March 16, 2016



MANARA

Na Saleh Ally
HIVI karibuni kumekuwa na gumzo kubwa kuhusiana na wakuu wawili wa vitengo vya habari vya klabu kongwe nchini, Yanga na Simba.

Haji Manara ambaye pia ni msemaji wa Simba kama ilivyo kwa Jerry Muro upande wa Yanga, mara kadhaa wameingia katika malumbano.

Huenda ni utani au vinginevyo lakini kila mmoja amekuwa akiangalia anachoamini sana. Muro ambaye amekuwa akitoa majina kadhaa kwa Simba au anachokizungumzia, amefanikiwa kulikuza neno la “Wamchangani”, akimaanisha Simba haishiriki michuano ya kimataifa.

Inaonekana wanaopanda ndege ni Yanga na Azam FC pekee kwa kuwa wanashiriki michuano ya kimataifa. Simba wanaendelea kukomaa na basi lao “mkoa kwa mkoa”.
 Pamoja na kuonekana hapendi kuzungumza, Championi Jumatano lilimpata Manara na kumshawishi kulizungumzia hilo.

SALEHJEMBE: Haji kabla hatujasonga mbele, kipi hasa kinakufanya uwe mgumu kujibu mashambulizi ya msemaji wa Yanga anapoangusha ‘mabomu’ Simba?
Manara: Mimi hupenda kuzungumzia ‘issues’ siyo porojo. Haiwezekani nikawa kiongozi kisha nikazungumzia lugha za kishabiki.


SALEHJEMBE: Lakini mashabiki wa Simba wangependa kuona kuna majibu kutoka kwako!
Manara: Mashabiki na wapenzi wa Simba wataniwia radhi kwa kutokuwa muimba ngonjera za uchochoroni. Nibaki msemaji wa klabu kubwa nchini. Nikizungumza ujue ni masuala ya msingi.

SALEHJEMBE: Wewe ni msemaji wa klabu Haji, vipi inakuwa kama muoga, hujiamini?
Manara: Nisijiamini kwa sababu ya mtu? Katika hili, jibu langu ni jepesi tu, lazima tujitofautishe msemaji wa klabu na mropokaji wa klabu.

SALEHJEMBE:Ukisema hivyo unamaanisha nani ni mropokaji wa klabu?
Manara: Hata mimi sijui.


SALEHJEMBE: Mengi hupendi kuyajibu, lakini hata hili la Simba wa mchangani, umekaa kimya kwa kuwa kweli ni sahihi au siyo ishu?
Manara: Kama wanaozungumza hawajui, nitafanyaje?

SALEHJEMBE: Ni kweli Simba inacheza michuano ya nyumbani tu, si kimataifa?
Manara: Sawa, hiyo haitoshi kuiondoa Simba au kufuta mafanikio yake yote. Simba ndiyo timu kutoka Tanzania inayojulikana zaidi kimataifa barani Afrika.

SALEHJEMBE:Angalia  nawe usije kuwa mropokaji wa klabu, hasa kama huna uhakika!
Manara: Ukifika katika hoja, hapo ndipo anga zangu. Nitafafanua ili watafute neno jipya la kuitukana Simba.

SALEHJEMBE:Unaweza kuzitoa, lakini ukubali kipindi hiki kupanda ndege ni nadra kwa Simba.
Manara: Suala la ndege haliwezi kuwa ishu kwa Simba. Maana ndiyo timu ya kwanza nchini kupanda ndege mwaka 1963 wakati huo ikiwa ni Tanganyika. Simba ilialikwa na Rais wa Ethiopia wakati huo, Haile Selassie.


SALEHJEMBE: Yote yamepita, hiyo ni zamani sana!
Manara: Kamwe huwezi kulifuta hilo, Simba kuwa ya kwanza kupanda ndege na wanaoshabikia sasa ndege hawajui lolote. Huwezi kufuta Simba ndiyo timu ya kwanza kuanza kuvaa jezi mwaka 1938, ilicheza na kombaini ya mabaharia wa meli za wageni zilizosimama Dar es Salaam.

SALEHJEMBE: Una uhakika timu nyingine hazikuwa na jezi?
Manara: Kabisa, wenzetu hadi wakabandikwa jina la “Gongo Wazi”, kisa ni kucheza bila jezi. Pia Simba ni ya kwanza kuvaa viatu mwaka 1949. Ilicheza na timu ya Jeshi la Maji la Afrika Kusini.
Kuna mengi sana ndugu yangu, Simba ilianza karibu katika kila kitu. Hata kumiliki usafiri kama basi, Simba ndiyo ilianza 1968.

SALEHJEMBE: Lakini haya ukiangalia wala hayaingiliani na suala la kimataifa na mchangani, sivyo?
Manara: Simba ndiyo bingwa wa kwanza kabisa nchini wa soka mwaka 1966, mwaka uliofuata yaani 1967 wakaiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa. Sasa nani hapa ni wa kimataifa? Kukosa misimu mitatu ndiyo tufute hata hili?

SALEHJEMBE:Niliandika kuhusu suti mkaja juu kweli!
Manara: Unajua Simba ndiyo klabu ya kwanza kwenda Ulaya, mwaka 1974 timu ilienda Poland na tukavaa suti.

SALEHJEMBE:Najua hata mlipokwenda Algeria mlivaa suti, sasa ziko wapi na sasa wote hamvai hadi Azam FC ndiyo wamerekebisha na hauoni kwa kizazi cha sasa mtaonekana mmewafuata wao?
Manara: Simba ingekuwa inashiriki michuano ya kimataifa, basi ungeona tunavyofanya kimataifa. Sijui wengine hao wanaosafiri bila kuwa na mpangilio, ugeni wa jambo pia ni tatizo.

SALEHJEMBE: Unaposema ugeni, unamaanisha Yanga waliosafiri kwenda Mauritius na Rwanda bila ya suti?
Manara: Sijaitaja timu yoyote, wewe ndiye umesema.

SALEHJEMBE: Rekodi za Simba, nyingi zinaonekana bora zamani, huoni nalo ni tatizo?
Manara: Wewe ndiye unaona hivyo, lakini angalia bado rekodi za Real Madrid kuchukua ubingwa mara nyingi zaidi Ulaya zinabaki, za miaka ya nyuma sana wanajumlisha na sasa.

Ndiyo maana sasa tunasema Simba ni mabingwa wa kihistoria Afrika Mashariki, wa kwanza kuwa bingwa na wamechukua makombe mengi zaidi. Lakini ndiyo timu pekee kufika hatua ya nusu fainali klabu bingwa, hiyo ni mwaka 1974. Hata Fainali ya Kombe la Caf kwa Afrika Mashariki iliyofika fainali ni Simba tu.

Kumbuka Mfulila ya Zambia walitufunga hapa nyumbani 4-0, Simba ikaenda kuwafunga mabao 5-0 kwao mbele ya Rais Kaunda. Sijui kama kuna timu imewahi kufanya hivyo Afrika au duniani kote.


SALEHJEMBE: Simba ilijulikana kama kiboko ya Waarabu, timu za Afrika Kaskazini zilikuwa na hofu zinapojua zinacheza na Simba, sasa si Simba ile, viongozi wa sasa hamlioni hilo kama tatizo au sehemu ya mliyofeli?
Manara: Huu ni upepo, unapita na sasa tunaanza kukaa vizuri, utaona timu inavyocheza na tulipo sasa. Kuhusu kiboko ya Waarabu natamani wangekuwepo watu wa Widad Casablanca (Morocco), Setif na El Harach (Algeria), Zamalek au Al Ahly (Misri), wote wanajua mziki wa Simba.

SALEHJEMBE: Kwa maneno yako, unataka kusema Simba ni wa kimataifa? Lakini inaonekana sasa wote ni watu mnaosema tu kujisifia. Au niwaite Simba ni wa kimataifa wa zamani na Yanga wa sasa?
Manara: Kwa lipi wawe wa sasa? Simba kukosa misimu hiyo michache basi iwe tofauti! Kwani Yanga wamefika wapi katika hiyo michuano ya kimataifa? Hata ukiangalia wachezaji waliowahi kucheza nje au walio nje wengi ni Simba. Achana na huyo Mbwana Samatta kwa sasa, rudi enzi za akina Athumani Machuppa lakini mwanzo kabisa rundo la wachezaji kama Nico, Deo Njohole hata mdogo wao Renatus Njohole.

 Wengine akina Kassim Matitu, George Kulagwa, Khalid Abeid, Haidar Omar Abeid, Martin Kikwa, Athumani Mambosasa. Njoo kwa kina Kihwelo Mussa, Iddi Pazi, George Masatu na wengine wengi sana.

Kama unakumbuka hata wakati wa kutangaza timu bora za karne, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), liliitangaza Simba kwa upande wa Tanzania. Sasa hao ndiyo wanaojua wa kimataifa ni akina nani, si kila mmoja anaropoka tu! Kama mtu anaweza, awabishie na Fifa.


 SOURCE; CHAMPIONI




3 COMMENTS:

  1. Manara dizaini kama unawaogopa YANGA

    ReplyDelete
  2. NAHISI NA WEWE SHABIKI WA SIMBA SIYO

    ReplyDelete
  3. Akili za Saleh Ally na Haji Manara zinafanana tofauti ni rangi tuu,wote walewale wa matopeni!Hakuna jipya hapo kwani umekopi kutoka blog ya Michuzi!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic