March 28, 2016YANGA na Azam FC ambazo zinaiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa, zimepiga hatua nzuri ambayo Watanzania wanaweza kujivunia.

Yanga ambao wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wamefanikiwa kuzing’oa timu kutoka Mauritius na Rwanda. Ingawa katika mechi dhidi ya APR, hakika kulikuwa na walakini mkubwa na Yanga ikapita kwa jasho kwelikweli.

Kwa upande wa Azam FC nao walifanya kazi nzuri baada ya kuanza na Bidvest ya Afrika Kusini. Ingawa timu hiyo iliamua kutumia kikosi cha vijana, mchanganyiko na wakongwe kidogo, lakini haiwezi kuzuia rekodi kuandikwa kwamba kwenye Kombe la Shirikisho, imeng’olewa na timu kutoka Tanzania.

Hiki ni kitu cha kujivunia, ingawa tunachopaswa kukumbuka ni kwamba kila unapopiga hatua ni lazima unakutana na ugumu zaidi na hapo ndiyo kipimo sahihi kuhusiana na uwezo wako au hatua ya kimaendeleo uliyopiga.

Baada ya Yanga na Azam FC kuzitoa timu za Rwanda na Afrika Kusini, sasa ramani ya michezo inawahamishia Afrika Kaskazini ambako hakuna ubishi ndiyo ubora wa juu kabisa wa soka la Afrika uko huko.

Yanga inakutana na Al Ahly ya Misri wakati Azam FC inakutana na Esperance ya Tunisia, timu ambayo mwaka 2009, iliing’oa Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuichapa kwa mabao 3-0 jijini Tunis.

Hizi ni timu kutoka katika nchi za Kiarabu, nchi ambazo zimepiga hatua kubwa sana. Kwa kifupi, hakuna tofauti kubwa sana ya kimaendeleo kwao na Ulaya kama utazungumzia mchezaji mmojammoja au kiwango cha uwekezaji.

Pamoja na ubora wa Azam FC kiuwekezaji, utagundua Esperance ni timu kongwe, yenye mafanikio makubwa na iliyowekeza zaidi kuliko Azam. Hali kadhalika, Al Ahly, pia ni kubwa na yenye mafanikio ya juu kabisa.

Kweli katika mchezo wa soka tuna ule msemo wetu, “mpira unadunda”. Mimi ninaamini hauwezi kudunda vizuri bila ya kuwa na upepo wa kutosha, huenda sasa ndiyo wakati mzuri wa kujaza.

Yanga na Azam FC, lazima wawe na plani sahihi kwa kuwa Waarabu maandalizi yao huwa na umakini wa juu kabisa. Ni lazima kujipanga tofauti kama inafikia wakati wa kukutana nao.

Naliona tatizo moja, watu hawataki kuelezana ukweli, hawataki kuambiwa ukweli na wengine wanataka kuificha hofu iliyo wazi kwa kutumia viganja vyao huku wakiwa wamesahau, kiganja hakifuniki kwa kuwa kina mianya mingi.

Hofu ya Waarabu au hadhari ya Waarabu ni kubwa kuliko viganja vyetu. Kwanza kabisa lazima tukubali tunakutana na timu bora, zenye uwezo uwanjani, zenye wachezaji bora, zinazojua fitna na ikiwezekana Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lingependa kuziona zenyewe zinasonga mbele zaidi ya timu za Tanzania.

Ili kufanikiwa dhidi yao, lazima kuwe na maandalizi ya kutosha ambayo yana dira tofauti kabisa ukilinganisha na yale maandalizi dhidi ya Cercle de Joachim, APR au Bidvest iliyoleta vijana wake kupambana na Azam FC.

Tukikubali kwanza tunaokutana nao ni imara kama ambavyo Yanga ilifanya mara ya mwisho dhidi ya Al Ahly, basi kutakuwa na majibu bora mwishoni mwa mechi hizi. Kama tusipofanya hivyo, basi wawakilishi hao wa Tanzania, huo ndiyo utakuwa mwisho wake.

Maandalizi makubwa ni lazima, nafasi ya kutosha pia inatakiwa na Yanga na Azam FC, huenda huu ndiyo wakati wa kuonyesha uzalendo kwao lakini nao wakubali wapo kwa ajili ya taifa kwa kuwa Waarabu hawataziacha timu hizo za Tanzania zipite kirahisi.

Nawatakia sikukuu njema wadau wote wa michezo na burudani ambao ni wasomaji wa SALEHJEMBE.1 COMMENTS:

  1. Hukusema ni nini kifanyike, nafikiri huu ujumbe wako ulitakiwa uwe specific kwa Bodi ya league na TFF ambao wanaonyesha dhamira ya wazi kuvihujumu vilabu hivi! Unawapa siku saba Azam kujiandaa kwa ajili ya club amvayo waliifunga gori 3, Yanga kwa ajili ya APR then unawapa siku 2 za kujiandaa kwa ajili ya waarabu!!? This is st.... n crazy!!

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV