March 28, 2016


NI mwendo wa kimyakimya, ndiyo kauli unayoweza kuisema kufuatia Klabu ya Azam FC kutamka kuwa wamekuwa wakiwachunguza wapinzani wao Esperance kwa ukaribu ili kuweza kutambua mbinu zao mbalimbali ambazo zitawarahisishia pale watakapokutana nao kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho.

Kikosi hicho cha Azam kinachonolewa na Muingereza, Stewart Hall, kitavaana na Esperance katika mchezo wa kusaka nafasi ya kutinga makundi ya michuano hiyo ambapo mechi yao ya kwanza itapigwa katika Uwanja wa Chamazi Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar Aprili 10, mwaka huu.

Msemaji wa kikosi hicho, Jaffar Idd, amesema wamekuwa wakiwafuatilia kwa ukaribu wapinzani wao kwa ajili ya kutaka kupata mbinu zao za kiuchezaji pamoja na wachezaji wao hatari kwa ajili ya kumpatia kocha wao, Stewart ili kuanza kuwaundia mipango ya kuwadhibiti.

“Siyo kwamba hatuna habari na mchezo wetu dhidi ya Esperance wa Kombe la Shirikisho Afrika, bali tunafanya mambo yetu kwa ukimya ambapo tunawafanyia uchunguzi kwa ajili ya kukitambua vyema kikosi hicho.

“Tumekuwa tukifuatilia vitu vingi kuhusu wao ambapo miongoni mwao ni kutaka kufahamu aina ya mbinu wanazotumia pamoja na aina ya uchezaji lakini pia tunafuatilia wachezaji wao hatari ambapo tukikamilisha suala hilo, tutakuwa tunajua jinsi ya kucheza nao,” alisema Idd.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV