Na Saleh Ally
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametangaza kuvunja kamati ya muda ya Stand United ambayo imekuwa ikiendesha timu hiyo baada ya kuundwa.
Kamati hiyo iliundwa baada ya figisu za muda mrefu na mwisho suala hilo likapelekwa hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Nassoro Lufunga ambaye aliamua kuunda kamati.
Kamati tayari ilianza mchakato ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya katiba. Ilionekana kabisa kwamba mabadiliko hayo yalilenga kuwaweka madarakani watu fulani.
Taarifa za ndani zilieza kwamba kuna mtu mmoja ambaye alishindwa katika uchaguzi wa Simba ndiye alikuwa akifanya juu chini kupata nafasi ya kuiongoza Stand United.
Hivyo figisu zote hizo ziliongozwa na mtu huyo kwa kushirikiana na kigogo mmoja ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye alitaka kumlipa fadhila mtu wake huyo ambaye ni swahiba wake.
Lengo la kutaka mtu huyo apate nafasi Stand United ni kwa kuwa alikuwa mtu wake wa karibu na alimsaidia sana katika uchaguzi wa TFF hadi anaingia madarakani.
Inawezekana kabisa mkuu wa mkoa hana kosa kwa kuwa hakujua mipango ya wahusika ambao walimuingiza ‘chaka’ kwa ajili ya kutimiza malengo yao.
Ukiangalia vita yote hiyo wala haikuwa ikihusisha maendeleo badala ya maslahi au kulinda matumbo binafsi na si maendeleo ya Stand United wala Wanashinyanga.
![]() |
| NAPE |
Waliokuwa wakifanya hivyo walikuwa wanapigania matumbo kwa kuwa wanajua Stand United kupitia kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Acacia kuna mkataba unaofikia Sh bilioni 2.
Kwa maana ya klabu na mkataba na wadhamini, ule wa Stand United na Acacia ndiyo mkubwa zaidi kuliko mingine. Kwa viongozi wenye njaa na waliougeuza mchezo wa soka kuwa mradi wa kuendesha maisha yao, waliona ndiyo sehemu sahihi ya kupigania.
Watu hao waliona ni jambo la kawaida kufanya dhuluma ya wazi, maana hakuna hata mmoja wao aliyewahi kuipigania Stand United ambayo ilianzishwa na walalahoi ambao ni wapiga debe wa mabasi yaendayo mikoani na ndani ya mkoa wa Shinyanga.
Watu walianzisha kitu si kwa ajili ya fedha, badala yake waliangalia suala la mapenzi yao kwa soka na furaha ya mioyo yao. Kwamba baada ya kazi ngumu ya kushinda wamesimama wakipiga kelele na kukimbilia abiria basi watakwenda kujifurahisha kwa kuwa soka ndiyo kipozeo cha mioyo yao.
Kutokana na mapenzi yao ya dhati, watu hao walipata maendeleo, kutoka daraja la chini kabisa kwenda la kwanza hadi mwisho wakapaa na kutua Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baada ya hapo, sasa wanaonekana hawafai kwa kuwa hawana digrii, hawafai kwa kuwa wanaishi Shinyanga na timu inaonekana inapaswa kuongozwa na watu kutoka jijini Dar es Salaam ambao wana akili nyingi kwa kuwa wanajua mengi sana kuhusu mpira.
Hao wa Dar es Salaam walikuwa wapi wakati wale makamanda wa Stand United wakiipigania timu yao kutoka kwenye mavumbi wakipanda mizizi kwenda kwenye shina na mwisho wake katika matawi yaliyobeba majani yaliyonawiri, ndiyo inaonekana inawafaa wajanja, walaji na wenye tamaa kutoka Dar es Salaam.
Ajabu zaidi, wale wanaoiongoza TFF ambao walipaswa kuwa watetezi wa wapenda soka kwa dhati, wanaopigania maendeleo ya mchezo kwa kujitolea, sasa inageuka mtetezi wa wale wanaotaka kula na kushibisha matumbo yao.
Asante Nape, huenda ujio wako ukawa ukombozi wa mchezo wa soka na mingine na kuanza kuwatafuna wababaishaji.
Kwani kabla, ilionekana TFF kama Serikali, tena ndani yake kuna viongozi wasio waaminifu ambao walivuruga mambo mengi makusudi huku wakiamini wao hawawezi kuguswa kwa kuwa mtetezi wao wa maovu Sepp Blatter yupo. Lakini Mungu ni mkubwa, naye amepigwa chini kwa kufungiwa miaka nane kutokana na wizi. Haya mawili, kufungiwa kwa Blatter na ujio wako, huenda ni ukombozi mpya wa soka Tanzania. Karibu tena.








0 COMMENTS:
Post a Comment