February 26, 2016



Na Saleh Ally
MARA nyingi sana nimezungumza kuhusiana na kati yetu, hasa mashabiki na viongozi wa mpira kutofurahia kuelezwa ukweli hata pale wanapokuwa wanakosea.

Nimeeleza mambo mengi sana, najua nimekuwa nikiwaudhi wengi sana. Kama kawaida sichoki na leo ni siku nzuri ya kukumbushana kuhusiana na uozo uliokuwa ukijitokeza ndani ya Coastal Union, jana wachezaji wamechoka.

Mchana kutwa wa jana, wachezaji wa Coastal Union walionekana mitandaoni wakiwa wamesambaza picha yao ya pamoja, wamepiga wakiwa wameshika bango lenye maneno: “Coastal, wachezaji tunataka pesa zetu zote za mishahara.”

Wachezaji wa Coastal Union wamechoka, taarifa zinasema wanadai mishahara ya miezi mitatu, posho zao rundo hawajalipwa. Wengi wao wakiwemo baadhi niliozungumza nao wanasema hata mazingira ya maisha yao ni duni kabisa.

Usisahau. Coastal ndiyo timu pekee iliyozifunga timu zinazoongoza Ligi Kuu Bara. Ilikuwa ya kwanza kuifunga Yanga kwa mabao 2-0 msimu huu, halafu ikarejea na kufanya hivyohivyo kwa kuitandika Azam FC kwa bao 1-0.

Vijana wanaonekana kuchoka, mioyo ya uvumilivu waliokuwa nao hadi wakaweza kuzifunga Yanga na Azam FC wakiwa hawajalipwa mishahara umekoma na sasa wanataka haki yao.

Nakumbuka, wakati nilikuwa nikikosoa mwenendo wa viongozi wa Coastal, wako waliokuwa hawajali au kuangalia hoja za msingi nilizokuwa nikiwaeleza na hasa suala la kukumbushia umoja, kuachana na kuwakataa wanachama wengine kwa hofu ya kupokwa madaraka na badala yake waangalie mafanikio ya klabu yao.

Niliwakumbusha kuhusiana na aliyekuwa mfadhili wao, Nassor Bin Slum, ambaye alijitolea mengi ikiwa ni pamoja na kutengeneza makazi bora ya wachezaji wa kikosi chake.

Wakamgeuka na maneno ya kwenye “kahawa”, ajabu jana, wachezaji wanamuomba arudi awakomboe kwa kuwa wamechoka.

Uliona wakati huo, viongozi wa Coastal walidhani wanaweza kujificha milele katika mwamvuli wa maovu. Sasa wanaumbuka, kwa kuwa walikataa ushirikiano na hawakutaka umoja. Leo wachezaji ndiyo wanawata Coastal wenye msaada, walioonekana wahujumu waende kuwaokoa. Hii nayo ni hujuma?

Huu ndiyo ukweli kabisa, Coastal inaendelea kudhalilika utafikiri si timu ya Wanatanga. Wengi wanaotaka kuisaidia wameingia woga, wasiopenda kelele wameamua kukaa kando akiwemo Bin Slum.

Nakumbuka msimu uliopita, walilazimika kumkaribisha awasaidia kuiokoa isiteremke daraja. Wakaungana na baada ya hapo, timu ikawa yao peke yao. Sasa wanahaha na kila kitu kimekuwa kigumu na hili ndiyo jibu la umoja ni nguvu.

Hii si mara ya kwanza viongozi wa Coastal kuonyesha hawana pumzi, kwani kila ligi inapofika mwishoni, wanaonyesha kushindwa na kuomba msaada kwa Wanatanga na Wanacoastal Union.

Mimi naona si sahihi, wamekuwa wakifanya mzaha au ujanja kwa makusudi kwa kuwasukuma wengine nje ya klabu kipindi ambacho fedha za udhamini zinaingia ndani.

Baada ya hapo, mwishoni kama sasa, hakuna fedha wanawakaribisha wengine ili waingie na kuisaidia timu isishuke. Ikiokoka, mwanzoni mwa msimu inakuwa yao peke yao hadi mwishoni wanapokuwa wameishiwa “pumzi” na mambo ni mabaya kabisa.

Huu ndiyo wakati wa maamuzi sahihi kwa Wanacoastal, vema kuwaambia viongozi waliopo hasa asilimia kubwa ya watu wazima wanaotaka mambo yaende kizamani, wakae kando na kuwakabidhi vijana wapambane.

Haiwezi kuwa Coastal Union inayopambana kuepuka kuteremka daraja kila mwishoni mwa msimu huku wahusika wakiona wako sahihi na kutetea mwendo wao wa hovyo kwa visingizo visivyo na tija.

Nilieleza Tanga inavyodhalilishwa na ubovu wa timu za Tanga ikiwemo African Sports lakini kwa upande wa Coastal kama ni jipu, tayari limeiva, kazi kwenu mnaopenda maendeleo ya dhati ni kulitumbua kwa mambo mawili tu.

Kwanza wapumzisheni wazee wenu, uongozi nao ukubali kushirikiana na vijana wenye mawazo mapya na si yale ya Coastal ya mwaka 1988. Mwisho nguvu yenu iwe umoja na malengo yenu yawe umoja. Aibu iko mbele yenu inakuja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic