Na Saleh Ally
NIANZE kwa kukumbusha baadhi ya
Watanzania kuhusu wanasoka wanaotembelea moja ya magari ghali ya Range Rover
katika soka.
Nawajua John Terry wa Chelsea, Wayne
Rooney wa Manchester United, Kolo Toure wa Liverpool, Gareth Bale wa Real
Madrid na wengine kadhaa. Yanaweza kupishana thamani, lakini ndiyo Range Rover.
Labda hapa nyumbani acha nikukumbushe
wafanyabiashara maarufu wanaotumia gari la aina hiyo la Range Rover; Mwenyekiti
wa Yanga na milionea, Yusuf Manji, milionea mwingine Simba damu, Mohammed
Dewji, milionea Tanil Somaiya na wafanyabiashara wengine wachache walionazo.
Lakini nataka nikuambie kitu
ambacho huenda ulikuwa haukijui au ulikijua lakini ukawa umekisahau kwamba
wanasoka pekee wanaotembelea magari hayo ghali ni Mbwana Samatta na Thomas
Ulimwengu wanaokipiga TP Mazembe ya DR Congo.
Wawili hawa, huenda ndiyo
Watanzania wenye umri mdogo zaidi kuwahi kumiliki gari ya aina hiyo ambayo
thamani yake ni kuanzia Sh milioni 80 kwenda juu.
Jamani, hata Ulimwengu anamiliki
gari aina ya Range Rover ambalo huenda wafanyabiashara kibao maarufu inakuwa
vigumu kuingia kwenye bajeti ya kulinunua. Kwani uendeshaji wake, (si ule wa
kukaa kwenye kiti) ni ghali sana, mfano matengenezo au ununuzi wa vipuri.
Kilichosababisha kuandika makala
haya, nilikuwa nikiperuzi mambo kadhaa mtandaoni, nikaona picha ya Ulimwengu
akiwa nyuma ya usukani ulioandikwa Range Rover. Alikuwa ameweka maelezo kwamba
anatokea Morogoro kwenda Dodoma kumsamilia na ‘kudeka’ kidogo kwa mama yake.
Niliganda kwenye picha hiyo na
kufikiri mambo mengi sana, mwisho nikatabasamu. Pia nikakumbuka mengi ambayo
nimeona litakuwa ni jambo jema ‘kushea’ nanyi kuhusiana na hili.
Miaka minne na ushee iliyopita,
Ulimwengu alikuwa akifika ofisini kwangu Global Publishers pale Bamaga na
kunisubiri nje nikiwa naendelea na shughuli zangu. Baada ya hapo nilitoka na
kuongozana naye kwenda kwenye ubalozi wa Sweden ambako nilikuwa nikimsimamia
kupata visa baada ya klabu AFC ya huko kumhitaji.
GARI KAMA ANALOMILIKI ULIMWENGU. |
Rafiki zangu wawili
walishughulikia safari yake, mmoja akiwa hapa Tanzania na mwingine Sweden.
Hivyo niliwasaidia wao, lakini Ulimwengu ambaye hakika hakuwai kuchelewa hata
siku moja kwa kuwa alionyesha kweli alipania kwenda Sweden.
Alikwenda, baadaye akarejea na
mwisho tukaanza tena utaratibu huo wa kushughulikia visa. Wakati akija ofisini
kwangu, alikuwa akitumia daladala, hakuwa hata na baiskeli nafikiri kwa kuwa
sikuwahi kuiona.
Usisahau, Ulimwengu alikuwa
akitegemea usafiri wangu kwenda ubalozini na sehemu nyingine tulizokuwa
tukihitaji kufika.
Miaka minne na ushee, Ulimwengu
anamiliki Range Rover, gari ambalo lina thamani mara kumi au zaidi ya lile
langu alilokuwa akilipanda. Tena anamiliki na mengine zaidi ya hilo.
Hapo ndipo nilipoanzia kuwaza
mambo mengi sana, hapa lengo si kukuelezea urafiki wangu na Ulimwengu lakini ni
kukuonyesha mambo yanavyoweza kuwezekana hata kwa vijana wetu wa Kitanzania na
pia ndani ya Afrika.
Kuwezekana:
Kuna watu wengi wanaamini mafanikio ni
lazima mtu ahitimu elimu tena kwa kiwango cha digrii, nafikiri ni fikra finyu
kabisa. Nchi nzima hawawezi kwenda shule na wote kuhitimu kwa kiwango cha juu.
Hata Lionel Messi na Ronaldo hawana digrii na wamefanikiwa.
Kikubwa ni watu kuangalia katika ndoto
zao na mwisho kuhakikisha wanafanikiwa kuzifia tena kwa nidhamu kuu.
Maisha ya Ulimwengu wa miaka minne tu
iliyopita si huyu wa sasa na lazima tukubali kwamba amefanya juhudi kubwa.
Kwani hata maisha yake alikuwa akilala kwenye hosteli za TFF na mazingira si
bora, lakini alijua anatafuta nini.
Vijana wengi wa Kitanzania hawataki
kujaribu, hawako tayari kuingia kwenye mateso au shida na wanataka mambo yaende
kwa ulaini utafikiri filamu., ndiyo maana wanakwama. Ulimwengu awe shule kwenu.
Afrika:
Bado vijana wengi wanasoka wanaamini
mafanikio hadi Ulaya ambalo ni jambo potofu kabisa. Ulimwengu anaendesha gari
kama la Rooney au Terry na anacheza soka barani Afrika.
Leo yuko Japan na TP Mazembe kucheza
Kombe la Dunia la klabu, Cristiano Ronaldo hana nafasi hiyo wala Raheem
Sterling hajawahi kucheza katika michuano hiyo.
Hii inaonyesha hata Afrika kunaweza kuwa
na mafanikio makubwa kulingana na mtu au watu wanavyoamini au walivyojipanga.
Wakati mwingine vema kuanza kutafuta
mafanikio nyumbani, nje ya nyumbani kuanzia karibu au jirani na sasa nafasi ya
Ulimwengu kwenda Ulaya ni laini zaidi.
Kumbuka, Ulimwengu alitoka Sweden kwenda
TP Mazembe, huenda alionekana hana lolote. Usisahau Ulimwengu alifeli majaribio
Hamburg ya Ujerumani wakati huo staa pale akiwa Ruud van Nisterlooy. Lakini
Ulaya kwake si kitu kigumu tena, anacheza Kombe la Dunia. Niseme najivunia
alipofikia Ulimwengu kama Mtanzania, bado ninaamini kuna wengi sana wanaweza
kufikia hapo na zaidi na nikajivunia pia. Ewe mchezaji kinda, soma haya makala,
tumia muda wako kutakari, uamuzi wa maisha yako ni wako. Kila la kheri.
0 COMMENTS:
Post a Comment