December 26, 2015


Na Saleh Ally
MESUT Ozil alizaliwa miaka 27 katika mji mdogo wa Gelsenkirchen nchini Ujerumani, asili yake ni nchini Uturuki ambayo ndiyo nchi iliyo katika mabara mawili.
Asilimia takribani 15 ya ardhi ya Uturuki iko barani Ulaya na iliyobaki iko Asia. Lakini Ozil ni Mjerumani ambaye amezaliwa na kukulia na sasa ni mchezaji tegemeo wa timu ya taifa ya Ujerumani.

Utakuwa unamkumbuka akiwa Real Madrid ambako alitamba zaidi, lakini, Ozil ameingia katika rekodi ya mchezaji aliyevunja ubahili wa Kocha mchumi Arsene Wenger wa Arsenal, ambaye alikubali ‘kuvunja benki’ na kumnunua kwa kitita cha pauni milioni 42.5.

Kununuliwa kwa Ozil katika kikosi cha Arsenal yalikuwa ni kama mapinduzi, kwani Wenger akawa amerejea katika kuanza kununua wachezaji walio tayari, si wanaohitaji kutengenezwa, kwani baadaye alifuatia Alexis Sanchez na wote walicheza La Liga katika timu vigogo kama Real Madrid na Barcelona.

Wajerumani wamembandika maneno haya “finesse and improvisation”. Mtu mwenye uwezo mkubwa wa kudanganya, kuchanganya, kutimiza anachotaka na kuburudisha.
Ozil sasa ndiye gumzo unapoizungumzia Arsenal ambayo inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kubeba ubingwa ili kufuta machungu ya mashabiki wa Arsenal walioukosa ubingwa kwa zaidi ya miaka 10.

Msimu uliopita hasa mwishoni, Ozil alionekana kuishindwa Arsenal na baadhi ya wachambuzi wa soka nchini England wakaanza kuamini Wenger aliingia mkenge kumnasa Mjerumani huyo mwenye sura ya upole, lakini mjeuri sana akikasirika au kutofurahia kitu.

Ozil hakuwa yule waliyemtegemea, kitu ambacho kiliwashangaza wengi ni kuwa mashabiki wa Real Madrid walipigana ile mbaya kuhakikisha mtaalamu huyo haondoki kwa kuwa waliamini haikuwa sahihi, lakini walishindwa kwa kuwa hawana mamlaka ya mwisho katika uamuzi.

Wenger akaendelea kushikilia msimamo wake, kwamba Ozil ataendelea kubaki Arsenal kwa kuwa anahitajika pia ni msaada mkubwa. Lakini wako waliolalamika kwamba vipi mbona hafungi wakati alinunuliwa ghali? Wenger akawaambia: “Ozil ni dereva wa kikosi.”

Huenda ilikuwa si rahisi kumuelewa ingawa taratibu majibu yanaanza kupatikana kwani Ozil ndiye anaongoza kwa kutoa pasi nyingi za mabao katika kikosi cha Arsenal hadi sasa.

Mkali huyo ambaye anafanya mpira uuone rahisi anavyocheza kwa kujiamini, ametoa pasi 15 katika mechi 15 za Ligi Kuu England alizocheza msimu huu akiwa na kikosi hicho cha Wenger.

Ozil amepata wastani wa juu zaidi Ulaya kwa kuwa ana pasi 15 katika mechi 15 ikiwa na maana amesababisha bao katika kila mechi aliyocheza kama utazungumzia wastani. Pia amefunga mabao mawili katika dakika 1293 alizoichezea Arsenal msimu huu kwenye Ligi Kuu England.


Pia anaonyesha ni hatari kwa kuwa asilimia 60 ya pasi zake za ndani au nje ya 18 ndiyo zimezaa mabao huku asilimia 40 zikiwa ni krosi.

Ubora wa Ozil ulikuwa unatakiwa na Wenger, yeye alikuwa akijua kwa kuangalia rekodi na utendaji. Mashabiki na wachambuzi walikuwa na haraka kwa kuwa waliangalia fedha ambazo Arsenal imelipa na walitaka mchezaji ghali afunge mabao mengi, jambo ambalo Wenger alionyesha si sahihi na sasa Ozil kweli ni dereva wa kikosi.

