December 19, 2015


Na Saleh Ally
KATIKA makala ya jana, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart John Hall alieleza mambo mengi sana kuhusiana na kikosi chake na soka la nyumbani.

Katika makala ya jana, Hall raia wa Uingereza alichambua mambo kadhaa likiwemo lile kuhusiana na mipango yake kwenda kwenye ubingwa.

Hall alieleza namna ambavyo Azam FC haiangalii kwa jicho kali suala la kukaa kileleni. Badala yake ni mipango ya hesabu na wanataka pointi ngapi ili kubeba ubingwa wa Tanzania Bara.

Baada ya kuwa ameizungumzia mechi ya Simba; likaingia suala la upana wa kikosi chake na swali la mwisho ambalo hakuwa amelijibu ni lile kwamba vipi amekuwa akimbania Didier Kavumbagu hadi anafikia kutaka kuondoka?  Sasa endelea…

SALEHJEMBE: Kweli una kikosi kipana, lakini kwa nini umekuwa ukimbania Kavumbagu kwa kumuweka nje hadi anafikia kutaka kuondoka?
Hall: Hili suala watu wengi hawajui linavyokwenda, nafikiri maneno mengi si sahihi. Kwanza kama nilivyokueleza, wachezaji watacheza kwa kupeana nafasi na unajua mwenyewe umesema nina kikosi kipana.

SALEHJEMBE: Lakini Kavumbagu anaona yeye ni kama anakaa sana nje na anataka kucheza?
Hall: Kila mmoja anataka kucheza, lakini nikueleze, watu hawajui Didier amekuwa na matatizo makubwa ya kifamilia. Unajua Burundi kuna vita na yeye familia yake ilikuwa katika hali si ya usalama.

SALEHJEMBE:  Alikuambia asingeweza kucheza kutokana na matatizo hayo?
Hall: Hapana, mimi ni kocha napaswa kuona na kusoma vitu haraka. Mfano mara mbili tumempa ruhusa kwenda Burundi kushughulikia suala hilo na mwisho aliileta familia yake Dar es Salaam.

SALEHJEMBE:  Kulikuwa na mabadiliko baada ya Kavumbagu kufanikisha hilo?
Hall: Kabisa, kulikuwa na mabadiliko makubwa na aliporejea mazoezini alikuwa amechangamka na nilipompanga mara mbili, alifunga mabao mawili kila mchezo.
KAVUMBAGU
SALEHJEMBE: Nimesikia unazuia asiondoke, hutaki auzwe?
Hall: Kabisa, nilisikia kuna timu inamtaka Sweden, nikamruhusu aende. Lakini kama hapa (Tanzania) au Afrika Mashariki, hakuna nafasi ataendelea kubaki Azam, huo ni msimamo wangu.

SALEHJEMBE: Una washambuliaji wa kati watano katika kikosi chako, huoni ni matumizi mabaya?
Hall: Mabaya kivipi? Wewe ndiye unafikiria hivyo lakini haujui ninachofanya. Kila mmoja ana aina yake na maana yake.

SALEHJEMBE: Unaweza kufafanua angalau kidogo?
Hall: Bocco unamuona, ana nguvu, kasi kiasi lakini anafunga mabao. Kipre ni mtu wa ufundi, ana kipaji, anaweza kutengeneza na kufunga pia.
Didier ni mrefu, hauwezi kumpokonya mpira, anapiga mipira ya vichwa vizuri. Ikiwa mechi ya nguvu na vurugu, nitamuweka Ame Ali. Lakini Wanga hata hauwezi kumuona lakini anafunga. Ninaangalia hapa na kimataifa, niacheni najua ninachofanya.

SALEHJEMBE:  Unakwenda kucheza na Majimaji ambao wametoka kutwangwa na Toto Africans nyumbani kwao Songea kwa mabao 5-1, umejiandaa vizuri?
Hall: Najua watakuwa wanataka kurudi, tena watakuwa wamejiandaa kubadilisha hali ya hewa. Lakini sisi tutakwenda kucheza bila ya kujali matatizo yao.

SALEHJEMBE:  Unaposema matatizo, maana yake nini?
Hall: Nimesikia walikuwa na matatizo ya kutolipwa mishahara, imechangia wao kutokuwa katika kiwango kizuri. Sisi tutaenda tukiwa hatujali wamelipwa au la, badala yake tunakwenda kucheza kwa kutaka kupata pointi, tena tatu.

SALEHJEMBE:  Unajua Uwanja wa Majimaji unazungumziwa kuhusiana na kuwa na kiwango cha chini kabisa kwa maana ya ubora?
Hall: Si geni kwangu hilo, kama kiongozi wa benchi la ufundi, tumelifanyia kazi na sasa tunafanya mazoezi kwenye uwanja mbovu ili kuendana na hali halisi.

SALEHJEMBE:  Mtafanya mazoezi kwa muda gani katika uwanja huo wenye kiwango duni?
Hall: Nimepanga tufanye mara tatu, halafu tutafika Songea na kufanya mara moja kwenye uwanja huo wa Majimaji. Baada ya hapo nafikiri tutakuwa tayari kwa ajili ya mechi.

SALEHJEMBE:  Unakwenda kwenye Kombe la Shirikisho, ninaamini kabisa utakutana na Bidvest, moja ya timu bora za Afrika Kusini. Azam FC imekuwa ikifeli kwenda mbali, unalizungumziaje?
Hall:  Kwanza nikuambie nikiwa na Azam FC kabla ya kuondoka tulifika 16 bora. Nilipoondoka nilisikia walikwama mapema hata kwenye ligi ya mabingwa.


SALEHJEMBE:  Ndiyo maana nikakuuliza, umejiandaa maana timu za Afrika Kusini ziko imara maana zina mazingira bora ya maandalizi?
Hall: Najua, Azam tuliwahi kuweka kambi Afrika Kusini, tukacheza na Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates na Molloka Swallows. Naujua ubora wao, pia tumejiandaa na ukienda katika michuano mikubwa kama hiyo ujue unakwenda kukutana na timu bora lazima ujiandae na uwe tayari.

SALEHJEMBE:  Kwa mwendo inayokwenda Azam FC inaonekana kama imezima ufalme wa Simba, sasa ni Yanga na Azam FC ukizungumzia ubingwa au nafasi ya pili. Hili litadumu?
Hall: Kabisa, kuna uwezekano likadumu au Azam FC ikaja kuwa mfalme hasa. Uongozi wa Azam FC ni tofauti kabisa na mambo yanakwenda kitaalamu si kama Yanga na Simba.

SALEHJEMBE:  Si kama Yanga na Simba unamaanisha nini?
Hall: Unasikia migogoro kila kukicha, wachezaji wanalalama, viongozi wanazozana, timu hadi leo hazina hata viwanja vya mazoezi na sina umri zaidi ya miaka 50, kichekesho kabisa.

SALEHJEMBE:  Nini hasa nguzo ya Azam FC?
Hall: Chamazi.

SALEHJEMBE: Fafanua, kwa nini Chamazi.
Hall: Familia ya Bakhresa imewekeza Chamazi. Ni mamilioni ya fedha, lakini ile ndiyo nguzo ya Azam FC kwa kuwa inaweza kujiandaa kwa uhakika maana kuna kila kitu pale utafikiri timu ya Ulaya. Nasema tuna kila kitu kwa maana ya vifaa na mazingira bora. Kamwe hatuwezi kuwa na malalamiko hata tukipoteza mechi.


Lakini kama tukitaka kukuza vijana, mpangilio ni bora, viwanja vipo, vifaa vipo, sehemu ya kulala ni bora. Watoto pia wanatunzwa pia nina uhakika wachezaji bora wenye matunzo bora kisoka kwa miaka 10 ijayo watakuwa wakipatikana kwenye akademi za Azam FC wakati huo Azam ikiwa ndiyo klabu bora kabisa Tanzania na ikiwezekana barani Afrika.

MAKALA HAYA KWA MARA YA KWANZA YAMETOKA LEO JUMAMOSI KATIKA GAZETI LA CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic