Kumekucha kwani African Sports ya Tanga inafanya mazoezi kwa muda wa saa saba kwa siku huko Mwakidira lengo likiwa kujiweka sawa kuweza kuifunga Yanga Jumatano ijayo.
Ikiwa chini ya Ramadhan Aluko, ambaye ni kocha mpya aliyechukua nafasi ya Joseph Lazaro, African Sports inafanya mazoezi ya nguvu ikitana iifunge Yanga lakini kesho Jumapili inaanza na Coastal Union.
Katika mchezo wa kesho wa watani wa jadi, African Sports imedhamiria kuifunga Coastal Union ili ijinasue mkiani mwa Ligi Kuu Bara kwani ina pointi tatu tu katika mechi tisa ilizocheza.
Ofisa Habari wa African Sports, Muhasham Hamad amesema, kikosi chao kimeweka kambi eneo la Mwakidira nje kidogo ya Tanga.
Alisema kuwa timu inafanya mazoezi kwa awamu tatu kila siku na wanaamini mazoezi hayo yatakuwa na faida kubwa kwa timu yao ambapo itawafanya wapate matokeo mazuri katika mechi zao.
“Timu kwa sasa ipo Mwakidira inafanya mazoezi mara tatu kwa siku, wanaanza saa 12:00 mpaka 2:00 asubuhi, halafu saa 3:00 mpaka 5:00 asubuhi, na kisha alasiri kuanzia saa 9:00 mpaka 12:00 jioni.
“Tunafanya hivyo ili timu iwe katika hali nzuri kama ratiba inavyoonyesha tuna mechi mbili ngumu mfululizo hivyo lazima tujikoki tuwe sawa,” alisema Hamad.








0 COMMENTS:
Post a Comment