March 30, 2016


Uongozi wa Azam umepambanua kuwa macho na akili yao kwa sasa ipo kwenye mchezo dhidi ya Waarabu wa Esperance ya Tunisia huku wakizichukulia mechi mbili kabla ya mtanange huo kama mazoezi.

Licha ya kuwa na kibarua kikubwa kesho Alhamisi dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA utakaopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi, lakini matajiri hao wa Bongo wamesema wanataka kuutumia kama chambo ya kukiimarisha kikosi kuelekea mchezo na Esperance.

Msemaji wa Azam, Jaffar Idd, amesema kama ni maandalizi dhidi ya Waarabu hao yalianza tangu wiki iliyopita ambapo wamekuwa kambini kabla ya kujazwa upepo na wale waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa.

Azam itawakaribisha Esperance Aprili 10, katika mchezo wa raundi ya 16 ya Kombe la Shirikisho Afrika, kabla ya kurejeana wiki moja baadaye huko Tunis, Tunisia.

“Maandalizi yanakwenda vizuri, tumekuwa kambini tangu wiki iliyopita, wale waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa wamesharejea na tayari wameanza mazoezi na wenzao,” alisema Idd na kuongeza:


“Unajua tuna mechi mbili, keshokutwa (kesho Alhamisi) na Aprili 3 (dhidi ya Toto Africans, mechi ya ligi kuu), kwetu zote tutazitumia kama sehemu ya mazoezi ya kujiandaa na mchezo na Esperance.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV