March 25, 2016



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) akizungumza na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam, juzi. Wa pili kushoto ni Rais wa TFF, Jamal Malinzi, Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine (kushoto), kulia ni bosi mwingine wa TFF, Juma Matandika na Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi.
PICHA: OFISI YA WAZIRI MKUU

Na Saleh Ally
MWANZONI mwa wiki hii, jopo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiongozwa na rais wake, Jamal Malinzi lilipata nafasi ya kwenda kumtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Jopo hilo, pia lilimjumuisha na Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine, Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi na wajumbe wengine akiwemo anayejulikana kwa cheo cha msaidizi wa Rais wa TFF, Juma Matandika.

Ukiiangalia picha ambayo inawaonyesha watu watano huku mmoja akiwa ‘amekatwa’ yaani haonekani. Katika wanne wanaoonekana, utamuona Malinzi akitupa macho kwenye kitabu ambacho ninaamini kilikuwa na mambo nyeti ya siku hiyo. Hali kadhalika, Mwesigwa na Madadi pia walikuwa na vitabu hivyo.

Matandika pekee, alikuwa na gazeti alilolikunja (inawezekana ni Championi), naye akiwa pamoja katika meza hiyo.
Kwanza nianze kumpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuonyesha kweli yeye ni mwanamichezo kwa kuwa ana taaluma ya ukocha. Mara kadhaa, nilikuwa nikijiuliza, lini ataingia na kukutana na wadau wa michezo. Wiki chache zilizopita alifanya hivyo, hongera sana tena.

Safari hii, ametoa heshima pekee kwa soka. Hata kama vyama vingine vitaitwa, tayari soka itakuwa ilipata heshima ya kutangulia kuitwa na Waziri Mkuu Majaliwa, ni jambo la kujivunia kabisa.

Wakati naiangalia picha hiyo, nikiwa nimevutiwa na nafasi hiyo na heshima kubwa waliyopewa wapenda soka. Nilianza kujiuliza maswali mengi kama binadamu wa kawaida ambaye nimeumbwa na tabia ya kuhoji kwa lengo la kujifunza zaidi.

Hivi Matandika alikuwa na ulazima wa kwenda pale? Sikupata jibu. Nikajiuliza tena, wakati wenzake wakiwa na vitabu kuonyesha watanakili mambo muhimu, vipi Matandika alikuwa na gazeti, tena kalikunja katika sehemu nyeti kama hiyo? Jibu likawa hakuwa sahihi.

Suala la nafasi ya kufika pale katika sehemu hiyo adimu, nikaanza kutamani kama wangeipata angalau wachezaji wakongwe au wastaafu kama Edibily Lunyamila, Bakari Malima, Zamoyoni Mogella, Oswald Morris ambao wengi walileta heshima katika nchi yetu lakini leo wanaonekana wapo tu.

Sitaki kuingia kwenye kundi la kwamba wengi “walichezea maisha”. Hilo haliwezi kuwa kigingi cha kuwafanya wasahaulike na inafikia nafasi muhimu kama hizo “zinachezewa”.

TFF ilialikwa, lakini naona kulikuwa na kila sababu kuamini Matandika ambaye ni msaidizi wa Malinzi angeweza kuwakilishwa na wengine ambao ni wadau wakubwa zaidi kwa kuwa kipi ambacho Matandika atakichukua na hawezi kukichukua Mwesigwa au Madadi.

Cheo cha msaidizi wa Rais wa TFF ni kipya, nafikiri ni ubunifu wa Malinzi. Najua kweli Matandika ni rafiki yake, nimeelezwa wametoka mbali ambalo ni jambo zuri, ikiwezekana wafike mbali zaidi. Lakini tunapoingia katika maendeleo ya mchezo wa soka na Malinzi na wenzake wakiwa wamepewa dhamana ya Watanzania, basi waitumie vizuri zaidi kwa maendeleo ya mchezo huo.

Inawezekana kabisa wakawa hawajakosea kwa kuwa Matandika ni kati ya wafanyakazi wa TFF, akifanya kazi ya kumsaidia Malinzi ambaye ana wasaidizi wengine ambao wangetosha bila hata ya Matandika.

Ninachoendelea kusisitiza hapa ni hivi; nafasi hiyo ingekuwa vizuri kumfikishia kiongozi huyo mkubwa wa nchi mambo muhimu kabisa kwa wakati mwafaka kwa kushirikisha wadau wengine ambao wako ndani au chini ya TFF.

Mfano, viongozi wa makocha, viongozi wa waamuzi ambao ingekuwa nafasi nzuri kupata mawili matatu kutoka kwa mkuu huyo ambaye ni mtu wa soka. Kuliko TFF kujazana huku wakijua kabisa wengine hawakuwa na sababu ya kwenda pale kama ambavyo hali halisi inaonyesha.

Naendelea kushikilia nilipo, kwamba siamini au sikubali kuwepo na suala la msaidizi wa rais wa TFF kwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za shirikisho hilo mali ya Watanzania.

Lakini pia nisisitize, ziara hiyo ya kwa Waziri Mkuu Majaliwa, nayo iwe sehemu ya picha kwamba kuna watu muhimu walio ndani ya TFF hawana nafasi, hawakumbukwi, hawathaminiwi na huenda kutodhaminiwa kwao kumezidi kutuporomosha kwa kuwa wamekuwa wakijisikia ni wapweke, hakuna anayewajali na huenda hakuna aliye tayari kuwasikiliza.

Hakuna asiyejua wachezaji kama Lunyamila, Bakari Malima, Mogella, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, Mohammed Mwameja, Iddi Moshi na wengine wengi wametoa mchango mkubwa katika mpira hapa nyumbani Tanzania.


Vizuri tukakubali kama kuna sehemu walikosea, lakini kuna mengi yalifanyika. Basi kuwe na nafasi kwao angalau kidogo hasa linapofikia suala la sehemu ya kusema ukweli, sehemu ya kutoa hisia zao kwa ajili ya kusaidia au kujumuishwa kwenye masuala mengine ya maendeleo kwa kuwa wasingejenga msingi, leo hii sisi tusingeweza kuezeka.

1 COMMENTS:

  1. Acha umbea na fitna za kisimbasimba wewe,kinakuuma nini mimi kuwepo katika kikao na waziri mkuu?kama wewe ulikuwa ni muhimu basi rais wa TFF angekualika ktk kikao kile!Mitanzania mingine kwa roho mbaya na chuki mmezidi!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic