March 28, 2016


Na Saleh Ally
TAKRIBAN mwaka mmoja sasa niliandika makala kali kumkosoa kiungo nyota wa Simba, Jonas Mkude ambaye alikuwa gumzo wakati huo kutokana na mkataba wake.

Pamoja na kupewa fedha nyingi, Mkude alipewa gari aina ya Toyota Grande Mark II uzao GX 110. Kwa kijana kama yeye aliyetokea maisha duni au ya kawaida kama mimi, lilikuwa ni jambo kubwa na la kushitukiza.

Mkude amekulia kisoka ndani ya Simba, hakuwa amewahi kuona utamu wa usajili kama huo. Inaonyesha ilimchanganya na sasa akataka awe nyota wa mtaa badala ya uwanjani.

Kwa wale wenye kumbukumbu, wanakumbuka namna kiwango chake kilivyoanza kuporomoka kwa kasi, hadi kufikia kutemwa kikosi cha Taifa Stars.

Kwa makocha wa Simba, hakuwa muhimu sana na huenda kikawa chanzo cha Mkude kutemwa katika kikosi cha Taifa Stars.

Niliamua kuandika makala kwa kuwa mara kadhaa nilimuona Mkude katika baa moja eneo la Kijitonyama, kila nilipopita. Wakati mwingine nikahisi ni bahati mbaya. Lakini kwa kuwa ni mtu wa kupenda kujiridhisha, nikaendelea kupita eneo lile mara kwa mara na nilimuona zaidi na zaidi.

Nilianza kujiuliza anapumzika muda upi, vipi saa zote mchezaji aonekane baa? Tena mchezaji kinda kama yeye ambaye anapaswa kujituma, kujilinda na kuelekeza nguvu nyingi katika kazi badala ya starehe.


Nikataka nipate jibu sahihi kupitia kiwango chake na kadiri siku zinavyosonga mbele, kiwango kikaanza kuporomoka kwa kasi kubwa. Nikawa nimejiridhisha kwamba ni wakati mwafaka wa ‘kumtungua’.

Lengo lilikuwa ni kumjenga na kumsaidia, lakini katikati wakatokea wale watu ‘wenye akili chache’, ambao wanaamini kusema ni jambo rahisi kuliko yote duniani na hawajui kauli nzuri lazima ihakikiwe kwenye ubongo kwa kuitafakari na mwisho kuzungumza.

Wakaanza kulaumu kuwa kaonewa, wakalaumu kuwa anasakamwa. Wengine wakasema: “Tuachie Simba yetu”.
Hawa wanaosema “tuachie Simba yetu” ndiyo adui wakubwa wa maendeleo ya soka nchini. Maana huwa hawaangalii hata kidogo umuhimu wa nidhamu, uwezo wa kujali malengo badala yake wanajali starehe ya mioyo yao.

Nilipokutana na Mkude mara ya kwanza ikiwa ni takriban miezi mitatu au minne tangu nimuandikie ile makala, alinisalimia vizuri sana na hakukuwa na ishara yoyote ya mtu aliyenuna au kukasirishwa. Nikajua alinielewa.
Baada ya hapo, Mkude ameanza kurudi taratibu. Huenda wapo waliomsaidia zaidi baada ya kuona makala yangu. 


Hakika sasa ni mtu aliyebadilika kwa kuwa nimepita zaidi ya mara 10 kwenye ile baa muda wa mchana sijamuona, wala sijabahatika tena kukutana naye akiendesha gari lake akiwa amevua shati utafikiri anaendesha roli la mchanga.
Umesikia Simba imekutwa na utovu wa nidhamu mfululizo, ile ishu ya Isihaka Hassan, baadaye ishu ya Abdi Banda. 

Utaona hadi Hamisi Kiiza ambaye ni mkubwa kwa vijana hao alishindwa kuwaongoza, naye akaingia ‘kichwakichwa’ na kuzungumza maneno ya kipuuzi kabisa. Uongozi wa Simba ukamtaka kukanusha, ajabu akasingizia eti iliandikwa kwenye magazeti, ambao ulikuwa ni uzushi mwingi. Lakini yote hayo, Mkude hukumsikia.

Hapa utagundua Mkude amebadilika, sasa anaangalia mbele pia ni mtu wa kupongezwa kwa kuwa ameamua kusikiliza na kuyafanyia kazi matatizo au makosa yake.

Watanzania wengi hatupendi kuelezwa ukweli, anayekueleza unataka umtishe jambo ambalo ni ujinga mwingine. Lakini kwangu, namuona Mkude ni mtu bora zaidi kwa kuwa amegundua kuna tatizo, kalifanyia kazi na anaanza kurejea na kuonyesha ubora wake.

 Kwa uchezaji wake wa sasa, hakuna shaka utategemea kusikia timu za nje zinamhitaji. Au kusikia Yanga, Azam FC zimeanza kutupa ndoano.


Lakini haitakuwa ajabu tena kusikia Simba inahaha kumuongezea mkataba mpya aendelee kubaki kwa miaka mingine mitatu au minne.

Uchezaji wake umeimarika, anaonekana uwanjani yuko makini, ana malengo, hataki utani na mtu mwenye msaada kwa kikosi cha Simba na sasa Taifa Stars.
Sijaandika makala haya ‘kumpasua kichwa’ kwa sifa, badala yake kuonyesha ukisikiliza wenye nia nzuri na wewe, unabadilika na kufanikiwa. Bravo Mkude.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic