December 9, 2015


Na Haji Manara
RAUNDI ya kumi ya Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza tena Jumamosi hii kwenye viwanja mbalimbali nchini huku timu yenu pendwa, Simba Sports Club, ikiingia vitani dhidi ya Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati na vinara wa ligi, Azam FC.


Kiukweli ni mechi ngumu sana ukizingatia Azam namna ilivyo hivi sasa na pia rekodi baina yetu ambayo inaonyesha ushindi wa mechi sita kwa Simba na nne kwa Azam huku tukitoka sare mara nne kwenye jumla ya mechi kumi na nne.

Rekodi hizo na uwekezaji walioufanya Azam vinaonyesha ugumu wa mchezo huo muhimu kwetu ukizingatia hamu na matumaini ya Wanasimba kutwaa ubingwa msimu huu.
Kukiri ugumu wa mchezo huo hakumaanishi woga au kwa lugha ya kisasa mchecheto, la hasha! Ni kuonyesha heshima kwa wapinzani wetu, kama miiko ya fair play inavyoelekeza.

Azam katika siku za hivi karibuni, imeleta changamoto kubwa sasa kwenye mchezo wa soka nchini na sisi pamoja na ukongwe wetu, lazima tuwaheshimu, ingawa hatuna woga na matarajio yetu ni kupata pointi zote tatu kwenye mtanange huo unaotarajiwa kukusanya maelfu ya mashabiki kutoka kona zote za nchi hii.

Wanasimba wenzangu, pia sina budi kuwakumbusha jambo moja muhimu kuhusu mchezo huo na mengine itakayokuja ya ligi hii kubwa kabisa nchini.

Jambo la kwanza ni kuhusu usajili wa wachezaji wetu wapya tuliowaongeza kwenye dirisha hili dogo la usajili.
Nyote mnafahamu Mnyama ameongeza kiungo mshambuliaji wa pembeni kutoka Uganda na ambaye alikuwa akiichezea Azam FC, Brian Majwega, Novatus Lufungo na wajina wangu mshambuliaji chipukizi, Mtanzania Haji Ugando.

Pia Simba imemrejesha namba tisa wake, Mkenya Paul Kiongera aliyekuwa kwa mkopo katika timu ya KCB ya nchini Kenya.

Mbali ya hao, kupatikana kwa hati ya uhamisho wa kimataifa ya mshambuliaji hatari, Danny Lyanga, aliyekuwa akiichezea FC Lupopo ya DR Congo na kupona kwa beki mahiri wa kati, Mohammed Fhaki aliyesajiliwa kwenye dirisha kubwa kutoka JKT Ruvu kutasaidia kuongeza nguvu.

Sisi tunaamini kwa dhati kabisa kuwa uwepo wa nyota hao, umekidhi upungufu ulioonekana katika mechi tisa za kwanza za ligi ambazo tumeshinda saba na kupoteza mbili.

Kila mmoja kwenye uongozi anaamini kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa kikosi chetu na sasa tunalisaka kwa kila hali kombe letu tulilolipoteza kwa misimu mitatu.

Lakin Watanzania na wapenda mpira wa Tanzania, tunalo tatizo moja kubwa la kutokuwa wavumilivu kwa wachezaji, hususan wale wapya.

Nilikuwa nasoma mitandaoni Wanasimba wengi walitaka Kiongera arejeshwe kuitumikia klabu na sote tunajua aliyoyafanya nchini Kenya kwenye ligi yao iliyoisha mwezi uliopita.

Na sote tunamjua vizuri Majwega, hasa uwezo wake.
Tuwape nafasi sasa wacheze mpira na mfahamu si wachezaji wote wapya huanza vema kwa mechi za mwanzo tu. Wengine huchukua muda kidogo kuzoea.

Mfano wa hilo ni mchezaji bora wa Simba kwa miaka mitano Emmanuel Okwi ambaye kwa msimu wa kwanza alishindwa kuwapa Wanasimba kile walichokitarajia.

Tusiwazomee wachezaji wetu pale wanapokosea au kuharibu kidogo. Lazima tuendelee kuwapa moyo na kuwashangilia. Hii itawafanya wacheze kwa moyo na kuwajenga kisaikolojia zaidi.
Kama nilivyoandika awali, sisi uongozi tupo kamili kwa ligi hii na biashara lazima ianze kwa Azam, ndiyo maana tumeleta vifaa hivyo ili kurejesha heshima na furaha yetu. Sasa mashabiki, kama mchezaji namba kumi na mbili lazima na ninyi mtimize wajibu wenu. Msije uwanjani kama ‘picnic’. Mje kuihamasisha timu yenu kwa nguvu kubwa.

Mimi naamini uwepo wa Kiongera au 'Ekotite' na Majwega 'Selema', ukichanganya na wachezaji wengine, sioni Azam anatokaje na pia sioni ubingwa tutaukosaje msimu huu.
Kikubwa ni kuombeana uzima kwa wachezaji wetu na pia kuwaona marefarii wakizitafsiri sheria kumi na saba za soka kwa vitendo.

Mwisho niwaombe msiache kuvaa jezi zenu rasmi za klabu yenu pendwa Jumamosi wakati Simba ikiilamba koni tamu ya Azam.

MAKALA HAYA YALIANDIKWA KWA MARA YA KWANZA LEO KATIKA GAZETI LA MICHEZO LA CHAMPIONI.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic