WAZIRI NAPE AKIWA OFISINI KWAKE |
Na Saleh Ally
KAMA utazungumzia moja ya vitu vilivyofeli kwa kiasi kikubwa nchini, michezo ni kati ya vitu au sekta zinazoongoza kwa kufeli.
Michezo imefeli kwa mambo mengi sana, viongozi wanaonekana wanapenda mafanikio na maendeleo yao na si yale ya michezo kwa jumla. Wachezaji wanaonekana hawako makini na hawajitambui. Hata serikali, nayo inaonekana imelala au haina habari kabisa na masuala ya michezo.
Serikali imekuwa ikishiriki lakini inaonekana kuichukulia michezo ni kama sehemu ya burudani tu tofauti na kwingineko duniani, michezo inatengeneza ajira kwa asilimia kubwa, inawafaidisha wananchi na inaisaidia serikali kuingiza kipato kupitia kodi.
Serikali ya awamu ya tano ina kasi ya aina yake, kwa upande wa michezo, tayari Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye naye ameanza mambo kwa kasi baada ya kuivunja ile kamati ya muda ya Stand United ambayo ilionyesha wazi ilikuwa imeundwa kwa ujanjaujanja kwa lengo la kuwafaidisha watu fulani hivi ambao waliingia kutaka uongozi, kwa kuwa tu wameona Stand United imepata udhamini wa bilioni mbili kutoka Wachimba Madini wa Acacia.
Nimefanya mahojiano na Waziri Nape kutaka kujua kama kasi yake hiyo itaendelea au ni nguvu ya soda.
SALEHJEMBE: Umeanza na kasi ukifumua ile kamati ya ujanjaujanja ya Stand, sasa ni suala la michezo kwa jumla?
Nape: La kwanza ni kuifanya michezo kuwa shughuli kubwa ya kiuchumi inayofaidisha pande zote kwa maana ya wanamichezo wenyewe pamoja na serikali pia. Mwanamichezo afaidike na jasho lake, serikali nayo iingize kodi.
SALEHJEMBE: Haufikiri kutaka kupata kodi kutoka michezoni bila ya kuisaidia kuimarika kuna tofauti na kumkamua maziwa ng’ombe asiye na chakula?
Nape:Nimesema tunataka michezo iwe shughuli rasmi ya kiuchumi badala ya burudani tu. Ili ufike huko, lazima uingie katika suala linaloitwa uwekezaji. Uwekezaji wenyewe lazima uwezo wa muda mfupi na muda mrefu pia.
SALEHJEMBE: Uwekezaji una miiko na mipaka yake, unafikiri kwa michezo tuliyonayo, inastahili kupokea uwekezaji?
Nape: Ili uvutie wawekezaji kutoka serikalini au kwa wadau binafsi, lazima ushughulike na vitu viwili vikubwa. Kwanza kushughulikia sheria zinazoongoza michezo ili wanaowekeza fedha zao ziwe salama pili ni kurudisha nidhamu katika michezo, hapa ni kwa wachezaji wenyewe na viongozi.
SALEHJEMBE: Nidhamu ya wachezaji, inaingiaje katika uwekezaji?
Nape: Lazima wawe ‘siriaz’ wakiona ni shughuli makini ya kiuchumi. Wakiwa hivyo watafanya vizuri na kufanya vizuri jambo ambalo litawavutia wawekezaji. Angalia miaka 1980, tulifanya vizuri sana kwa kuwa wachezaji wengi walitokea katika majeshi. Lakini leo ni rahisi kusikia wachezaji wanajihusisha hadi na madawa ya kulevya.
SALEHJEMBE: Hapa unawazungumzia wachezaji na nidhamu, vipi viongozi wao ambao ndiyo tatizo kubwa zaidi?
Nape: Hii ni sehemu ya pili ya nidhamu, hawa nidhamu yao haiko katika kiwango sahihi. Ndiyo maana ni rahisi kusikia migogoro, kusikia mambo ya rushwa, ulaji au ufujaji wa fedha. Hii inafanya wachezaji watumike tu na jasho lao linawafaidisha wengine.
SALEHJEMBE: Hili la jasho la wachezaji kufaidisha wezi au wazembe wengine ni pana. Viongozi wengi kama wewe wamesema tu, umejiandaa kweli vya kutosha?
Nape: Mimi haya nimekusudia kuyasimamia kwa nguvu zangu zote. Hata kama sitafikia asilimia mia, lakini kuhakikisha najenga msingi michezo kuwa shughuli rasmi ya kiuchumi na pia inasimamiwa na sheria na taratibu zinazofaa na michezo inakuwa na nidhamu.
SALEHJEMBE: Kuna nidhamu, uchumi, sheria. Sasa wewe umepanga uanze na lipi?
Nape: Aaah, vyama vinavyosimamia michezo hii, watuambie wanakwama wapi, sheria zipi zinawakwamisha, tuzishughulikie. Tuangalie uwezekano wa serikali kuvibana hivi vyama virudishe nidhamu, wakifanikiwa hata wachezaji wa michezo husika watajikuta wanalazimika kurudisha nidhamu.
SALEHJEMBE: Hauwezi ukaendeleza michezo bila kuwa na viwanja sahihi vya ngumi, soka, kikapu na michezo mingine. Utafanya nini?
Nape: Bahati mbaya hii ndiyo wizara yenye bajeti ndogo sana katika serikali. Ili uborejeshe miundombinu ya michezo, uwekezaji ndiyo jambo sahihi kama nilivyozungumza.
SALEHJEMBE: Kuna suala la kodi kwenye vifaa vya michezo, nalo linakwamisha ufanisi?
Nape: Kweli, ni suala la kuangalia uwezekano wa serikali kuingia makubaliano na mashirikisho mbalimbali duniani yanayoweza kusaidia na vifaa wanavyoleta vilipe kodi ndogo au iondolewe kabisa ili turahisishe upatikanaji wake na kuboresha miundombinu yetu.
SALEHJEMBE: Viongozi wa michezo, ni wauaji wakubwa wa michezo, wanaonekana ni untouchable (wasioguswa), wewe utawaweza kweli?
Nape: Kinachowafanya wawe untouchable ni sheria kuwa zisizo na makali, wanaachiwa wanatunga sheria zinazowalinda wao na si michezo na maendeleo yake. Mimi niseme katika kipindi ambacho nitakachokuwa waziri, viongozi wa michezo ambao wapo kwa ajili ya matumbo yao, nitashughulika nao.
Kwa kweli ni unyonyaji, unakuwa kiongozi wa michezo unayenyonya jasho la watu, unainyonya serikali na unajifaidisha binafsi. Hili nitashughulika nalo.
SALEHJEMBE: Serikali kama ya Rwanda, inasaidia timu au wanamichezo wanaoliwakilisha taifa katika michuano mbalimbali. Hapa zaidi serikali huwa inakabidhi bendera tu kwa hafla, utalibadili vipi hili?
Nape: Serikali ya awamu ya tatu imetuachia uwanja, awamu ya nne iliwekeza ikawalipa makocha. Sasa tunaendelea na mazungumzo kuwalipa makocha wazawa kama ilivyokuwa kwa makocha wageni lengo ni kuinua morali. Serikali ina nia ya kusaidia, tatizo kubwa ni uwezo.
SALEHJEMBE: Inawezekana uwezo ukapanda, naona Serikali ya Dk John Magufuli inapambana kuwabana wakwepa kodi?
Nape: Inawezekana, hakika ni juhudi kubwa zinazoweza kuisaidia serikali kuwa na uwezo zaidi. Wizara yangu inaweza kuishawishi serikali kuelekeza baadhi ya mapato katika michezo ikawa mwanzo mzuri wa kuisaidia.
SALEHJEMBE: Tunalia na maendeleo ya vijana, lakini hata wataalamu hatuna, serikali inashindwa vipi hata kuzungumza na nchi rafiki wanamichezo wakasome ili kuwa na wajuzi wengi?
Nape: Nimeanza mazungumzo na balozi wa China kama rafiki, lakini lengo ni hilo kufundisha makocha, lakini ningependa zaidi makocha vijana. Nitaendelea kuomba na kuzungumza na ubalozi mwingine kama Uturuki na zaidi ili kulifanikisha hilo.
SALEHJEMBE: Kuna Chuo cha Michezo cha Malya, kama kimekufa vile?
Nape: Hapana, tumeanza kukifanyia kazi na jambo la kwanza ni kuongeza utoaji kiwango cha juu cha elimu na si cheti tu.
SALEHJEMBE: Taasisi kumiliki timu, ilisaidia sana. Sasa nyingi zimejitokea, huoni hili ni la kulifanyia kazi pia?
Nape: Tumeanza mapema kabisa, ndiyo maana nilizungumzia nidhamu. Pia tutazishawishi taasisi kuanzisha timu. Angalia leo Azam FC haina mashabiki wengi lakini ina nafasi ya kufanikiwa kuzidi Simba na Yanga kwa kuwa uamuzi wake unakuwa ni wa watu wachache na si uliojaa siasa na lengo la kufaidisha matumbo ya watu fulani.
SALEHJEMBE: Vipi kuhusu michezo kama riadha, netiboli, kikapu na mingine?
Nape: Tutaweka nguvu, tunataka netiboli ile ya miaka ya 1980. Taasisi zikikubali kumiliki timu za michezo, itasaidia sana. Hata katika soka, huu ndiyo wakati wa kutengeneza akina Samatta (Mbwana) wapya.
Angalia leo akina Edibily Lunyamila, George Masatu hawasikiki tena. Itafikia siku, hata Samatta, hatasikika tena. Hivyo vizuri kutengeneza vijana wapya.
0 COMMENTS:
Post a Comment