December 19, 2015


Na Saleh Ally
MAISHA yana safari ndefu sana, ingawa hakuna mwenye uwezo wa kujua urefu wa maisha kwa kuwa yote ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Mungu ndiye anapanga kuhusu urefu au umri wa maisha ya mwanadamu. Lakini hilo halikuzuii kupanga mipango ya baadaye kwa kuwa kweli haujui mwisho wako utakuwa lini.

Wanasoka ni kati ya wanadamu wenye uwezo wa kupata malipo au fedha nyingi sana kama wataitumia nafasi yao kitaaluma au vipaji vyao kwa njia sahihi wakiwa ni wenye lengo la kutimiza ndoto zao.

Unajua wapo watu wanakwenda shule, wanasoma na kuhitimu kwa kiwango cha juu, lakini kamwe hawakuwahi kuishi kwa raha au kwa uwezo mkubwa kifedha kama wanasoka ambao makini waliofanikiwa kutokana na juhudi kazini kwao.

 Mishahara ya wachezaji kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Wayne Rooney, Yaya Toure na wengine ni kufuru. Malipo yake ya wiki, yanaweza kuwa mtaji wa Watanzania zaidi ya 100 ambao wataendesha maisha yao vizuri kabisa na wakiwa makini, hata kwa zaidi ya miaka 10.

Hapa nyumbani, wanasoka pia wanalipwa mishahara bora kabisa. Sh milioni 4 kwa mwezi, hakika si haba na hiyo bado Tanzania haijaingia katika ligi ya kulipwa.

 Kweli wachezaji wageni wanalipwa fedha nyingi zaidi, lakini hata wa hapa nyumbani, wapo wanaopata fedha ambazo zinaweza kuingia kwenye sifa ya kuwa mishahara bora kutokana na kiwango cha maisha ya Mtanzania wa kawaida.

Ronaldo ameonyesha jambo, linaweza lisiwe geni lakini likawa ni sehemu ya kuwafumbua macho na kuyalegeza masikio ya wachezaji au wanamichezo Watanzania kusikia kwamba, soka si rafiki wa muda mrefu.

 Kitaalamu inaonekana hivi; binadamu huweza kucheza soka la kiushindani ndani ya miaka 10. Baada ya hapo, anakuwa anaendelea kujifurahisha au atakuwa akicheza huku akijulikana kama mkongwe.

 Anayecheza miaka 10 soka la ushindani ni yule ambaye amejaaliwa kuwa na afya njema zaidi bila ya majeruhi au mambo mengine ambayo yangepunguza kasi yake kiuchezaji.


Ronaldo ameliona hilo, amekuwa ni mfanyabiashara miaka minne sasa, ingawa kuanzia miaka miwili iliyopita, alichanganya vilivyo hadi jana alipozindua mpango wa hoteli zake nne utakaomgharibu hadi pauni milioni 54 (zaidi ya Sh bilioni 170.7).

 Wakati wa uzinduzi wa mpango wa hoteli hizo zitakazokuwa katika miji ya Funchal, Lisbon (yote Ureno), Madrid (Hispania) na New York (Marekani), Ronaldo amesema anajua uchezaji soka una muda wake na yeye angependa kuendeleza maisha kwa raha baada ya hapo.

Ronaldo amesisitiza kwamba hoteli hizo chini ya Kundi la Pestana ambalo litasimamia viwango vya ubora, amezipa jina la CR7, nembo yake ya kibiashara ambayo angependa kuilinda kwa maisha yake yote kwa kuiendeleza.

Ronaldo amekuwa akiuza nguo za ndani, soksi na vitu mbalimbali. Sasa ameamua kuangalia mbali zaidi kwa kuingia katika biashara ya hoteli. Biashara ambayo ina uwezo wa kufanya vizuri kwa miaka mingine 100 na ikasaidia watoto, wajukuu na vitukuu kama itaendelezwa kiufasaha.


 Mchezaji wa Kitanzania ambaye anapata mshahara ambao anaweza kuwekeza hata kidogo, hawezi kujenga hoteli kama za Ronaldo. Lakini mradi wowote ambao unaweza kuendana na anachokipata. Yupo anayefikiria hivyo?

Tofauti au kitu kibaya ambacho huwaongoza wachezaji wengi ni kuamini kununua gari zuri na kupanga Sinza, Kinondoni au sehemu zinazoonekana wanaishi watu maarufu, inakuwa ndiyo mwisho wa maisha ya wachezaji.

Tuache unafiki na kuoneana aibu, hakika wachezaji wengi sana wakongwe ambao sasa wameshastaafu kucheza soka, wanateseka na maisha yao ni duni sana.

Wapo wanaoishi hivyo kwa kuwa kipindi chao hawakuwa na nafasi ya kuingiza fedha nyingi. Wapo walioingiza wakazitumia vibaya wakiamini wataendelea kucheza tu soka na sifa kibao.
Wachezaji lazima sasa waamini kwamba kila mfalme ana zama zake na zama za wanasoka hazina muda mrefu, hivyo wakumbuke kesho.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic