December 18, 2015


Na Saleh Ally
MOJA ya sakata linaloshika vichwa vya habari katika vyombo mbalimbali nchini ni kuhusiana na kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima.

Tayari uongozi wa Yanga umetangaza kumsimamisha kwa muda usiojulikana ukimtuhumu kwa utovu wa nidhamu. Kwamba kila kiungo huyo mkongwe anapoondoka kwenda kwao Kigali, Rwanda amekuwa akichelewa kurejea kambini.

Imeelezwa Novemba 4, mwaka huu, uongozi wa Yanga ulilazimika kufanya mkutano mdogo kati ya Niyonzima na kamati ndogo iliyoteuliwa kulimaliza suala lake la kuendelea kuchelewa kurejea kazini kila anapoitwa timu ya taifa.

Uongozi wa Yanga pia umeshusha shutuma kwamba Niyonzima hakucheza mechi dhidi ya Azam FC kwa kuwa alichelewa kurejea katika timu ya taifa wakati mchezaji kama Jean Baptiste Mugiraneza alirejea mapema na kuichezea Azam FC katika mechi hiyo.

Taarifa zinaeleza Niyonzima aliwahi kuondoka nchini kutokana na kufiwa. Yanga ilicheza na Mtibwa Sugar bila yeye kuwa pamoja na kikosi. Akiwa Rwanda akateuliwa katika timu itakayoshiriki michuano ya Chalenji Ethiopia, lakini Shirikisho la Soka Rwanda (Ferwafa), wala yeye hawakutuma barua au taarifa yoyote kwa Yanga.

Kumekuwa na taarifa pia kwamba Niyonzima hana uhusiano mzuri na Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, hivyo anaamini anasakamwa kwa makusudi. Shida imekuwa ni vigumu kumsikia Niyomzima akiliweka hili hadharani.

Huenda nianzie hapo, kwamba inawezekana Niyonzima akaanza kuhisi kuwa Dk Tiboroha hampendi kwa kuwa anakutana naye katika mambo kadhaa ambayo yanakuwa yanahusisha lawama au kukosoana baada ya yeye kutenda jambo.

Kama Dk Tiboroha kweli atakuwa hana uhusiano mzuri, kuna hana ya kumuita Niyonzima kama kijana wake wakakaa na kuyajadili mambo na lazima wajue kwamba wao wawili ni watumishi wa Yanga na wanalazimishwa kuwa na umoja ili kutimiza lengo la kuwapa mkataba ili waisaidie klabu na timu kupata mafanikio kwa maana ya faida na heshima.

Ukiachana na hivyo, mimi kama binadamu nimekuwa na mawazo au nimeliangalia tofauti kabisa suala hilo.

Historia inaonyesha wachezaji wengi wakitaka kuondoka katika klabu fulani kama wamepachoka au wanaona hawana furaha huanza vituko ikiwa ni pamoja na kukosa mazoezi kwa makusudi, ilimradi kuwaudhi waajiri na mwisho wawape nafasi ya kuondoka. Mmeona katika klabu nyingi hasa za Ulaya hili likifanyika.

Nikaingia katika mawazo kwamba mwaka 2015 ni mwafaka kwa Niyonzima kuondoka Tanzania na kurejea Rwanda na huenda ni malengo ambayo anataka kuyatimiza kwa kuwa anaona mapenzi yake na Yanga yamepungua, au mfumo uliopo haumpi furaha tena lakini inaonekana amelenga kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) ambayo mwakani itafanyika katika ardhi ya kwao ya Rwanda.

Hii ni mara ya kwanza michuano hiyo kufanyika katika ukanda wetu, Niyonzima ni nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda. Hakuna ubishi kwa binadamu yeyote angependa kuungana na taifa lake na kuletetea katika kipindi kama hicho. Tena ukizingatia, kwa Niyonzima hiyo itakuwa ni michuano yake mikubwa katika kipindi hiki.

Haya ni mawazo yangu; lakini kama yatakuwa na ukweli na Niyonzima akaona niko sahihi basi namshauri kukutana na uongozi wa Yanga na kuueleza ukweli kwamba ana nia njema na taifa lake na angetaka kwenda kwa kupitia njia fulani.

Kama kuna klabu ya Rwanda inamhitaji ambalo ni jambo linalowezekana, basi ifike na kufanya mazungumzo na Yanga na mambo yaende kwa ulaini kupitia taratibu na makubaliano. Yeye arejee nyumbani na kuichezea Rwanda.

Si sahihi kwa Niyonzima ambaye ametoa mchango mkubwa kwa Yanga, mashabiki wakampa heshima kubwa. Akajenga undugu na urafiki na wengi, aondoke kwa kufarakana. Binadamu wanakosea, lakini bado kila upande iwe Yanga au Niyonzima, aliyekosea arekebishe.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic