March 25, 2016



Na Saleh Ally
NIMEKUWA nikiendelea kupata hoja nyingi ambazo zinazidi kunilazimisha niamini huenda suala la uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake limekuwa likiwafanya watu wengi sana wasiwe wenye kuamini kufikiri ni jambo jema.

Fikra sahihi humfanya mwanadamu kufanya mambo mengi mazuri, yenye usahihi na hata kama atakosea basi ana kila sababu ya kulenga mafanikio au kuanzishwa kwa jambo bora.

Kwetu Watanzania, hasa wale wanaopenda mchezo wa soka, wengi si watu wanaopenda kufikiri. Si watu wanaoamini kufikiri kabla ya kutenda au kuzungumza linaloweza kuwa jambo jema.

Huenda kufikiri bila kutafakari ili upate jambo sahihi, nako kunaweza kukawa hakutoshi pia. Mimi ninaamini kila mmoja ana akili alizopewa na Mwenyezi Mungu, lakini matumizi yake ndiyo husababisha mtu mmoja kuonekana ana akili na mwingine hana.

Pia bado siamini kwamba watu huwa hawana uwezo wa kufikiri kwa lengo la kuegemea tafakuri jadidi ili kupata uhakika wa kitu fulani. Uvivu wa kutotaka kuzitumia akili walizopewa zimekuwa ni tatizo.


Watu wengi wanaopenda soka, nimewaona mitandaoni wakijadili kuhusiana na lile sakata la Kocha Jackson Mayanja wa Simba na mchezaji Abdi Banda ambaye aligoma kupasha misuli wakati kocha huyo alipomuambia kufanya hivyo wakati Simba ikipambana na Coastal Union.

Banda alikataa kufanya hivyo kwa madai kwamba kocha alisema alitaka kumtoa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye alikuwa amepiga kona na krosi kwa ufanisi wa chini.

Huenda wanaojadili wanaona ni kama sifa, jambo ambalo liko wazi si hali nzuri kwa wachezaji wetu ambao baadaye tunawategemea kuwa uokovu wa taifa letu ambalo soka lake linamalizwa na migogoro ya kipuuzi.

Katika hali ya kawaida, kati yetu mimi na wewe nani hajui mchezaji anapoambiwa na mwalimu asimame na kupasha misuli akakataa ni kosa. 

Lakini mimi na wewe, kama kweli tunapenda soka nani asiyejua kocha ndiye mtu wa mwisho katika upangaji wa kikosi? Yupi asiyejua kocha ndiye anayeamua nani acheze kwanza, nani baadaye?

Vipi Banda anaweza kujua umuhimu wa kocha kutaka kumuingiza wakati fulani kuliko kocha mwenyewe? Hamuoni kama Banda analeta ushikaji ndani ya kazi?

Bado inashangazwa kama wewe unataka kukubali kwamba Banda ana huruma kwa Tshabalala kuliko Mayanja? Kwani ambaye amekuwa akimpanga Tshabalala katika mechi zote ni Banda au Mayanja?

Ninaona kama nitauliza hadi nitachoka na majibu yatakuwa magumu. Ukweli ni lazima tupevuke na kuonyesha tunaupenda mpira lakini tuwapende vijana wanaochipukia kwa kuwaeleza ukweli badala ya ushabiki wa kipuuzi ambao haulengi kuwajenga.

Bado ninaamini, huenda Mayanja alitaka kumuinua Banda apashe misuli kama kumpa ujumbe Tshabalala kutokana na makosa mfululizo. Jambo ambalo bado lingekuwa msaada kwa Tshabalala pamoja na Simba yenyewe.

Kama nilivyoeleza, kuendelea kumdanganya Banda kwamba alionewa ni kuendelea kummaliza kwa sifa za kijinga. Kuna mtu anahoji kwa kusema, “Vipi kila mara ni Mayanja tu!” wakati mwingine na mimi najiuliza huyu anayehoji, huenda anapaswa kujiuliza mara nyingi sana kabla ya kusema kila jambo.

Pia nimekuwa nina hofu na kikosi cha Simba, kwamba Kocha Dylan Kerr aliyeondoka aliingiza utamaduni wa Kingereza ambako watu wanajielewa zaidi akiamini hapa kwetu Tanzania watu wako hivyo.

Sasa Banda na wenzake, wanataka kuishi maisha ya Kerr katika utawala wa Mayanja. Niwe wazi, katika suala la nidhamu, nitamuunga mkono Mayanja mara zote.

Najua wako ninaowaudhi, huenda katika hili nitawaudhi zaidi na zaidi. Mwisho najua itakuwa msaada kwa Banda na wenzake hapo baadaye. 



1 COMMENTS:

  1. Kuna mkpno wa pembeni huwa tunapewa waandishi kutoka kwa baadhi ya walimu wa michezo(makocha) ili tuwapambe naamini hata wewe saleh badala ya kuwa jembe sasa unaanza kuwa shamba la kulimiwa na hao makocha.Hivi vijisenti visitufanye sisi waandishi tukadharau kazi yetu na kujiingiza katika utamaduni wa akupae ndiye aandikwae vizuri,tuwe makini.
    Banda ni kijana wa kitanzania na ni lazima tumlinde kama walivyo waingereza wanavyowalinda akina Handerson japo mpira wenyewe wanabahatisha!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic