February 1, 2016


Na Saleh Ally
HESABU pekee ndiyo huwa hazina ujanja, hazina kudanganya. Hilo naweza kulithibitisha kwa kukuonyesha hesabu za washambuliaji wawili wa Yanga na Simba.
Hamisi Kiiza wa Simba na Amissi Tambwe wa Yanga ambao unaweza kusema “wamebadilishana kiti”, mmoja anatoka upande mmoja kwenda mwingine, mwingine akachukue kiti cha mwenzake.

Wawili hao, Kiiza raia wa Uganda na Tambwe kutoka Burundi, wanafanana sana kiuchezaji, ni aina ya wachezaji ambao wanapoingia kwenye boksi, joto la hatari hupanda kwa nyuzi joto za juu zaidi kwa kuwa wakati wowote wanaweza kukudhuru.

Hadithi ya watu hawa wawili, kama haichekeshi basi itakukera lakini ukweli wake inaonyesha ndani ya mpira kuna matatizo kibao ambayo yanajificha kwa kuwa wahusika wakuu wanakuwa na uwezo wa kufanya hivyo kutumia kigezo cha “heshima”.

Kocha anapokosea, wachezaji wataficha tu, akikosea kiongozi hali kadhalika. Jasiri atakayesababisha kujulikana kwa madudu ya kocha au kiongozi, mara nyingi hutwikwa zigo la utovu wa nidhamu.

Hii yote inatokana na nguvu ya kocha au kiongozi, hivyo kuwafanya wachezaji kuwa wanyonge, wanaoonewa au kudhulumiwa huku wakilazimika kuwa kimya kwa ajili ya kutaka uhakika wa kulinda vibarua vyao.

Hesabu pekee ndiyo hazina heshima, hizi hazijali kiongozi wala kocha, zenyewe zinavyojipanga, majibu yake yanakuwa wazi kwa kila mmoja. Mfano mzuri ni kinachoendelea sasa, kwamba baada ya Yanga na Simba, kila moja kucheza mechi 16, wafungaji wanaoongoza katika timu zao ni Amissi (Tambwe) na Hamisi (Kiiza).


Kiiza ana mabao 12, ndiye kinara wa ufungaji wa Simba hadi sasa, Tambwe ana mabao 13, ndiye kinara wa Yanga na Ligi Kuu Bara hadi leo. Ndiyo maana wakanikumbusha hiyo hadithi ya kina Hamisi na Amissi dhidi ya makocha na viongozi.

Hawafai:
Wote hao wawili tuliwahi kuelezwa hawafai, tuliwahi kuelezwa kwamba wanaonekana uwezo wao umeporomoka na sasa, klabu zilichukua uamuzi wa kuwaacha! Yanga ilimuacha Kiiza, baadaye Simba nayo ikapitia reli ileile, ikamuacha Tambwe.

Wakati Yanga wanamuacha Kiiza, Kocha Mkuu, Marcio Maximo, aliamini kiwango chake cha ufungaji mabao kilikuwa kimeporomoka sana. Pamoja na kukumbushwa rekodi zake za nyuma, Mbrazil huyo hakutaka kusikiliza, nitakueleza kwa nini.
Tuanze na rekodi za Kiiza, msimu wa 2011-12 alikuwa na mabao 10, msimu wa 2012-13 akapiga mabao 8, 2013-14 akatupia mabao 12. Ndani ya misimu mitatu akiwa na Yanga kwenye Ligi Kuu Bara, tayari alikuwa na mabao 30.


Maximo hakuijali rekodi hiyo ya mabao 30 kwa misimu mitatu ukiwa ni wastani wa mabao 10 kila msimu. Akaamua kumuondoa ili kulinda “ugali” wa ‘mjomba’ wake, Denilson Jaja raia wa Brazil. Pia kutoa nafasi nzuri kwa mwenzake Andrey Coutinho, hasa ikifikia siku anataka kumchezesha namba 10.

Msimu mmoja baadaye, Simba wakaingia kwenye mkenge uleule. Viongozi wamekuwa wakijitetea katika hili kwamba si wahusika na badala yake Kocha Patrick Phiri aliwashawishi kufanya hilo.

Phiri, katika mahojiano na Championi, akashikilia msimamo kuwa kamwe asingeweza kumuacha mfungaji bora wa msimu mmoja uliopita. Tambwe ambaye alitua Simba akitokea Vital’O, msimu wa kwanza tu Msimbazi, licha ya kikosi kuwa kinasuasua, yeye akapiga bao 19 na kuwa mfungaji bora.

Msimu wa 2014-15, akatupiwa virago ndiyo akiwa amepiga bao moja, akavuka barabara ya Msimbazi na kutua mitaa ya Jangwani na Twiga. Akapiga mabao mengine 13, akafikisha 14 na kuwa nafasi ya pili kwa ufungaji nyuma ya Simon Msuva aliyefunga 17.


Reli moja:
Simba na Yanga ni kama mapacha waigizaji, upande mmoja ulimuacha Kiiza, mwingine Tambwe. Halafu upande mmoja ukamchukua Tambwe, mwingine Kiiza. Lakini ukweli aina ya wachezaji hao haina tofauti kubwa.

Yanga walikuwa wepesi kuona kosa la Simba kumuacha Tambwe, kwamba alikuwa mfungaji bora na mzoefu tayari wa Ligi Kuu Bara. Simba pia hivyohivyo, nao wakaona Yanga wamekosea kumtema Kiiza ambaye alijaribu kwenda Uarabuni, mambo hayakuwa mazuri wakamrudisha, nao pia walikuwa sahihi.

Lakini wakabaki kuwa katika kundi la kuchekesha pia, kwamba waliyemuacha na waliyemchukua hawakuwa na tofauti kubwa na utaona kilichofanyika katikati ya ukamilishaji ya haya mawili ni matumizi mabaya ya fedha, lakini matumizi mabaya ya nguvu ya madaraka na hili kila upande, hawapendi liguswe maana wanakuwa wakali kwelikweli wakiona kama wanaanikwa, hiyo ndiyo “nguvu ya uongozi”.

Maximo alichoangalia ni maslahi yake, yeye na wenzake wanawezaje kuingiza fedha na kuendeleza maisha na si manufaa ya Yanga. Lakini viongozi wa Simba pia waliangalia furaha ya nafsi na huenda sifa ya usajili na sijui kama ina maslahi yake ndani. Maana walimtoa mfungaji bora wa Tanzania Bara, halafu wakaona mfungaji bora wa Kenya, Dan Sserunkuma ndiye anafaa kufanya vema Ligi Kuu Bara, ikawa kichekesho.

Ukianzia mwaka 2011-12, ni misimu minne na nusu ukijumlisha na huu wa 2015-16 ambao uko katikati. Kila mmoja, Tambwe na Kiiza wamecheza misimu mitatu na nusu.

Tambwe hakuwa amefika msimu wa 2011-12, Kiiza akafunga mabao 10 akiwa na Yanga. Kiiza akaukosa 2014-15 baada ya kutemwa na Maximo, Tambwe akatupia mabao 14.


Hesabu za mwisho zinaonyesha kwa kipindi chote hicho kuanzia 2011-12, Kiiza hadi sasa ana jumla ya mabao 42, huku Tambwe akiwa na 46. Hapa utaona namna nguvu ya hesabu inavyoweza kuzidi nguvu za “uongozi” na “makocha”.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic