Simba haitaki mchezo kabisa katika kujenga
kikosi chake, kwani imetenga kiasi cha dau la dola 50,000 ambazo ni zaidi ya Sh
milioni 100 ili iweze kumsajili straika wa Vital’O ya Burundi, Laudit Mavugo.
Nguvu yote hiyo imewekwa na Simba kuhakikisha
Mavugo anatua kikosini kwao aungane na Hamis Kiiza kuipa nguvu safu ya
ushambuliaji ya timu hiyo iliyofunga mabao 15 hadi sasa.
Awali kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu
Bara, Simba ilimtaka Mavugo na kumtangulizia dola 10,000 lakini uongozi wa
Vital’O uliweka ngumu ukitaka dola 100,000 ili umuachie straika huyo na dili
likaishia hapo.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya Simba,
uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais Evans Aveva, upo tayari kutoa dola 50,000
ili Mavugo asajiliwe na si zaidi ya hapo kwani ndiyo uwezo wa timu kwa sasa.
“Kama
asipotufanyia uhuni, basi tutamsajili lakini akileta tamaa ya fedha tutamwachia
aende zake, ila kusema kweli tunamuhitaji na tayari tumeshaanza naye
mazungumzo,” kilisema chanzo hicho.
Simba ina uhakika ikimpata Mavugo na kiungo
mshambuliaji Raphael Kiongera inayemrejesha kutoka KCB ya Kenya, basi itakuwa
na kikosi bora katika ligi.
Alipoulizwa Aveva kuhusiana na mpango huo,
alisema: “Ni kweli kabisa tuna mpango wa kumsajili Mavugo, ila kuhusu hizo
fedha ni nani aliyewaeleza? Nyie tambueni tunamtaka Mavugo.”
Hata hivyo, Mavugo amebakiwa na miezi mitano tu
katika mkataba wake na sasa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote ila
kuhusu kusajiliwa ni hadi klabu yake ikubali kuvunja mkataba. Kamati ya Usajili
ya Simba iliyo chini ya Mwenyekiti, Zacharia Hans Pope ndiyo yenye maamuzi ya
mwisho ya usajili.
0 COMMENTS:
Post a Comment