Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwamuzi Msaidizi katika mchezo
wa Mbao dhidi ya Rhino Rangers, Jilili Abdalah kutoka Singida, alijikuta
akipokea kichapo kutoka kwa wachezaji wa timu ya Rhino Rangers baada ya timu ya
Mbao kufunga bao la pili katika mchezo huo wa Ligi Daraja la Kwanza
uliomalizika kwa Mbao kuifunga Rhino kwa bao 2-0.
Rhino Rangers inamilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ulikuwa na
vurugu za hapa na pale. Wachezaji wa Rhino walianzisha vurugu baada ya mwamuzi
wa kati, Linus Joseph kutoka Arusha kutoa faulo iliyopigwa kuelekea lango la timu
hiyo na kuzaa bao ambalo lilifungwa na Ndanki Robers dakika ya 90.
Championi lilishuhudia mchezaji wa Rhino Rangers, James Mwambembe,
akipewa kadi nyekundu baada ya kumpiga mwamuzi msaidizi ambapo baada ya
mchezaji huyo kupewa kadi hiyo, vurugu zikaanza na kusababisha mchezo huo
kusimama kwa muda kabla ya kuendelea kwa dakika 2 na kisha mchezo huo
kumalizika.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika, wachezaji wa Rhino Rangers
walimvamia mwamuzi wa kati Linus Joseph na kuanza kumshushia kichapo kabla ya
kuokolewa na baadhi ya wanajeshi waliokuwepo uwanjani hapo.
Nao baadhi ya wadau wa soka waliokuwepo katika uwanja huo,
wamelaani vikali kitendo hicho ambacho kwa hakika siyo cha kimichezo.
“Sisi tumehuzunishwa sana na kitendo cha wanajeshi ambao wanajiita
wachezaji wa Rhino kumpiga mwamuzi, ni wazi kwamba TFF watapata taarifa ili
waweze kutokomeza vitendo hivi ambavyo havikubaliki katika soka,” alisema
shabiki mmoja.
Ikumbukwe kuwa, hii siyo mara ya kwanza kwa timu ya Rhino Rangers
kufanya vurugu katika michezo ya Ligi Daraja la Kwanza kwani hata msimu
uliopita, wachezaji wa timu ya Toto African walijikuta wakichezea kichapo
kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na kusababisha baadhi yao
kulazwa hospitali.
Katika tukio jingine, viongozi wa Rhino ambao wanasadikika kuwa ni
wanajeshi, walimnyang’anya kamera mpiga picha wa Clouds Media Group, Hamza
Mkuza na kumuamuru afute kila kitu alichokuwa akirekodi kwenye mchezo huo.
“Kwanza walinifuata wakanipiga kichwa huku wakinikaba na kuanza
kunilazimisha kuwa nifute kila kitu, vinginevyo kamera itavunjwa na mimi baada
ya kusikia hivyo, ikabidi nitii amri kwa kuwa sikuwa na la kufanya,” alisema
Hamza.
0 COMMENTS:
Post a Comment