Na Saleh Ally
TAIFA Stars ni timu ya taifa ya soka ya
kila Mtanzania. Hakuna anayeweza kujiita Mtanzania halafu akajigamba timu yake
ya taifa ya soka ni nyingine zaidi ya hiyo.
Kufanya vizuri au vibaya kwa Taifa
Stars kutakuwa maumivu kwa kila ambaye angetamani kitu au jambo kutoka ndani ya
taifa lake la Tanzania hasa kuona kikosi hicho kinafanya jambo lenye sifa njema
au ya kujivunia kwake na Watanzania wengine.
Taifa Stars Novemba 14, itakuwa
uwanjani kuivaa Algeria kuwania kupata nafasi ya makundi kuwania kucheza Kombe
la Dunia 2018. Kumbuka Algeria ni timu ambayo kama utazungumzia ubora wa
viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ndiyo inaongoza barani
Afrika.
Algeria ina wachezaji bora na
wanaotamba Afrika na Ulaya. Tunakubali ndiyo timu bora kwa maana hiyo. Je,
tuitoe Taifa Stars kwenye mapambano?
Kama jibu ni hapana, basi Taifa
Stars lazima iungwe mkono nayo ipambane kwa juhudi hiyo Novemba 14 ambayo ni
muhimu zaidi kwani itatoa majibu ya Taifa Stars ina mwelekeo gani kabla ya
mechi ya marudiano ya Novemba 17 ugenini.
Wapo ambao wameonyesha kuingia uoga,
mapema wamekuwa wakisema haitawezekana Taifa Stars kuifunga Algeria na kupata
nafasi ya kuingia kucheza katika hatua makundi.
Lakini wengine wametoa maoni yao
kwamba badala ya Taifa Stars bora kuanza kuziangalia timu za vijana kwanza.
Kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni,
lakini unaweza kugundua watoa maoni wanatazama mbali kiasi gani kulingana na
hali halisi lakini kikubwa kwa kila Mtanzania kuhakikisha anaweka mkono wake
kuisaidia Taifa Stars kwa maana ya kuipa nguvu pale uwanjani.
Kuiacha Taifa Stars leo litakuwa
ni jambo la kuchekesha sana, eti zianze kufanyika juhudi ya kukuza vijana.
Nafikiri hilo limekuwa likifanywa na TFF na wameshaeleza malengo yao lakini
msisitizo, vijana wanakuzwa na klabu zao kupitia vikosi vya watoto na vijana na
si shirikisho la soka.
Wakati huu ni kipindi sahihi cha
kuwa pamoja na kuonyesha uchungu wetu kwa taifa letu. Katika soka mengi
yanawezekana kuliko kuweka hisia hasi ambazo haziwezi kuwa na msaada.
Mtanzania usikubali kushawishika
kuwa Taifa Stars ni timu ya TFF, wao wamepewa jukumu hilo na wewe, mimi na
Watanzania wengine kuisimamia timu hiyo na kuhakikisha inafanya vizuri.
Huu ndiyo wakati wa kuonyesha
kwamba, Watanzania wanaweza kuungana pamoja na kufanya jambo fulani kwa ajili
ya utaifa. Kama kweli kutaonekana kuna matatizo, basi baada ya hapo tunaweza
kukosoana kutokana na tulichokiona ila itakuwa ni baada ya kuonyesha uzalendo
wa vitendo.
Lakini kama tukifanikiwa, bado
tutakuwa tumejifunza na tutajipongeza huku mafunzo tuliyoyapata tukiyafanyia
kazi.
Kama wakati huu hauungani na
Watanzania wengine kuisaidia Taifa Stars kwa kwenda uwanjani na kushangilia kwa
nguvu. Vipi utaweza kukosoa baadaye eti kikosi hakikufanya jambo fulani.
Atakayekosea kwa kuwa alikuwa
uwanjani, akaonyesha upendo wake, atakuwa na haki au ukosoaji wake utakuwa na
tija kuliko aliyekaa nyumbani ambaye sasa anapiga kelele nyingi bila sababu za
msingi.
Algeria wanaweza kuwa wagumu sana,
lakini ili Taifa Stars ivuke au kuleta kitu kipya au kuingia hatua nyingine,
lazima ivuke na kuzing’oa timu bora kwanza.
Algeria kuifunga Tanzania halitakuwa
jambo kubwa, lakini Taifa Stars ikawadondosha Waarabu hao wa Kaskazini, basi
litakuwa ni gumzo kubwa na hiki ndicho ambacho Watanzania wanapaswa kukipigania
kwa kuwa katika soka, mengi yanawezekana kuliko yanavyotarajiwa na ndiyo maana
mchezo huo umekuwa na mashabiki wengi zaidi duniani kuliko mingine kwa kuwa si
wenye majibu yenye uhakika kwa asilimia 100.
0 COMMENTS:
Post a Comment