KIIZA |
Hamisi Kiiza, Waganda waliamua kumbandika jina la Diego, wala hawakukosea na unaona anachokifanya sasa, “uu…unamjua, uuu…unamsikia!”
Kiiza, raia wa Uganda, tayari ameifungia Simba mabao 12 katika mechi 14 tu za Ligi Kuu Bara alizocheza.
Juzi aliiongoza Simba kushinda mabao 4-0 dhidi ya African Sports ya Tanga huku yeye akipachika mabao mawili na kufikisha 12 katika mechi 14, alizocheza wakati Simba imeshuka dimbani mara 16.
Kiiza alikosa mechi dhidi ya Mbeya City, Simba ikashinda kwa bao 1-0 mfungaji akiwa Juuko Murshid, akakosa pia dhidi ya Prisons, Simba ikalala kwa bao 1-0.
Bao lake la pili hiyo juzi ambalo lilikuwa ni la tatu kwa Simba, kwake lilikuwa ni bao lake la 42 kuanzia misimu mitatu na nusu iliyopita.
Kuanzia msimu wa 2011-12, Kiiza ana jumla ya mabao 42, kati ya hayo 30 amefunga akiwa Yanga na 12 akiwa Simba na huenda ataendelea kufunga zaidi kama atakuwepo uwanjani.
Kiiza ni “goal machine”, kwa kuwa kikosi cha Simba kina wachezaji wengi makinda, pia hakitengenezi nafasi nyingi zaidi za kufunga ukilinganisha na Yanga, lakini Kiiza amekuwa akitumia nafasi nyingi vizuri ukilinganisha na Amissi Tambwe mwenye mabao 13 sasa na Donald Ngoma mwenye 9.
Chini ya Kocha Jackson Mayanja, kikosi cha Simba kinaonekana kubadilika na kutengeneza nafasi nyingi na ikitokea kikaendelea kucheza kwa kasi hiyo, basi inaonyesha Kiiza hatakamatika.
Tambwe anaweza kuwa mshindani wake mkubwa, lakini bado anaweza kuangushwa na utumiaji mzuri wa nafasi.
0 COMMENTS:
Post a Comment