Huenda itakuwa rahisi wengi kujua Arsenal ina matatizo kama Ozil ataumia. Yeye ndiye anashikilia mfumo wote wa uendeshaji timu na hasa linapofikia suala la umaliziaji.
Wenger alijua ndiyo maana akaendelea kutaka kumpa muda akijua ana nafasi ya kufanya vema kama atacheza katika kiwango chake.

Kocha huyo Mfaransa alikuwa ameangalia mambo mengi na kwa kuwa ni mtaalamu isingekuwa rahisi kukubaliana na wengine kwamba Ozil si mwenye msaada katika kikosi chake.

Kwa rekodi, zinaonyesha Mjerumani huyo si mfungaji bora. Badala yake ni mtoaji pasi bora kabisa barani Ulaya na hilo linathibitishwa na rekodi ndiyo maana Kocha Jose Mourinho aliwahi kumfananisha na Zinedine Zidane.

Msimu wa 2010-11, Ozil alishinda kuwa mchezaji wa kiwango cha juu zaidi kuliko wote Ulaya kwa utoaji wa pasi za mabao au asisti baada ya kugawa pasi 25 katika michuano ya ndani na Ulaya.


Msimu wa 2011-12, Ozil tena akaibuka mtoaji basi bora wa mabao wa La Liga akiwa na Madrid, alitoa pasi za mabao 17.

Kama hiyo haitoshi, alionyesha kuwa yeye ni ‘pass master’ baada ya kutangazwa mtoaji bora wa asisti katika Michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, nchini Afrika Kusini ambako gazeti hili lilimshuhudia live, pia Michuano ya Uefa Euro 2012, ambako pia alikuwa mtoa asisti bora.

Hii ilikuwa ni sababu tosha kwa mashabiki wa Real Madrid kulia asiondoke, lakini ilikuwa ni sababu pia kwa Wenger kumvumilia azoee mazingira ya Arsenal na England ili aanze mambo yake na sasa ndiyo hayo unayoyaona.

Kitita cha pauni milioni 42.5, kilichovunja ubahili wa Wenger kilimfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kununuliwa kwa fedha nyingi kama hizo kutoka Ujerumani.

Ozil ana akili nyingi, ana uwezo mkubwa wa kutambua ubora wa wachezaji wenzake na nini cha kuwafanyia kutokana na alichowaona wanacho. Hivyo ni rahisi kuendelea kuifanya Arsenal iendelee kung’ara, ikiwezekana kutwaa ubingwa.

Si mfungaji mzuri, lakini bado ana uwezo mkubwa wa kufunga hasa kama akipata nafasi. Usisahau, Ozil ndiye alikuwa mfungaji mwenye mabao mengi katika kikosi cha Ujerumani kilichobeba Kombe la Dunia nchini Brazil, mwaka jana.


Ozil alitupia nyavuni mabao nane na kuwa mfungaji bora zaidi kwa Wajerumani katika kufuzu Kombe la Dunia 2014, pia alikuwemo katika kikosi cha kukata na shoka kilichowaadhibu wenyeji Brazil kwa mabao 7-1 na kuweka rekodi ya kipigo kikubwa kwa mwandaaji wa Kombe la Dunia.

Ubora wa kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani umekuwa juu mfululizo kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Ozil amekuwa katika kikosi hicho tangu mwaka 2009, tena ana nafasi ya kucheza. Amekuwa timu ya taifa ya vijana tangu mwaka 2006. Hii ni sehemu tosha ya kuonyesha huyu jamaa ni mchezaji hasa na wala si wa kubabia.


ALISABABISHA MABAO NA PASI ZA…
KICHWA……..0%
KROSI………..40%
PASI…………..60%
KROSI    39

MASHUTI LANGONI
Kapiga …………..13
Kipa kuokoa…….60%
Mguu wa kushoto…..80%
Mguu wa kulia………20%

MASHUTI YASIYOLENGA
Nje kushoto…………..20%
Nje kulia…………….80%
Kupiga mwamba……0%


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic