Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans VanDer Pluijm, amekiri ugumu wa
ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini amepanga kupambana kuhakikisha anashinda kila
mchezo atakaocheza.
Kauli hiyo, ameitoa hivi karibuni baada ya kufanya tathmini nzima ya
ligi kuu katika mechi tisa walizozicheza baada ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) kusimamisha ligi hiyo ili kupisha kambi ya Taifa Stars.
Timu hiyo, hadi hivi sasa tayari imecheza michezo tisa, kati ya hiyo,
imetoka sare michezo miwili dhidi ya Azam FC mabao 1-1 na Mwadui FC 2-2 huku
hiyo mingine ikishinda.
Akizungumza na Championi Jumatano, Pluijm alisema kwa jumla ligi kuu ni
ngumu kwa upande wao kutokana na kila timu wanayokutana nayo kucheza soka la
fujo na kulinda lango lao dakika zote 90.
Pluijm alisema, hilo ameliona tayari na amepanga kulifanyia kazi mara
ligi kuu itakapoanza tena kwa kuhakikisha anawapa mbinu wachezaji wake za
kuhakikisha wanashinda kwa kila mechi watakayoicheza.
Aliongeza kuwa, watakuwa wanawalazimisha wachezaji wa timu pinzani
kutoka langoni kutokana na kushambulia kila wakati kwa ajili ya
kuwachosha.
“Moja ya tahadhari nitakayoingia mara baada ya ligi kuu kuanza ni
kuwataka wachezaji wangu kucheza kwa umakini mkubwa kwenye mechi zote kwa
kuhofia majeruhi kikosini kwangu.
“Hiyo ni kutokana na timu pinzani kucheza soka la fujo kwa kuwachezea
rafu za makusudi wachezaji wangu, ninaamini kama wachezaji wangu wakipata
majeraha, basi malengo yangu hayatatimia.
“Pia nimepanga wachezaji wangu kucheza soka la kushambulia dakika zote
kwenye lango la timu pinzani, hiyo ni kutokana na kila timu tunayokutana nayo
kulinda lango lao,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment