Wakati Simba ikitarajiwa kushuka dimbani kesho Jumamosi kuwavaa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, jina la straika wao tegemeo, Hamis Kiiza limewekewa nyota na kocha mkuu wa Toto, Mjerumani Lukas Stellmach kuwa ndiye mtu hatari na lazima apewe ulinzi wa kutosha katika mchezo huo.
Mjerumani huyo ambaye amechukua mikoba ya Mjerumani mwenzake, Martin Grellics, aliyejiuzulu mwezi uliopita, amekiri mchezo huo kuwa mgumu lakini akajipa matumaini na uwepo wa wachezaji wa zamani wa Simba wakiongozwa na Edward Christopher ‘Edo’ kuiangamiza Simba.
“Karibu mechi zote za Simba nimeziangalia, ukiacha ya Jumamosi (dhidi ya Azam). Ni timu nzuri na safu yao ya ushambuliaji ni nzuri na ina watu hatari wanaoendana na mahitaji ya mchezo…Kiiza ndiye anaonekana kusumbua sana, lakini nina imani ya vijana wangu watamdhibiti yeye na wenzake,” alisema.
Aidha, Stellmach alisema hali ya ukata inachangia kuharibu mikakati yake ya kukijenga kikosi hicho na kushindwa kutimiza baadhi ya progamu zake.
0 COMMENTS:
Post a Comment