Unakumbuka historia ya tiketi za elektoniki, mara zinaanza, mara zinazuiwa. Hii ilikuwa ni sehemu ya wajanja au wezi na wapigaji, hawakutaka ziendelee. Ila sasa, mambo yamebadilika.
Maana Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli imetangaza kurejesha haraka matumizi ya tiketi za elektroniki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kudhibiti mapato.
Uamuzi huo ulitangazwa jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alipofanya ziara katika kambi ya timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.
“Tunataka kuweka usimamizi mzuri wa mapato, katika hilo tunataka tiketi za elektroniki zitumike tena, ambazo tunaamini tutajua kiasi halisi cha mapato yatakayoingia kwa kila mechi.
“Awali tulikuwa tukifanya makato kwa makadirio ya watu wanaojaza uwanja mzima, kitu ambacho siyo kweli. Makato ya fedha yatakayopatikana yatazisaidia timu za taifa hasa Twiga Stars,” alisema Annastazia.
Katika hatua nyingine naibu huyo alisema serikali imeagiza viwanja vyote vya wazi vilivyovamiwa na wananchi, kuhakikisha vinarejeshwa.
“Tumeagiza halmashauri zote kuhakikisha viwanja vya wazi vilivyovamiwa vinarejeshwa na ujenzi wowote wa shule au makazi mapya ni lazima kuwepo na kiwanja cha michezo,” alisema Annastazia.
0 COMMENTS:
Post a Comment