Sali Ngwale, Lubumbashi
Unakumbuka kesho ni Jumapili, siku maalum kwa soka la Afrika kwa kuwa kwenye Uwanja wa TP Mazembe jijini
hapa, kikosi cha TP Mazembe kitacheza mechi ya marudiano ya fainali ya Ligi ya
Mabingwa Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Katika mchezo wa awali kwenye Uwanja wa Omar
Hamadi jijini Algiers, Algeria, Mazembe ilishinda mabao 2-1, hivyo wenyeji sasa
wanahitaji sare tu kutwaa ubingwa.
Kwenye kikosi cha Mazembe, wamo Watanzania
Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao wanaweza kuandika historia ya kutwaa
ubingwa huo wa Afrika endapo timu yao itabeba taji hilo.
Ukiachana na rekodi hiyo, Samatta ambaye ni
straika wa zamani wa Simba, pia anawania kutwaa tuzo ya ufungaji bora kwani ana
mabao saba sawa na Bakri Al-Madina wa El Merreikh ya Sudan ambayo imetolewa
awali.
Hii ni nafasi ya kipekee kwa Samatta kwani kama
akifunga hata bao moja atakuwa ametwaa Tuzo ya Ufungaji Bora Afrika na kuweka
rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufanya hivyo.
Baada ya mchezo huo, Samatta na Ulimwengu
watajiunga na kambi ya Taifa Stars huko Afrika Kusini kujiandaa na mchezo wa
kufuzu Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Algeria.
0 COMMENTS:
Post a Comment