February 26, 2016


Na Saleh Ally
KATI ya jambo linalotuangusha huenda kuliko lolote, ni suala la watu kutokuwa tayari kuelezana ukweli pale kunapokuwa kuna kosa.

Wengi hawataki kukosolewa kwa kigezo cha wanasakamwa, wanaonewa au hawapendwi lakini hakika wanajua kuwa wanachokosolewa ni kosa au tatizo.

Mimi nilishaamua kuendelea, kusema ninachoona si sahihi na sahihi bila ya kujali nani atanuna au kuacha kunisemesha. Leo ninaangukia huku, wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara na hasa wale wa vikosi vya Yanga na Simba.

Najua watu wengi wanalilia mabadiliko kwa klabu zetu hizo, wanataka kuziona zinapiga hatua kwa kuwa ni kubwa na zina mtaji wa watu. Mara nyingi tumelia na viongozi.

 Hata tukikataa vipi, Simba na Yanga zinauliwa na mazoea na siasa zisizo na tija. Zinaendelea kubaki kutembea katika reli ya historia zikiamini sasa ni mwaka 1975! Wachezaji nao ni hovyo ndiyo maana wengi wameshindwa kucheza Ulaya kwa kuwa ndani ya akili zao ni watu waliopitwa na wakati lakini wenye mwonekano wa sasa.

Kwa wachezaji walio Yanga na Simba, kwa sasa, inakuwa ni vigumu kucheza Ulaya kwa kuwa mambo yako kimpangilio na yanafuata utaratibu sahihi ambao ndiyo uendeshaji wa kisasa wa mchezo wetu wa soka.


Inapofikia mechi ya watani, Yanga na Simba zinakutana. Unakuwa ni wakati mwafaka wa kujua kiasi wachezaji wanaocheza katika timu hizo wana mawazo ya kijinga pia ni watu ambao kamwe hawawezi kusonga mbele au wao ni tatizo la maendeleo ya soka hapa nchini.

Kwanza wachezaji wanachungwa kweli eti watahongwa.  Hivi unaajiri mtu, halafu unaanza kumchunga, wa nini? Utendaji bora lazima uaminiane. Arsenal wana mechi na Barcelona, eti usikie wanamlinda Olivier Giroud au Theo Walcott! Ni jambo ambalo haliwezekani hata kidogo.


Unaweza kuwalaumu viongozi, lakini nao wana hofu ya kutowachunga kwa kuwa wanawajua ni watu wa kuchungwa.

Nakumbuka wakati fulani, kuna kiongozi mmoja wa Simba aliwahi kuhisi mchezaji wake amehongwa licha ya kwamba tayari kuna ahadi ilitolewa ya mamilioni kwa wachezaji wote wakiifunga Yanga.

 Mapumziko, alimtumia mchezaji huyo ujumbe, kwamba akirudi uwanjani kipindi cha pili, afunge naye atampa Sh milioni tatu. Kweli mchezaji huyo alifanya hivyo, akafunga bao bora kabisa, yule kiongozi Sh milioni 3 ikamtoka. Maana ahadi ni deni.

Huu ndiyo mfano ningependa kuanzia, angalia mchezaji anayelipwa mshahara, aliyesajiliwa kwa fedha nyingi, leo hadi aahidiwe fedha ndiyo aifanye kazi yake kwa juhudi. Kwa nini analipwa mshahara, analipiwa nyumba? Au kwa nini alilipwa wakati wa kusajiliwa?

Siku zinabadilika, hapa Tanzania, wanasoka ni kati ya wafanyakazi wanaolipwa mishahara na marupurupu bora kabisa kwa asilimia kubwa, lakini ili aifanye kazi yake vizuri, lazima kiongozi atoe fedha ya ziada!

Miaka kama sita au saba imepita, kiongozi mmoja alilazimika kukopa ili kuongeza fedha za ziada kwa mchezaji afanye vizuri. Mwisho wakaishia kwenye ugomvi mkubwa akimtuhumu alipokea fedha zake, pia akahongwa na timu pinzani, halafu wakafungwa.

Bado hapo, wakati mwingine wachezaji wanapewa fedha asilimia hadi 60 za mapato ya mlangoni. Kwa timu kama Yanga na Simba ambazo bado kwa asilimia kubwa zinategemea fedha kutoka mifuko ya watu binafsi, si sahihi hata kidogo.

SIMBA

Wachezaji wanapaswa kuwa ni wale wanaojitambua. Makubaliano ya kimkataba, mshahara na marupurupu. Baada ya hapo ni kufanya kazi tu na si kuanzisha visingizio ili walipwe zaidi.

Hawa wakitoka nje ya Tanzania kila kitu kinakuwa kigumu. Kule watu wanajitambua, kila mmoja baada ya malipo yanayotokana na mkataba, basi anajituma zaidi kuisaidia timu yake ifanikiwa. Hali kadhalika yeye kuonekana apate soko.

Mfumo wa hapa nyumbani unawafanya wachezaji waone kila sehemu ni kugumu. Lazima wawe na mfumo bora unaotumika sehemu nyingi duniani.

YANGA

Mchezaji aliyenunuliwa, sasa analipwa mshahara mkubwa. Halafu ili aifunge timu pinzani, lazima umnunue. Ni kitu kibaya kabisa kinachoubakiza mchezo wa soka Tanzania matopeni, vigumu kuukwamua.

Motisha ni jambo jema, lakini viongozi waondoe hofu, wachezaji nao wajitambue. Wasiwe watumwa wa fedha, badala yake waangalie mafanikio ya timu wanazozichezea pia wao binafsi.

Pamoja na uwezo wa kimwili na vipaji wanavyopewa. Ili wafanikiwe, vichwa navyo lazima vifanye kazi kwa kuweka malengo sahihi. Ukiwa mtu mzima unayechungwa wewe ni tatizo, kama ili utekeleze kazi yako, lazima ulipwe ziada, wewe ni tatizo na ndiyo maana nasema soka nchi hii lina mambo mengi yasiyo na tija kama hilo, hakika ni ujinga kabisa!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic