February 27, 2016


Na Saleh Ally
KUNA vita ya kukata na shoka kati ya washambuliaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unajua kwamba Hamis Kiiza wa Simba na Amissi Tambwe wa Yanga wanafukuzana kwa karibu sana!


Kiiza ana mabao 16 akifuatiwa na Tambwe mwenye 15 na hakuna kati yao mwenye uhakika kwa kuwa kiuchezaji, kila mmoja ana uwezo wa kufunga mabao mawili hadi matatu katika mechi moja tu.


Bado pia kuna hofu kati yao kwa kuwa nyuma yao wapo Jeremiah Juma wa Prisons mwenye mabao 11 kama ilivyo kwa Donald Ngoma wa Yanga. Elias Maguri amekwama na mabao 10, huenda akaamka lakini Kipre Tchetche wa Azam FC ana tisa na Ibrahim Ajib wa Simba ana nane. Hawa wote si wa kuwadharau.


Si unajua mechi zilizobaki. Yanga na Azam FC kila moja imebakiza mechi 11 na ndiyo zinazoshika nafasi ya kwanza na ya pili katika Ligi Kuu Bara. Kila moja ikiwa na pointi 46, tofauti ni mabao ya kufunga na kufungwa.


Simba wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 45 wamebakiza mechi 10 mkononi. Bado hakuna anayeweza kuwabeza kwa sasa, kwani kufungwa mabao 2-0 na Yanga wiki iliyopita, hakuwaondoi kwenye kundi la wanaowania ubingwa.


Kwa hesabu ya mechi 10 hadi 11 zilizobaki kwa timu hizo tatu, sasa inaonekana ligi imejigawa rasmi na kundi la timu zinazowania ubingwa ni hizo tatu tu.


Ukiangalia kutoka katika nafasi ya tatu kati ya Simba yenye pointi 45 na inayoshika nafasi ya nne, Mtibwa Sugar yenye pointi 33, unaona nafasi ya ubingwa ni asilimia 15 kwa timu zinazoanzia nafasi ya nne hadi ya sita na asilimia tatu kwa zinazoanzia nafasi ya saba ya msimamo hadi nane huku ikiwa ni asilimia ziro kwa zilizobaki.


Yanga, Azam FC na Simba zinarudi kwenye vita ya miaka minne mfululizo ambayo imekuwa ni miaka yenye neema zaidi kwa Yanga na Azam FC na Simba imekuwa ikiambulia nafasi ya tatu hadi ya nne wakati mwingine.


Mechi tano zijazo za timu hizo zinaonyesha zitakuwa na uamuzi wa sita au tano zilizobaki zimaliziwe vipi. Yanga na Azam FC watakutana ndani ya mechi hizo na huenda kama mmoja wao atapoteza, atakuwa ameipa nafasi Simba kupanda katika nafasi ya pili kama itashinda.


Mechi hizo tano ni dakika 450 kwa kila timu na itatakiwa kukaa mguu sawa kweli kuhakikisha hakuna hadithi zaidi ya kazi tu.
 


Yanga SC:
Mechi tano za Yanga ni dhidi ya Azam FC, African Sports, Toto Africans, Mtibwa Sugar na Mwadui FC. Katika mechi hizo tatu zitakuwa za nyumbani Dar es Salaam, mbili za ugenini lakini hiyo moja dhidi ya Azam itachezwa Uwanja wa Taifa na kwa Jangwani wataona kama wako nyumbani.


Iwapo Yanga itafanikiwa kukusanya pointi zote 15 kwa kushinda zote, itakuwa imefikisha pointi 61 na itakuwa imeipokonya Azam pointi tatu na kuisukuma mbali. Kama itakosea hesabu, basi itatoa mwanya kwa Azam FC kupanda juu.
Yanga tayari inajua uchungu wa kipigo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Coastal Union. Hivyo bado haiwezi kudharau mechi za timu kama Toto na Africans Sports na ubaya kwake, itacheza na Toto ugenini.


Bado Yanga haijui utamu wa kipigo kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu. Lakini inatakiwa 'kukaza' kwa kuwa African Sports na Toto nazo zinapigania 'roho' zao kubaki ligi kuu. Mara nyingi timu hizo ni hatari kweli.

Azam FC:
Kwa mwendo uliozoeleka wa Azam FC inaonekana kama imepoteza radha yake. Huenda ni uchovu wa michuano kule Zambia ilipoalikwa. Lakini bado ina nafasi kubwa kabisa ya ubingwa licha ya kwamba ilikutana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Coastal Union na kusuluhu na Prisons.


Mechi zake tano zijazo ni kati ya Yanga, Mtibwa Sugar, Ndanda, Stand United na Ruvu Shooting. Hakika ni mechi ngumu zilizopangana na Azam FC lazima iwe makini.


Hofu ni kwamba Azam FC inaweza isiende kwa mpangilio sahihi wa mechi zinavyoonyesha kwa kuwa TFF ni wazee wa kupangua ratiba hovyo na hasa kwa Azam FC, kwani mechi zake nyingi zitapangiwa tarehe.


Lakini kama mechi zingeenda kama ratiba inavyoonyesha, kungekuwa na ugumu wa juu kabisa kwa Azam FC kwa kuwa inakutana na timu ngumu mfululizo ikianza na Yanga, inafuatia Mtibwa Sugar, Ndanda, Stand United halafu angalau kwa JKT Ruvu.


Ligi haina mwenyewe kwa maana ya ugumu, lakini kuna timu zinazojulikana kwamba ziko vizuri kabisa. Hivyo Azam FC nao lazima wazicheze mechi zao tano kwa uhakika bila ya kupoteza.


Nao pia hawajafungwa kwenye Uwanja wa Taifa, lakini wanajua utamu wa kipigo ugenini. Katika mechi hizo tano watakuwa na mechi mbili za ugenini dhidi ya Mtibwa na Ndanda ambazo umakini inabidi uwe maradufu, la sivyo watakutana na kipigo cha pili na kupoteza mwelekeo.
 


Simba:
Ukiangalia haraka hasa baada ya kipigo cha Yanga, unaweza kuona kama wamepoteza mwelekeo. Lakini kwa uhalisia bado kabisa. Wao wameshafungwa mara tatu lakini wako katika nafasi ya tatu.


Kinachoweza kuwaathiri zaidi na huenda wakajitoa kabisa katika mbio za ubingwa ni kama watakubali tena kipigo yaani idadi ifikie vipigo vinne. Tayari wamefungwa mara mbili, wamefungwa Uwanja wa Taifa dhidi ya Yanga na mara moja dhidi ya Prisons pale Sokoine, Mbeya.
Simba wanajua uchungu wa vipigo nyumbani na ugenini. 


Huenda wanaweza kuwa makini zaidi kuepusha kipigo kingine huku wakiwaombea njaa Yanga na Azam FC ambao ndiyo wapinzani wao pekee waliobaki.

Mechi zao tano zijazo ni dhidi ya Mbeya City, Ndanda FC, Prisons, Coastal na Majimaji. Utaona karibu zote ni mechi ngumu zinazojumuisha moja ya wababe wao Prisons.


Mbeya City inakutana nao ikiwa imejeruhiwa kwa kuchapwa mabao 3-0 na Azam FC lakini wana kocha mpya, Kinnah Phiri na wana wachezaji wazoefu kama Haruna Moshi 'Boban', Ramadhani Chombo 'Redondo' na wanacheza kwenye Uwanja wa Taifa ambao wameuzoea na unakuwa bora kwa kila timu.


Ndanda pia ni wagumu, Prisons itakuwa ni mechi ya kisasi na kusaka pointi, Coastal Union watakuwa kwao, hawa ni kiboko ya vigogo hadi sasa na Majimaji nao watakuwa wanapigania 'roho' yao kubaki Ligi Kuu Bara.


Utaona kwa maana ya rekodi na mwenendo, ni mechi ngumu kwa Simba ambazo zitakuwa za kuamua, ibaki kwenye mbio za ubingwa au iondoke rasmi kama itazicheza vibaya.


Kama itashinda zote na kufikisha pointi 55, basi itakuwa na nafasi nzuri ya kucheza vizuri mechi tano zilizobaki na uhakika wa kubaki kwenye mbio za ubingwa ingawa si kazi rahisi.


Mechi muhimu zaidi kwa Simba, itakuwa ni dhidi ya Mbeya City. Watakaposhinda, watarudisha imani tena na morali upya kwa kikosi chake ambacho kilishinda mechi sita mfululizo kabla ya kukutana na kigingi cha Yanga na kuchapwa bao 2-0.


Mechi hizo tano zinaweza kuwa mabadiliko makubwa au majibu sahihi ya wanaowania ubingwa kuendelea kubaki watatu au wawili baada ya mmoja kudondoka.


Lakini kama timu hizo tatu zitamaliza mechi tano zijazo zikaendelea kuwa na tofauti ya pointi moja au mbili kimsimamo, huenda itakuwa ligi ngumu zaidi mwishoni kwa kipindi cha misimu mitano iliyopita.

YANGA
Machi 5, 2016

Azam             Vs        Yanga             Taifa           
Machi 9, 2016
Yanga             Vs        Sports            Taifa
Machi 12, 2016
Toto             Vs        Yanga              Kirumba
Machi 16, 2016
Yanga            vs        Mtibwa            Taifa
Machi 19, 2016
Yanga            Vs        Mwadui         Taifa

AZAM:
Machi 5, 2016

Azam             Vs        Yanga             Taifa
Machi 9, 2016
Mtibwa         Vs        Azam             Manungu
Machi 12, 2016
Azam             Vs        Ndanda         Azam Complex
Machi 16, 2016
Azam             Vs        Stand             Azam Complex
Machi 19, 2016
Azam             Vs        JKT Ruvu        Azam Complex
      

SIMBA
Machi 6, 2016

Simba             Vs        Mbeya             Taifa                   
Machi 10, 2016
Simba             Vs        Ndanda         Taifa
Machi 13, 2016
Simba             Vs        Prisons            Taifa
Machi 19, 2016
Coastal            Vs        Simba             Mkwakwani
Aprili 2, 2016
Majimaji        Vs        Simba             Majimaji

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic