SARE ya Taifa Stars dhidi ya Algeria
iligeuka kitu kisichotarajiwa kwa njia tofauti ambayo pia haikutarajiwa.
Imekuwa ni mambo ya kisichotarajiwa kwa kuwa
kabla ya mechi hiyo, wengi sana walisema Taifa Stars haina nafasi hata kidogo
kwa Algeria na lazima itafungwa hapa nyumbani.
Kitendo cha kukosa mabao kadhaa na kuongoza hadi
mapumziko, wengi wakageuka na kuanza kuamini Taifa Stars sasa ilikuwa na nafasi
ya kushinda hata mabao manne. Safari hii wengi wakawa wamesahau kabisa kwamba
waliamini Stars haina lolote dhidi ya Waalgeria hao ambao kwa ubora wa viwango
vya Fifa, inashika nafasi ya pili barani Afrika.
Baada ya mechi kuisha, matokeo yakiwa ni 2-2,
Algeria wakisawazisha mabao yote mawili, watu wengi wakaingia kwenye ule mtindo
wetu kwamba ni lazima tulaumu tu kila linapotokea jambo lolote la mpira, iwe ni
sare au kushinda.
Lawama zinamwangukia Kocha Charles Boniface
Mkwasa ambaye aliamua kufanya mabadiliko katika dakika ya 63 baada ya kuwatoa
wachezaji, Elias Maguri na Mudathir Yahya na kuwaingiza Mrisho Ngassa na Said
Ndemla.
Hakika wakati mabadiliko hayo yakifanyika,
niliingia hofu kidogo. Nikaona kulikuwa na dakika 27 ambazo zilikuwa nyingi
sana kwa kutoa wenye uwezo mkubwa wa kukaba na kuingiza wengine kwa ajili ya
kushambulia.
Kwa waliokuwa wameingizwa, ingekuwa Stars
iko katika hali ngumu na inahitaji bao kwa namna yoyote, basi Mkwasa angefanya
hivyo. Badala yake niliona ingekuwa sahihi kumuingiza Jonas Mkude ambaye ana
nguvu na uwezo wa kukaba na sasa angekuwa bado na pumzi ya kutosha tofauti na
Mudathir aliyekuwa amechoka.
Hii maana yake, Stars ingeweza kulinda mabao
yake. Halafu ingewezekana kuingiza mtu mwingine wa kushambulia kama ilivyo kwa
Ngassa kwa ajili ya kujaribu kupata bao la tatu ili kujihakikishia nafasi nzuri
katika mechi ya pili.
Pili, niliona Mkwasa alifanya mabadiliko
hayo haraka sana. Angalau kuanzia dakika ya 75 au kama ni mapema zaidi, mkabaji
alihitajika zaidi ya mchezeshaji.
Pamoja na yote hayo, sioni kama kuna sababu
ya kugeuza suala la mabadiliko hayo ndiyo gumzo kubwa na kuanza kulaumu
kupitiliza.
Sare na Algeria bado ni jambo zuri na funzo
kubwa kwetu. Pia jambo la kuwakumbusha wengi ambao waliamini Taifa Stars
itafungwa hata mabao matano nyumbani kabla ya kufungwa tena wakienda Algeria.
Bado nashangazwa na watu wengi ambao hakuna
hata mmoja anakumbuka kumpongeza Mkwasa kuhusiana na uamuzi wake wa kuanza na Maguri
ambaye ni ‘Top Striker’ hapa Tanzania kwa sasa na kweli akafunga. Jiulize kama
asingefunga, huenda wengine wangelia sana kwamba alikosea kumuanzisha ndiyo
maana amechemka, bora angemuanzisha Ngassa!
Katika soka pia lazima tukubali, kocha
anaweza kuwa na mipango, ikafanya kazi au kugoma. Hivyo lazima twende na
mafunzo ya kila kinachofanyika.
Tumekuwa na makocha wa kigeni au Wazungu
kama Mart Nooij, huyu anatokea Uholanzi. Stars imefungwa mabao hadi matatu na
timu dhaifu kama Swaziland na Lesotho.
Lakini Watanzania leo wanalia au
kukasirishwa na sare dhidi ya Algeria. Jambo ambalo kwangu nalichukulia kama
hatua kubwa ya kimaendeleo ya soka nchini na hatupaswi kujilaumu na kama
tunaona alichokifanya Mkwasa ni kosa. Kwake litakuwa funzo kama aliona hivyo,
nasi tulitumie kama mafunzo badala ya kupoteza muda mwingi tukilalamika.
Kwamba tumeweza kutangulia kwa mabao mawili,
halafu tumeruhusu yote yarejeshwe. Hongereni Watanzania mliojitokeza kwa wingi
kuiunga mkono timu yetu, tuendelee kuiunga mkono kwa kuwa inacheza ugenini
Algeria na bado ina nafasi na mambo hakika yanawezekana.
SOURCE: CHAMPIONI
Watanzania ni mabingwa wa kulaumu, lazima tukubali kuwa Mkwasa alifanya kazi kubwa!! Hakuna aliyejua kuwa angeanza na Maguri lakini hilo bado hatulioni, asingefanya mabadiliko na tukafungwa watu bado wangelaumu kwa kutofanya mabadiliko ama kuchelewa kufanya mabadiliko!! Mpira una maajabu yake na lazima tujifunze kukubali matokeo, sio kila kitu siasa!!
ReplyDeleteSalehe umesema sawasawa kabisa kama ulikua kwenye kichwa changu, maana sisi watanzania tunajua kulaumu bana we acha tu...kama Ndemla na Ngasa wangefunga basi Mkwasa angekua Special one
ReplyDelete