Moja ya sifa kubwa za kikosi cha Cercle de Joachim kinachocheza na Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali nje ya eneo la hatari la adui.
Takwimu mbalimbali na video za michezo ya timu hiyo, ukiwemo ule wa awali dhidi ya Yanga waliolala kwa bao 1-0, zinaonyesha Cercle de Joachim wapo vizuri kwa mashuti tena yale ya ‘kuagizia’ kutoka mbali.
Licha ya kufungwa katika mchezo wa kwanza nchini Mauritius, timu hiyo ilionyesha umahiri mkubwa wa kupiga mashuti ya mbali wakilenga lango la Yanga, hivyo wapinzani wao wamepanga kuzuia hali hiyo.
Katika mazoezi ya jana asubuhi ya Yanga, kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm, alionekana akitumia muda mwingi kuelekeza wachezaji kukaba, kuzuia adui asipate nafasi ya kupiga shuti langoni kwa adui.
Wakati huohuo, Kocha wa Cerce de Joachim, Abdel Ben Kacem, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, timu yake inacheza mechi ya leo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi ya Kombe la FA nchini kwao.
“Tumeshinda mechi ya FA Jumatano wiki hii, ushindi huo umetupa morali ya kushinda mechi hii, tumekuja Tanzania kupambana hatukuja kutalii, hivyo Yanga wajiandae,” alisema Kacem.
0 COMMENTS:
Post a Comment