Simba iko kamilini na imepanga kuimaliza Singida United katika mchezo wa Kombe la FA kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja ambaye katika mechi ya mwisho kikosi chake kilipoteza dhidi ya Yanga kwa mabao 2-0, amesema katika mechi hiyo hatafanya masihara na atahakikisha anatumia silaha zake zote ili kupata ushindi.
“Sitaki aibu kwani wapinzani wetu ndiyo kwanza wamepanda daraja kutoka daraja la pili hadi la kwanza, tukifanya mchezo wanaweza kutufunga, sitaki itokee hali hiyo.
“Tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi hiyo na hatutaki masihara kabisa kwa sababu Kombe la FA lina umuhimu mkubwa sana kwetu kwani tunataka kucheza michuano ya kimataifa,” alisema Mayanja.
Kwa upande wake Kocha wa Singida United, Frugence Novatus, alisema: “Mechi hiyo ni ngumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ambayo yatatuwezesha kusonga mbele.”
Mechi nyingine za Kombe la FA kesho ni kati ya Panone ya Kilimanjaro na Azam FC ya Dar kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi wakati Toto Africans itacheza na Geita Gold kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment