JOHN
Joseph Pombe Magufuli kaapishwa, ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huu ni uthibitisho kipindi cha kampeni kimepita na tayari rais wa nchi
amepatikana, hivyo heshima ichukue mkondo wake.
Niwe kati
ya watu wa mwanzo kabisa kuungana na wengine watakaofuatia kumkaribisha Rais
Magufuli.
Hakika Rais Magufuli ana mambo mengi sana ya
kufanya na suala la kumpa muda halikwepeki kwa kuwa mengi atakayokuwa
akiyafanya, pia yatahitaji muda.
Wakati
akianza utekelezaji wa ahadi zake, tafadhali namkumbusha katika michezo nchini
na kama akianza, basi katika mchezo wa soka kuna mengi ya kufanya pia.
Soka ndiyo
mchezo unaopendwa zaidi nchini, namhakikishia Magufuli kwamba una uwezo wa
kuwanufaisha watu wengi zaidi kuliko mambo yanavyokwenda kwa sasa.
Vijana hao
wanafaidi matunda ya vipaji vyao, lakini wana bahati mbaya bado hawajapata
viongozi sahihi wa kuwaongoza na kuwatengenezea njia inayoweza kupitika.
Kweli Rais
Magufuli atakuwa na kazi nyingi, ndiyo maana ninataka kumkumbusha asiisahau
michezo na ikiwezekana iwe na wizara yake inayojitegemea kabisa ili iweze kuwa
na mwendo sahihi.
Kuna kila
sababu pia ya kuweka utaratibu wa kupambana na viongozi wababaishaji walio
katika michezo ikiwemo soka.
Simba na Yanga zina viongozi wengi wasio
wakweli, wengi walio ndani ya klabu hizo ni kwa ajili ya maslahi yao na si
Watanzania wengine. Klabu zao hazina hata viwanja vya mazoezi, TFF ilibahatika
kupata wa msaada!
Ndani ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nao kuna watu wasio wakweli, walio kwa ajili
ya maslahi yao ambao hawaangalii nchi hii inataka nini, badala yake wao
wanataka nini.
Wapo ambao
wanatetea maovu kwa kuwa wanataka kufaidika wao. Wapo wanaotetea maovu ya
rafiki zao angalau tu wawafurahishe na si kwa ajili ya mpira wa Tanzania.
Wapo rundo
la watu wanaoimaliza michezo ya Tanzania na wana nafasi ya kuwa jeuri kwa kuwa
tu wana hiyo nafasi na utaratibu unaonyesha hakuna lolote la kuwafanya.
Kipindi
chako, tafadhali iangalie michezo kama sehemu hasa ya mipango ya maendeleo ya
taifa letu. Usiiangalie kama unaisaidia tu, usiiangalie kama ni sehemu ya
ziada, michezo ina msaada mkubwa katika maendeleo.
Watanzania
wamechoka na kudanganywa tangu enzi za Chama cha Soka Tanzania (Fat). TFF bado
inaonyesha haina mabadiliko makubwa kwa kuwa ndani yake kuna chembe za uzembe
ambazo hazijaisha pia.
Lakini
vyama vya mikoa, navyo vinarithi na katika soka ndiyo kunaonekana kuna majungu
makubwa badala ya maendeleo makubwa.
Unaweza kushangaa, kwamba unawezaje kuingia
huko. Lakini serikali yako inaweza kama itajikita na kutupa macho ya kutosha
katika michezo, hasa soka. Tatua suala la viwanja kwanza, maisha ya soka yawe
uwanjani zaidi ya kwenye makabrasha na majungu.
Serikali
izipiganie timu zetu zinazoshiriki michuano ya kimataifa. Rwanda wanaweza vipi
sisi tushindwe?
Mafanikio
zaidi kupitia uwanjani, taratibu kutaanza kuwakimbiza viongozi wavivu
wanaozidisha majungu badala ya kazi tu.
Viwanja kwa ajili ya kukuza na kuendeleza
vipaji, maeneo ya wazi yaliyoibiwa yarudishwe na ikiwezekana uwe unakemea
viongozi wanaotuangusha maana wengine wanajidai wameziba masikio, lakini
ukizungumza wewe, watayafungua tu hata bila ya kupigiwa hodi.
0 COMMENTS:
Post a Comment